STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, July 11, 2015

Man United yamtambulisha rasmi Memphis Depay

Meneja wa Manchester United Louis van Gaal Leo huko Old Trafford Jijini Manchester alimtambulisha rasmi Mchezaji mpya Memphis Depay mbele ya Wanahabari katika Mkutano maalum na pia kuthibitisha Mchezaji wa Kimataifa wa Italy Matteo Darmian anaelekea England kukamilisha Uhamisho wake kutoka Torino.
Hata hivyo, Van Gaal alikataa kuzungumza lolote kuhusu habari za kuuzwa kwa Mholanzi mwenzake Robin van Persie kwa Klabu ya Uturuki Fenerbahce.
Akijibu swali kuhusu kuuzwa kwa Van Persie, Van Gaal alisema: "Tukihisi anapaswa kwenda, utasikia toka Manchester United. Kwa sasa bado."
Alipohojiwa kuhusu mipango yao ya Uhamisho na kama inakwenda kama walivyotarajia, Van Gaal alikataa kusema kwa undani na badala yake kueleza: "Huwezi kujibu hilo kwani kununua na kuuza ni kitu kinachoendelea na hatujafika mwisho wake. Mwisho ni Agosti 31. Hatuwezi kusema lolote kuhusu Uhamisho wetu, mikakati yetu kwani nyie mtaandika kila kitu."
Aliongeza: " Manchester United haiwezi kununua kwa sababu ya kununua tu. Ukinunua lazima iwe ni kitu bora kuliko ulichonacho."
Nae Memphis Depay, mwenye Miaka 21 na alienunuliwa Mwezi uliopita kutoka PSV Eindhoven ya Holland Klabu aliyoisaidia kuwa Mabingwa Msimu uliopita huku yeye akiwa ndie Mfungaji Bora wa Ligi, alisisitiza amejiunga na Manchester United ili kutwaa Vikombe vyote vinavyowezekana na yeye atajituma hadi mwisho.
Depay aliongea: "Hii ni Klabu kubwa Duniani na hivyo ni lazima nicheze kwa ajili ya Vikombe. Nimekuja kushinda Vikombe."
Alipoulizwa kuhusu kufanana na Cristiano Ronaldo aliejiunga Man United akiwa na Miaka 18, Depay alieleza: "Sitaki kujifananisha na Mtu kama yeye. Cristiano Ronaldo ni mmoja wa Wachezaji bora Duniani na sitaki kusema sana, nitaachia Miguu yangu iongee!"

No comments:

Post a Comment