STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, September 20, 2012

IJUE HISTORIA YA NGUMI ZA KULIPWA UBINGWA WA AFRIKA MASHARIKI NA KATI (ECAPBF) ULIVYOANZA MWAKA 1983‏



LEO tumeona ni vyema kuwakumbsha Watanzania na wapenzi wa ngumi kwa ujumja ili kuweka kumbukumbu sahihi za taarifa  kuhusu masuala ya ngumi za kulipwa na ambazo tunafurahi kuwa zimeanza kutolewa na bwana Yasin Abdallah (Ustaadh), tungependa pia kuwapa maelezo sahihi kuhusu ubingwa wa Ngumi za Kulipwa wa Afrika ya Mashariki na Kati.

Ubingwa huu umekuwa unapigiwa kelele na baadhi ya watu ambao wana malengo ya kuharibu taswira nzima ya nguni za kulipwa na kuturudisha nyuma kwenye enzi za vurugu zilizowahi kutokea hapo nyuma.

Ubingwa wa Ngumi za Kulipwa wa nchi za Afrika ya Mashariki na Kati ulianzishwa mwaka 1983 katika jiji la Nairobi nchini Kenya.

Mpaka kufikia wakati huo (1983) ni nchi ya Tanzania pekee iliyokuwa imeshaanzisha ngumi za kulipwa katika ardhi yake ambapo Kenya na Uganda zilikuwa bado hazijaanzisha ngumi za kulipwa nchini mwao japokuwa zilikuwa na mabondia kadhaa waliokuwa wanacheza ngumi za kulipwa katika nchi za Ulaya na Asia.

Mabondia wa Kenya waliokuwa wanacheza ngumi za kulipwa nje ya nchi yao wakati huo walikuwa ni pamoja na Steven Muchoki na mdogo wake Michael Irungu, waliokuwa wanapigana ngumi nchini Denmark chini ya Promota maarufu Mogens Palle. 

Mabondia wengine wa Kenya waliokuwa wanapigana ngumi za kulipwa nje ya Kenya walikuwa ni pamoja na Modesti Napunyi Oduor, Isayah Ikoni na Philip Warwinge waliokuwa wanazipiga nchini Japan.

Aidha mabondia wa Uganda waliokuwa wanacheza ngumi nje ya nchi yao waliongozwa na Ayub Kalule, John Odhiambo, Mustapha Waisaja, John Mugabi (The Beast), John Rubin Byaruhanga na Cuban Businge ambao wote pia walikuwa chini ya promota maarufu Mogens Palle wa Denmark.

Kwa upande Tanzania bondia pekee aliyekuwa anacheza ngumi za kukipwa nje ya nchi wakati huo alikuwa Gerald Isaac (Tanzania’s Devil kama wapenzi wa ngumi na vyombo vya habari vya Marekani walivyokuwa wanamwita kwa ajili ya ukali wake kwenye masumbwi ulingoni) aliyekuwa anazichapa nchini Marekani.

Tarehe 18 mwezi wa Juni liliandaliwa pambano la kwanza la aina yake kwa ubingwa mpya kabisa wa Afrika ya Mashariki na Kati lililofanyika katika ukumbi wa mikutano ya kimataifa jijini Nairobi (Kenyatta International Conference Center, KICC).

Waandaji wa mpambano huo walikuwa ni pamoja na DS Njoroge wa kampuni maarufu ya ngumi wakati huo DS Boxing Promotions ya jijini Nairobi nchini Kenya, Joe Akech ambaye wakati huo alikuwa ndiye Meneja Mkuu wa Kanda wa shirika la ndege la Marekani, Pan American Airlines (Pan Am) na David Attan na mkewe Linda Brown Attan wa kampuni ya Davlin Boxing Promotions ambaye baadaye alikuja kuwa Promoter wa bondia Onesmo Ngowi. 

Joe Akechi alikuja kuwa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Kenya (KPBC) na Meya wa Jiji la Nairobi.

Mpambamno huo wa kugombea mkanda wa Bantamweight uliwakutanisha mabondia wawili ambao walikuwa wanatamba sana katika nchi zao katika miaka ya 1980!.

Bondia Onesmo Alfred Ngowi (Piston Mover) wa Tanzania alikuwa ameshawapiga mabondia wote waliokuwa tishio kwenye uzito wake wa bantamweight wakiwa ni pamoja na Musa Mwabata, Sasi Sarungi, Ali Mohammed, Antoni Nyembela, Pius Lwandalla na David Migeke.

Kwa upande wa Kenya Modest Napunyi Oduor (Babaa) alikuwa ndiye bondia aliyekuwa anatamba sana kwa wakati huo na ndio tu alikuwa anatokea nchini Japan alikokuwa anapigana ngumi za kulipwa.

Wawili hao (Ngowi na Oduor) walikutana katika mpambano wa kwanza kabisa wa Afrika ya Mashariki na Kati tarehe 18 Juni 1983 katika ukumbi wa Kenyatta International Conference Center (KICC) na kugombea mkanda wa kwanza wa Afrika ya Mashariki na Kati.

Katika mpambano huo mabondia wengine kutoka Kenya (Steven Muchoki, Athumani, na Michael Irungu) Uganda (Cuban Businge) Tanzania (Clement Chacha, Emmanuel Kimaro na Fidel Haynes) nao walipanda ulingoni kusindikiza pambano hilo la kihistoria ambalo lilianzisha ngumi za kulipwa katika nchi za Kenya na Uganda kwa mara ya kwanza.

Mwamuzi wa mpambano huo wa ubingwa wa Afrika ya Mashariki na Kati alikuwa Emmanuel Mlundwa wa Tanzania wakati huo akiwa ndiye Rais wa Boxing Union of Tanzania (BUT) iliyokuja kubadili jina na kuwa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC) mwaka 2000.

Miaka 21 baadaye mwaka yaani 2004, Kamisheni za Ngumi za Kulipwa za Kenya (Kenya Professional Boxing Commission, UPBC), Uganda (Uganda Professional Boxing Commission, UPBC na Tanzania Professional Boxing Commission, TPBC zilikutana mjini Moshi na kuunda rasmi Shirikisho la Ngumi za Kulipwa la Afrika Mashariki na Kati (East & Central Africa Professional Boxing Federation au ECAPBF.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na Marais wa Kamisheni hizo tatu Celestino Mindra (UPBC) Memba Muriuki (KPBC) na Onesmo Ngowi (TPBC) uliweka uongozi mpya wa Shirikisho la ECAPBF kama ifuatavyo:

Onesmo Ngowi (Tanzania) – Rais
Celestino Midra (Uganda) - Makamu wa Kwanza wa Rais
Memba Muriuki (Kenya) - Makamu wa Pili wa Rais
Shaaban Ogola (Kenya) Katibu Mkuu wa ECAPBF
Nemes Kaviehe (Tanzania) Mweka Hazina Mkuu wa ECAPBF
Paul Chiwa (Uganda) Afisa Uhusiano na habari Mkuu wa ECAPBF
Imetolewa na:
Uongozi
ECAPB

No comments:

Post a Comment