STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, December 5, 2012

Tanzania kubeba maombi AFCON 2017



Na Sanula Athanas
RAIS wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), Leodegar Tenga amesema kuwa wamejipanga kutuma maombi ya kuandaa fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2017 huku akiipa nafasi kubwa Tanzania kuwa moja ya nchi zitakazoandaa.
Tenga, ambaye pia ni rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya shirikisho hilo jijjini Dar es Salaam jana.
"Kuna kitu ambacho tunakifanya kuhusu kuandaa michuano hiyo, kitakapokamilika tutawataarifu. Tanzania ina nafasi kubwa ya kuwa moja ya nchi zitakazoandaa michuano hiyo kutokana na miundombinu iliyopo na mapenzi ya soka miongoni mwa watu wake,” alisema Tenga bila kubainisha kitu kipi hasa wanakifanya.
Hata hivyo, taarifa kutoka Kenya zinaeleza Waziri wa Michezo na Vijana wa nchi hiyo, Ababu Namwamba alisema mwezi uliopita kuwa viongozi wa soka wa nchi za Uganda, Kenya na Tanzania walipanga kukutana Kampala, Uganda wakati wa michuano inayoendelea ya Kombe la Chalenji kuzungumza kutuma maombi ya kuandaa kwa pamoja AFCON 2017.
Waziri huyo alikaririwa na vyombo vya habari nchini humo akisema: “Tunasikitika kushindwa kutuma maombi ya kuandaa mashindano makubwa kutokana na miundombinu mibovu. Tunahitaji kuwekeza kwenye miundombinu ya michezo ili kuwa kwenye nafasi nzuri ya kuandaa mashindano makubwa,” alisema.
Kenya haijawahi kuandaa michuano mikubwa tangu iandae mashindano ya All African Games mwaka 1987. Tanzania yenye uwanja wa kisasa wa Taifa wa Dar es Salaa unaoweza kuchukua watu 60,000, ‘inazipiga fimbo’ nchi jirani za Kenya na Uganda.

UFAFANUZI WA WARAKA
Katika hatua nyingine, Tenga alisema sababu ya kuwaandikia wanachama wa TFF waraka wa kuwaomba wapitishe mabadiliko ya katiba ya shirikisho hilo badala ya kusubiri idhini hiyo kwenye Mkutano Mkuu wa Dharura, ni tatizo la ukosefu wa fedha.
Tenga alisema ni kweli kwamba walipaswa kuitishia mkutano wa dharura ili kupitisha mabadiliko hayo lakini TFF haina fedha ya kuitisha mkutano huo ambao hugharimu hadi Sh. milioni 110.
Alisema mabadiliko hayo ni maagizo ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) na kwamba wasipoyatekeleza, Tanzania haitaruhusiwa kushiriki michuano yoyote ya kimataifa kuanzia mwakani.
Nahodha huyo wa zamani wa timu ya taifa (Taifa Stars), alisema baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF wakiwamo wa mkoa wa Kagera wamepinga hatua hiyo huku Pwani wakihitaji ufafanuzi zaidi kabla ya kupitisha waraka huo.
“Tumetuma waraka kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF ili waturuhusu kufanya marekebisho ya katiba yetu. Tunatambua kwamba tulipaswa kuitisha Mkutano Mkuu wa Dharura ili wajumbe wakae na kupitisha, lakini hali yetu kiuchumi siyo nzuri,” alisema Tenga.
“Kwa miaka saba iliyopita tulikuwa tunatumia kati ya Sh. milioni 90 hadi 110 kuandaa kila Mkutano Mkuu wa TFF. Pesa iliyopo kwa sasa inatosha Mkutano Mkuu mmoja tu ambao ni wa Uchaguzi Mkuu.
“Endapo agizo hili la FIFA tungeliipata mapema, tungelizungumza katika mkutano uliopita, lakini tulipata taarifa Julai mwaka huu,” alisema.
Rais huiyo pia alizipongeza timu za taifa za Kilimanjaro Stars na Zanzibar Heroes kwa kuingia hatua ya nusu fainali katika michuano inayoendelea ya Kombe la Chalenji.

Chanzo: NIPASHE
   

No comments:

Post a Comment