STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, January 9, 2013

Mrisho Ngassa, John Bocco wainogesha Stars

Ngassa na Bocco wakipongezana


 
WASHAMBULIAJI Mrisho Ngassa wa Simba na John Bocco ‘Adebayor’ wa Azam ni miongoni mwa nyota zaidi walioripoti katika kambi ya timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) itakayosafiri leo jioni  kwenda jijini Addis Ababa, Ethiopia kucheza mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya wenyeji keshokutwa Ijumaa.
Awali, Bocco, Ngassa, kipa Juma Kaseja na wachezaji wengine kadhaa walioitwa Stars kutoka katika klabu za Simba na Azam walishindwa kuripoti katika kambi ya timu hiyo kwavile walikuwa na klabu zao kwenye michuano inayoendelea visiwani Zanzibar ya Kombe la Mapinduzi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema kuwa nyota kutoka Simba, Azam na Mtibwa wameungana na wenzao na kwamba sasa Stars itasafiri leo ikiwa na kikosi chenye wachezaji wengi zaidi miongoni mwa wale walioutwa na kocha wao Mdenmark, Kim Poulsen.
Mbali na Bocco, Ngassa na Kaseja, wachezaji wengine walioitwa Stars kutoka Simba, Azam na Mtibwa ni Shomari Kapombe, Amri Kiemba, Amir Maftaha, Mwinyi Kazimoto, Salum Aboubakar 'Sure Boy', Mwadini Ali, Mcha Khamis, Aggrey Morris,  Erasto Nyoni, Aishi Manula na nyota Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ na Shabani Nditi kutoka Mtibwa Sugar,
"Stars inaondoka leo huku ikiwa kamili baada ya nyota wengi kuripoti kambini," alisema Wambura.
Alisema timu hiyo itarejea jijini Dar es Salaam baada ya kumalizika kwa mechi dhidi ya Ethiopia na kuendelea na kambi yao kujiandaa kwa mechi nyingine mbili za kirafiki, zote zikiwa ni sehemu ya maandalizi kabla ya mechi ya kuwania kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia dhidi ya Morocco itakayochezwa Machi.

No comments:

Post a Comment