STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, February 23, 2013

YANGA, AZAM NI VITA TUPU LEO TAIFA


KLABU zilizopo kileleni mwa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Yanga na Azam leo zinatarajiwa kukutana katika pambano ambalo ni sawa na 'vita' katika mfululizo wa ligi hiyo.
Timu hizo zitakwaruzana kwenye mechi itakayochezwa jioni ya leo kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam huku kila mmoja ikiwania ushindi ili kujihakikisha kukalia kiti cha uongozi kwa raha.
Yanga ndiyo inayoongoza msimamo wa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa, ikilingana kwa pointi 36 na wapinzani wao Azam waliotangulia mbele kwa mchezo mmoja zaidi.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa mkali kutokana na ukweli kuwa timu zote zimeonyesha viwango vya juu kwenye michezo ya ligi kuu na zote zimekuwa zikifanya vizuri kwenye michezo hiyo.
Ubora wa kila kikosi ni mzuri kiasi kikubwa kwamba umetia hofu kila kocha wa timu hizo.
Akizungumza jana kocha Ernest Brandts wa Yanga alisema mchezo wa leo utakuwa mgumu kwao hasa kutokana na uwezo wa Azam walioonyesha kwenye michezo ya ligi kuu mzunguko huu wa pili.
Aidha alisema timu hiyo ya wauza vyakula ina morali ya juu baada ya kushinda mchezo wake wa Kombe la Shirikisho la klabu za Afrika dhidi ya Al Nasri Juba ya Sudan Kusini.
"Mchezo hautakuwa rahisi... kwangu nategemea mchezo mgumu na wenye upinzani kwa sababu naamini timu zote zipo kwenye kiwango cha juu kwa sasa," alisema Brandts.
Aidha, alisema kuwa kikosi chake kipo tayari kwa ajili ya mchezo wa leo na amepata nafasi ya kuiangalia Azam kwenye baadhi ya mechi zake hivyo anjua nini cha kufanya hili kujiwekea mazingira ya ushindi.
Kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza, Azam ambayo imeshinda mechi zake zote nne za duru la pili lililoanza mwezi uliopita, ilifungwa kwa magoli 2-0 na Yanga kwenye uwanja huo wa Taifa.
Kocha wa Azam, Stewart Hall, amesema Yanga ni timu nzuri lakini wapo tayari kukabiliana nayo.
"Wana wachezaji wazuri na wanacheza kitimu lakini ukiangalia hata sisi (Azam) tuna wachezaji wazuri na timu imekuwa kifanya vizuri hivyo hakuna cha kutuogopesha," alisema Hall.
Hata hivyo, Azam inaweza kuwa kwenye wakati mgumu hasa kutokana na safu yake ya ulinzi kutokuwa kwenye kiwango cha juu hasa baada ya kuwasimamisha Aggrey Moris, Said Moradi na Erasto Nyoni waliokuwa wakiunda ukuta wa timu hiyo.
Lakini Azam kama ilivyo Yanga inajivunia safu kali ya ushambuliaji inayoongozwa na Kipre Tchetche ambaye amefunga magoli 10 kwenye ligi huku Yanga ikimtegemea Jerry Tegete mwenye magoli manne katika mechi tatu za ligi zilizopita.

No comments:

Post a Comment