STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, March 5, 2013

Hatma ya Lyon kesho Chamazi, Ligi Kuu ikiendelea




NA BONIFACE WAMBURA
HATMA ya African Lyon kuendelea kushika mkia au la kwenye Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inajulikana kesho wakati itakapokuwa mwenyeji wa Ruvu Shooting kwenye Uwanja Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam.
Lyon yenye pointi 13 kutokana na mechi 19 inabidi iifunge Ruvu Shooting kama inataka kuirejesha mkiani Toto African yenye pointi 14. Kama kweli inazitaka pointi zote tatu itabidi ifanye kazi mbele ya Ruvu Shooting inayotiwa makali na Kocha Charles Boniface Mkwasa.
Hiyo itakuwa mechi ya 18 kwa Ruvu Shooting inayoshika nafasi ya saba ikiwa na pointi 26 ikitanguliwa na vinara wa ligi hiyo Yanga, Azam, Simba, Coastal Union, Kagera Sugar na Mtibwa Sugar yenye pointi 28 ikinolewa na nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Mecky Maxime.
Mechi hiyo namba 139 itachezeshwa na mwamuzi Amon Paul kutoka Musoma wakati wasaidizi ni Anold Bugado wa Singida na Milambo Tshikungu kutoka Mbeya. Mwamuzi wa mezani atakuwa Shafii Mohamed wa Dar es Salaam.
Nayo Tanzania Prisons ya Jumanne Chale itakuwa mgeni wa Oljoro JKT katika mechi itakayochezwa Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha wakati Mgambo Shooting itaoneshana kazi na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Keshokutwa (Machi 7 mwaka huu) Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya JKT Ruvu ya Kocha Charles Kilinda na Kagera Sugar.
Ligi hiyo itaendelea tena Jumamosi ya Machi 9 mwaka huu kwa mechi mbili; Yanga vs Toto Africans (Uwanja wa Taifa), na Azam vs Polisi Morogoro (Azam Complex, Chamazi).

 

No comments:

Post a Comment