STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, March 5, 2013

TFF YAIPONGEZA AZAM KUSONGA MBELE AFRIKA


NA BONIFACE WAMBURA
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa timu ya Azam ya Tanzania Bara kwa kufanikiwa kusonga mbele katika michuano ya Kombe la Shirikisho iliyo chini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Ushindi wa jumla ya mabao 8-1 ambao Azam imeupata dhidi ya Al Nasir Juba ya Sudan Kusini si fahari kwa timu hiyo tu, bali Tanzania kwa ujumla, na unaonyesha jinsi klabu hiyo ilivyojipanga kiushindani katika michuano hiyo ya Afrika.
Hata hivyo, ni vizuri Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo, benchi la ufundi na wachezaji wa timu hiyo wakautazama ushindi huo kama changamoto kwao kuhakikisha wanajipanga vizuri zaidi kwa raundi inayofuata.
Timu ya Azam inayofundishwa na Mwingereza John Stewart Hall ilishinda nyumbani mechi ya kwanza mabao 3-1, na juzi kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 ugenini jijini Juba.
Kwa kufanikiwa kuing’oa Al Nasir Juba, Azam sasa watacheza raundi ya kwanza (raundi ya 16 bora) ya michuano dhidi ya Barrack Y.C.II ya Liberia ambayo katika raundi ya awali iliitoa Johansens ya Sierra Leone. Barrack ilishinda bao 1-0 nyumbani katika mechi ya kwanza na kulazimisha suluhu katika mechi ya marudiano jijini Freetown.
 
Azam itaanzia mechi hiyo ugenini kati ya Machi 15,16 na 17 mwaka huu wakati mechi ya marudiano itachezwa Tanzania kati ya Aprili 5,6 na 7 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment