STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, April 23, 2013

Mariam Mndeme: Mwanahabari, muigizaji aliyewageukia walemavu

Mamuu akiwa na Baby Madaha
MWENYEWE anasema japo hana muda mrefu tangu ajitose kwenye fani ya uigizaji akiiweka kando taaluma yake ya uanahabari, lakini anashukuru fani hiyo imempa mafanikio makubwa ya kujivunia ambayo yanazidi kumtia nguvu ili asonge mbele zaidi.
Mariam Khamis Mndeme maarufu kama 'Mamuu', mmoja wa waigizaji wanaozidi kujua juu nchini kutokana na kipaji kikubwa alichonacho katika fani hiyo aliyoanza kuitumikia tangu akiwa kinda, anasema wala hajutii kujitosa kwenye fani hiyo aliyoipenda tangu alipokuwa kinda.
Msanii huyo aliyewahi kuwa mtangazaji wa TBC na kuyaandikia magazeti ya Global Publishers, anasema mbali na kufahamiana na kupata rafiki wengi, fani ya uigizaji imemfanya pia amudu maisha kwa kujiingizia kipato na kupanua upeo wake kiakili na kisanii.
Mariam anasema kupanuka kwake kisanii ndiko kulikomfanya afyatue filamu zake binafsi mbili za 'Pooja' na 'Tatakoa' badala ya kuendelea kuzitumikia kazi za wengine, japo anakiri kwamba safari yake kuyaendea mafanikio zaidi bado ni ndefu kwa malengo aliyojiwekea ya kujitangaza kimataifa.
"Siyo siri fani ya uigizaji imenisaidia kwa mengi kiuchumi na kimaisha kwa ujumla, kwani mbali na kuyamudu maisha pia niliwahi kumiliki Pub iliyokuwa ikiitwa Mamushka kabla ya kuachana na biashara hiyo na kujikita kwenye shughuli nyingine ninazoendelea nazo kwa sasa," anasema.
Anasema baada ya kupakua filamu yake binafsi ya kwanza iitwayo 'Pooja' kwa sasa amekamilisha kazi nyingine iitwayo 'Tatakoa' ambayo anajiandaa kuitoa hadharani hivi karibuni huku akijiandaa kuondoka nchini kwa ziara ya karibu mwezi mzima katika nchi nne tofauti za Afrika.
Ziara hiyo ataifanya mwezi ujao kwenda katika nchi za DR Congo, Zimbabwe, Angola na Msumbaji kwa ajili ya maonyesho ya muziki na filamu ambapo yeye ataenda kama mratibu, lakini pia akishirikiana na wasanii atakaoambatana nao akiwamo Baby Madaha.

Mamuu katikati nyuma akiwa na wasanii wenzake walipokuwa wakirekodi filamu ya Tatakoa

KAOLE
Mariam  aliyezaliwa mwaka 1980 akiwa  mtoto wa nne kati ya watano wa familia yao yenye asili ya kabila la Kipare, anasema sanaa ya maigizo aliipenda tangu akiwa mdogo akivutiwa zaidi na kundi la 'Mambo Hayo' kabla ya mwenyewe kuja kujitosa rasmi miaka ya katikati ya 2000.
Anasema pamoja na kuonyesha kipaji shule, lakini alikidhirisha alipojiunga na kundi la Kaole Sanaa kabla ya kujitosa jumla kwenye filamu hasa baada ya kuhitimu Stashahada yake ya Habari aliyoipata kupitia katika Chuo cha DSJ, akishiriki kazi mbalimbali zilizomtangaza vyema.
Baadhi ya filamu alizocheza kisura huyo anayependa kula chakula chochote kizuri na kunywa juisi halisi na bia kidogo, ni pamoja na 'Bestfriend',  'Fake Pastor', kabla ya kutoa filamu binafsi ya 'Pooja' aliyoitaja kama bora kwake,kisha kufuatiwa na 'Dirty Game', 'Ghost Love' na sasa 'Tatakoa'.
Shabiki huyo wa klabu za Simba na Manchester United, nanayechizishwa na rangi nyeusi, njano na nyekundu, anasema hakuna tukio la furaha kwake kama alipotengeneza filamu zake binafsi za Pooja na Tatakoa na kuhuzunishwa na vifo vya babu na baba mzazi vilivyotokea kwa nyakati tofauti.
"Siyo siri nilikuwa nampenda sana babu yangu kipenzi Mzee Msinga, kifo chake kiliniumiza na kinaniuma mpaka sasa kama kilivyokuwa cha baba yangu mzazi," anasema.



Mamuu (kushoto) akiwa na wasanii wenzake
WALEMAVU
Mariam ambaye hajaolewa japo tayari anaye mtoto wa kiume aitwaye Steve Moses, anasema pamoja na mipango ya kuliteka soko la filamu nchini na kujitangaza kimataifa, akiota ndoto za kuja  kumiliki kampuni ya kuzalisha filamu na kusaidia chipukizi wwnye vipaji, pia anatarajia kunzishaa kipindi maalum cha runinga kwa ajili ya kuwasaidia watoto walemavu wakiwamo maalbino.
Kimwana huyo, mchumba wa kijana aitwaye 'D', anasema kipindi hicho kitawamulika na kuripoti taarifa mbalimbali za watoto walemavu na maalbino wanaoishi maeneo ya vijijini ambao wamepoteza matumaini kutokana na hali walizonazo na kusahauliwa na jamii.
Anasema kusudio kubwa la kipindi hicho mbali na kufungua milango ya kuwasaidia, pia kina lengo la kuwatia nguvu na kuwapa matumaini kutokana na hali ya kukata tamaa kutokana na maisha wanayoishi na kuathiriwa na hali alizonazo  hasa maalbino ambao wamekuwa wakiuwawa.
"Natarajia kuja na kipindi maalum cha runinga kwa ajili ya kufichua maovu wanayofanyiwa walemavu na hasa wenye matatizo ya ngozi, kitakuwa maalum cha kuwatia moyo na kufungua milango ya kusaidiwa na jamii, ili wafarijike na kuishi kwa uhuru kama watu wengine," anasema.
Mariam anasema kipindi chake hicho ambacho hajajua kitarushwa katika kituo gani, kinawezeshwa kwa msaada mkubwa wa mmoja wa Mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Nne ambaye hakupenda kumtaja jina kwa sasa, pamoja na Wema Isaac Sepetu, muigizaji anayemzimia na mmoja wa wasanii wanaojitolea kuwasaidia wenzake kwa hali na mali.

Mamuu akipozi kwa kusoma gazeti
"Ninapigwa tafu na watu hao wawili yaani Mhe Waziri na Wema Sepetu ndiyo wanaonipiga tafu, ili kufanikisha mipango ya kipindi hicho maalum cha kuwasaidia walemavu," anasema Mariam.
Mariam anawataka wasanii wenzake kupendana, kushirikiana na kuwa wabunifu ili kufanya kazi ziwe na soko la uhakika ndani na nje ya nchi, huku akiwashauri kupenda kujaribu kutoa kazi zao binafsi badala ya kuendelea kutumikishwa tu.
Msanii huyo ambaye anayeiomba serikali kuwapa sapoti wasanii ili waweze kusonga mbele na kunufaika na fani yao, anasema kama asingekuwa muigizaji au mwanahabari, angejishughulishana biashara, fani anayoifanya hata sasa wakati akiendelea na fani yake ya uigizaji.

No comments:

Post a Comment