STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, April 23, 2013

Yanga kutetea taji lake la Kagame Ethiopia

Yanga walipokuwa wakishangilia taji lao la Kagame mwaka jana

MASHINDANO ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati maarufu Kombe la Kagame mwaka huu yanatarajiwa kufanyika Juni jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Mabingwa watetezi wa michuano hiyo ni vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga ambao watataka kuweka rekodi ya kutwaa kimoja taji hilo iwapo watafanikiwa kulitetea mwaka huu.
Yanga ilitwaa taji hilo mara mbili mfululizo michuano hiyo ikifanyika Tanzania kwa kuwalaza Simba kwa  bao 1-0 katika fainali za mwaka juzi na mwaka jana waliizima Azam kwa 2-1.
Hata hivyo, Shirikisho la Soka la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limesema kwamba mashindano hayo yanaweza kufanyika katika nchi nyingine itakayokuwa tayari kufuatia Ethiopia kueleza katika barua yao kwamba wanataka michuano hiyo ifanyike mwezi Septemba.
Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye, aliiambia NIPASHE kwa njia ya simu kuwa bado suala la udhamini wa michuano hiyo limekuwa tatizo na ndiyo maana wanashindwa kueleza wazi mikakati ya michuano hiyo ya mwaka huu.
Musonye alisema kwamba ili mashindano hayo yafanyike katika ubora wake wa kimataifa, CECAFA inahitaji kiasi cha Dola milioni moja za Marekani.
"Tuko katika kutafuta wadhamini na hadi kufikia mwisho wa mwezi huu tutajua ni nani hasa atakuwa mwenyeji wa michuano hii kwa kuthibitisha kwamba ataweza kuhudumia mahitaji yanayotakiwa. Uenyeji kwa sasa ni wa Ethiopia japo michuano inaweza pia kuhamishiwa katika nchi nyingine," alisema Musonye.
Aliongeza kuwa mashindano ya Kombe la Kagame ni muhimu katika ukanda huu na hayatafanyika zaidi ya mwezi Julai hivyo kama mwenyeji atashindwa kuwa tayari kwa muda huo, michuano inaweza kuhamishwa huku wakiendelea kusaka wadhamini.
Awali nchi za Sudan na Rwanda ziliandika barua ya kuomba kuwa wenyeji wa michuano hiyo ya kila mwaka lakini bado vyama vya soka vya nchi hizo havijathibitisha kama vimeshapata udhamini wa kusaidia gharama za maandalizi.
Yanga ndiyo bingwa mtetezi wa michuano hiyo ambapo pia mwaka huu Simba itashiriki kutokana na kuwa bingwa wa Tanzania Bara msimu uliopita.

CHANZO:NIPASHE


No comments:

Post a Comment