STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, May 12, 2013

Kagera Sugar ndiyo basi tena, Azam yahitaji pointi moja kutinga CAF


Ruvu Shooting

Kagera Sugar
SARE ya bao 1-1 iliyopata Kagera Sugar nyumbani dhidi ya Ruvu Shooting imeihakikishia waliokuwa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba kumaliza kwenye Tatu Bora ya ligi ya msimu huu.
Kagera waliokuwa wamekalia nafasi ya tatu kwa muda mrefu kabla ya kuenguliwa na Simba hivi karibuni imepoteza matumaini ya kocha wake, Abdallah Kibadeni aliyeapa mwanzoni mwa msimu kuwa ni lazima amalize kwenye Tatu Bora msimu huu kama moja ya mikakati yake alipojiunga na timu hiyo.
Timu hiyo iliyosaliwa na mechi moja kabla ya kufunga msimu kwa sare ya jana imefikisha pointi 41 na hata ikishinda mechi ya mwisho itafikisha pointi 44 ambazo zimeshapitwa na Simba yenye pointi 45 na mchezo mmoja mkononi.
Katika mechi ya jana kwa mujibu wa Afisa habari wa Ruvu Shooting, Masau Bwire, Kagera ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 14 lililofungwa na Daud Jumanne kabla ya timu yake kusawazisha dakika 11 baadaye kupitia Juma Mdindi na kudumu hadi wakati wa mapumziko.
Katika kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko ya wachezaji na kushambuliana kwa zamu licha ya kutoweza kuongeza bao lolote na kuzifanya zigawane pointi moja moja.
Ligi hiyo itaendelea jioni ya leo kwa pambano moja tu kati ya waliokuwa wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho, Azam dhidi ya Mgambo JKT pambano litakalochezwa Chamazi, jijini Dar.
Azam inahitaji sare yoyote kuweza kufikisha pointi 49 ambazo hazitaweza kufikiwa na Simba na kukata tiketi nyingine ya kushiriki michuano hiyo ya Shirikisho mwakani.
Azam wana pointi 48 na imesaliwa na mechi moja baada ya pambano wakatalocheza leo, ambapo mbio zao za kuwania ubingwa zilikatishwa na Coastal Union waliowalazimisha sare ya bao 1-1 na kuipa Yanga ubingwa kilaini bila yenyewe kushuka dimbani.
Yanga waliotwaa taji hilo kwa mara ya 24 tangu kuanza kwa Ligi Kuu mwaka 1965 imejihakikishia kitita cha Sh Milioni 70 kutoka kwa wadhamini wa Ligi hiyo kampuni ya mtandao wa simu za mkononi, Vodacom na kukata tiekti ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Azam iwapo itanyakua nafasi ya pili itavuna kitita cha Sh. Milioni 35 na Simba tayari wana hakika ya kubeba Sh Mil 25 kwa kujihakikishia nafasi ya tatu.
Ligi hiyo itafikia tamati Jumamosi ijayo ambapo timu zote 14 zinazoshiriki ligi hiyo zitashuka dimbani, huku jicho na sikio la mashabiki likisubiri kwahamu pambano la watani Simba na Yanga litakalochezwa kwenye uwanja wa Taifa.

No comments:

Post a Comment