STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, May 3, 2013

Kiporo cha Simba, Ruvu Shooting kupigwa J'pili Taifa


Na Boniface Wambura
LIGI Kuu ya Vodacom (VPL) inaendelea Jumapili (Mei 5 mwaka huu) kwa mechi moja tu ya kiporo kati ya  Ruvu Shooting dhidi ya Simba itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10.15 jioni.

Hiyo itakuwa mechi ya raundi ya 24 kwa timu hizo ambapo Simba iko nafasi ya nne ikiwa na pointi 39 nyuma ya mabingwa Yanga wenye pointi 57, Azam yenye pointi 48 na Kagera Sugar ambayo ina pointi 40. Ruvu Shooting iko katika nafasi ya saba ikiwa na pointi 31.

Pambano hilo awali lilikuwa lichezwe Aprili 25, lakini likaahirishwa dakika za lala salama kutokana na uwanja huo wa Taifa kutumiwa na serikali kwa maandalizi ya sherehe za Muungano zilizofanyika siku iliyofuata kwenye uwanja wa Uhuru unaoendelea kutengenezwa.

Hadi sasa mabao 348 yameshafungwa katika ligi hiyo huku Yanga ikiongoza kwa kufunga 45. Polisi Morogoro yenye pointi 22 katika nafasi ya 12 ndiyo iliyofunga mabao machache ikiwa nayo 13 tu.

African Lyon yenye pointi 19 katika nafasi ya mwisho ndiyo inayoongoza kwa kuwa na kadi nyingi. Timu hiyo inayofundishwa na Charles Otieno ina kadi 44 ambapo kati ya hizo nne ni nyekundu. Mtibwa Sugar ya Manungu, Turiani mkoani Morogoro yenyewe inaongoza kwa kuwa na kadi nyingi nyekundu ambapo hadi sasa inazo saba.

No comments:

Post a Comment