STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, June 28, 2013

Golden Bush, Chuo Veterani kumaliza ubishi kesho Mlimani

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjv1SWGpAVVh3AeFAONPcqAEhha3BStjvn0YNGauB0GUtXNqJi_5DzbDbFPasom9XhppZgtV61Wt3Tx5XDUuOYbqCg2Y_fAaCiqjp8Kgx8gkWVdVA2RrALkRqpPNAZ5t_EpMpEJpL_xt04/s1600/Golden.JPG
Kikosi cha Golden Bush Veterani ambacho kesho asubuhi kinatarajiwa kuvaana na Chuo Kikuu Veterani
BAADA ya tambo za muda mrefu kutoka kwa wachezaji wa timu mbili zenye upinzani za Golden Bush Veterani na Chuo Kikuu Veterani, mzizi wa fitina unatarajiwa kukatwa rasmi kesho wakati zitakaposhuka dimbani viwanja vya Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) kupambana.
Timu hizo zimekuwa zikitupiana vijembe vya hapa na pale kwamba ni lazima mmoja kesho alie, huku Golden Bush ambayo mlezi wake aliyewahi kung'aa na timu ya Chuo Kikuu Veterani akiwachimba mkwara wapinzani wake kwamba kesho wakisalimika basi kipigo kitakuwa kama walichopewa Tahiti mbeleya Hispania katika michuano ya Kombe la Mabara inayoendelea nchini Brazili.
Mlezi na msemaji huyo, Onesmo Waziri 'Ticotico' anayetarajiwa kuongoza safu ya ushambuliaji ya timu yake asubuhi ya kesho, alisema kikosi chao kipo imara na kimejiandaa vyema kwa pambano hilo baada ya wikiendi iliyopita kutamba kwenye Bonanza maalum Jimbo la Ukonga kwa kutwaa taji.
"Tunapenda kuwafahamisha wapenzi wa soka kwamba siku ya jumamosi tarehe 29 June viwanja vya Chuo kikuu cha Dar ES salaam kutakuwa na patashika ambapo wapinzani wa jadi Golden Bush na Chuo veterans wataumana kuanzia saa moja na nusu asubuhi," alisema Ticotico na kuongeza;
"Ni mechi ambayo mpenzi wa soka hutakiwi kukosa kwasababu timu zote zitachezesha vikosi vya kwanza kabisa. Maandalizi yamekamilika kwa asilimia 100 na timu zote ziko tayari kwa mpambano huo," alisema.
Mshambuliaji huyo matata, alisema makocha wao, Madaraka Seleman 'Mzee wa Kiminyio' na Herry Morris 'Ng'onyi' tayari wamekiweka hadharani kikosi chao kitakachoshuka dimbani kuwaadhibu Chuo ambapo alisema golini atakaa nyota wa zamani wa Yanga, Steven Marash, shavu la kulia atasimama Salum Swedi 'Kussi', kushoto Faraj Salum 'Kipara' huku halfback four atasimama John Mwansasu na mkoba Wisdom Ndhlovu.
"Namba sita atacheza Godfrey Bonny 'Ndanje' na winga wa kulia atacheza yeye 'Ticotico', na namba nane atasimama Salum Athuman 'Mbududu', mkali wa zamani wa Jangwani, na mshambuliaji wa kati atacheza Kudura Omar, huku Inside 10 Omary Mgonja na winga wa kushoto itamilikiwa na Abuu Ntiro.
Ticotco alisema wachezaji wa akiba watakaowapokea wenzao ni wakali zaidi kuliko hata watakaolianza pambano hilo na kuhimiza mashabiki wajitokeze kwa wingi kuona wanavyowatoa nishai wapinzani wao ambao nao wamejitutumua na kutamba kwamba hawana maneno zadi watafanya kazi moja tu ya kuzima ndoto za Golden Bush Veterani.

No comments:

Post a Comment