Yanga iliyoanza kwa kishindo Dar |
Ashanti United waliotunguliwa mabao 5-1 |
JKT Ruvu walioshinda ugenini jijini Tanga |
Simba waliong'ang'aniwa na Rhino Rangers |
Kagera Sugar waliotoshana nguvu na Mbeya City |
JKT Oljoro walilala mabao 2-0 mbele ya Coastal Union |
PAZIA la Ligi Kuu Tanzania Bara limefunguliwa jioni ya leo kwa kushuhudiwa mabingwa watetezi, Yanga kuikaribisha kwa kipigo cha aibu Ashanti Utd, huku watani zao Simba waking'ang'aniwa ugenini na 'wageni' wa ligi hiyo Rhino Rangers mjini Tabora.
Yanga ikiwa kwenye uwanja wa Taifa iliishindilia Ashanti kwa mabao 5-1, wakati Simba iliyokuwa ikiongoza kwa mabao 2-1 ilijikuta wakizembea na kulazimishwa sare ya 2-2 na Rhino.
Mabao ya Yanga katika mechi hiyo yalifungwa na Jerry Tegete aliyefunga mawili, Simon Msuva, Haruna Niyonzima na Nizar Khalfan.
Mjini Tabora kwenye uwanja wa Ali Hassani Mwinyi, Simba ilipata mabao yake kupitia Jonas Mkude, wakati Rhino walipanda daraja walipata mabao yao kupitia Imani Noel na Soud Kipanga.
Katika mechi nyingine Coastal Union ikiwa jijini Arusha ilionyesha ilivyopania msimu huu kwa kuilaza JKT Oljoro kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Abdul Banda kwa shuti la mita 40 na Mkenya Crispian Odulla.
Nao Azam wakiwa ugenini Manungu kuumana na Mtibwa Sugar ililazimisha sare ya 1-1 wakisawazisha bao kwa mkwaju wa penati ya Aggrey Morris baada ya kutanguliwa kufungwa na Juma Liziwa.
Maafande wa JKT Ruvu wakiwa ugenini mjini Tanga waliishindilia Mgambo JKT kwa mabao 2-0, huku Ruvu Shooting wakipata ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Prisons Mbeya.
Nao wageni wengine wa ligi hiyo, Mbeya wakiwa nyumbani uwnaja wa Sokoine walilazimisa sare ya bila kufungana dhidi ya Kagera Sugar inayonolewa na Jackson Mayanja.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena siku ya jumatano kwa michezo kadhaa mabapo Simba itasafiri kuifuata Oljoro jijini Arusha, huku Ruvu ikielekea Mbeya kuwakabilia wenyeji wao Mbeya City.
No comments:
Post a Comment