STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, November 1, 2013

Azam, Mbeya City kuendeleza rekodi zao Bara kesho

Azam


Mbeya City
MECHI za raundi ya 12 ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) zinatarajiwa kuendelea tena kesho kwenye viwanja vinne tofauti, huku mashabiki wa soka wakitaka kujua kama Azam na Mbeya City ambazo ndizo pekee hazijapoteza mchezo mpaka sasa zitavuna nini?
Mbali na kuendeleza rekodi pia iwapo timu hizo zitashinda mechi zake hizo zitaiengua Yanga kileleni na kuiporomosha hadi nafasi ya tatu na zenyewe kurejea kwenye uongozi huo wakisubiri mechi za kufungia dimba la duru la pili katikati ya wiki ijayo.
Azam waliokuwa wakiongoza msimamo wa ligi hiyo mpaka jioni hii kabla ya Yanga kuwashusha yenyewe itaikaribisha Ruvu Shooting kwenye uwanja wa Chamazi, huku wapinzani wao, Mbeya City nao watakuwa dimba la nyumbani Sokoine kuialika Ashanti United.
Michezo hiyo ni migumu kwa timu zote nne, lakini kwa kasi ya Azam na Mbeya City ni wazi Ashanti na Ruvu watakuwa na kibarua kizito cha kuweza kudhibitisha kuwa wao nao ni kiboko iwapo watazisimamisha timu hiyo katika viwanja hivyo.
Afisa Habari wa Ruvu Shooting, Masau Bwire aliiambia MICHARAZO kwamba kesho wanataka kuweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza msimu huu 'kuwatengua udhu' Azam kwenye uwanja wa Chamazi, kwa madai wamejiandaa vya kutosha kupata ushindi.
Bwire alisema kikosi chao kipo imara japo itaendelea kumkosa kiungo mkabaji wao, Juma Seif Kijiko ambaye alionyeshwa kadi nyekundu katika pambano baina ya timu yao na Ashanti United lililoisha kwa sare.
Ruvu imesema wakali wao kama Elias Maguri, Cosmas Ader, Stephen Mwasyika, Said Dilunga na wengine wapo tayari kuwazima Azam ambao wenyewe wamenukuliwa kupiotia meneja wao Jemedari Said kwamba wanataka kumaliza mechi za duru la kwanza wakiwa kileleni mwa msimamo ili kutimiza ndoto za kuja kuwa mabingwa wapya nchini.
Mechi nyingine za kesho ni kati ya Mgambo JKT itakayoumana na 'majirani' zao Coastal Union katika pambano linalosubiriwa kwa hamu litakalochezwa kwenye uwanja wa  Mkwakwani, Tanga huku Mtibwa Sugar ya Morogoro itaialika Rhino Rangers ya Tabora katika dimba la Manungu, Morogoro.
Siku ya Jumapili kutakuwa na mechi moja tu itakayowakutanisha 'Wajelajela' Prisons ya Mbeya itakayoikaribisha timu ya Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Katika mechi zao mwisho, Prisons ililala mabao 2-0 mbele ya Mbeya City wakati Oljoro ililazimishwa suluhu na Ashanti United.
Mechi za kufungia duru la kwanza zitaanza kuchezwa Novemba 6 kwa pambano kati ya Jkt Ruvu dhidi ya Coastal Union, Ashanti United dhidi ya Simba, Kagera Sugar kuwa wenyeji wa Mgambo JKT na Ruvu Shooting kuumana na Mtibwa Sugar.
Siku inayofuata yaani Novemba 7, Azam itacheza na Mbeya City uwanja wa Chamazi, huku mabingwa watetezi Yanga itaikaribisha Oljoro JKT na Rhino Rangers itakuwa dimba la nyumbani kuikaribisha Prisons ya Mbeya.

No comments:

Post a Comment