STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, November 12, 2013

Said Ndemla: Kinda la Simba lililoifunika Yanga Okt 20

 
YANGA ilipokuwa ikiongoza kwa mabao 3-0 katika kipindi cha kwanza cha pambano lao dhidi ya watani zao, Simba lililochezwa Oktoba 20 mwaka huu hakuna aliyekuwa akiamini kama mabao hayo yangerudishwa na Simba.
Hii ni kwa sababu Yanga ilitawala mchezo huo na kuifunika kabisa Simba na hasa 'dimba' la kati na kuifanya Simba ya King Abdallah KIbadeni kuonekana siyo lolote wala chochote mbele ya vijana wa Jangwani wa Ernie Brandts.
Hata hivyo badiliko lililofanywa na Kibadeni kwa kumtoa Abdulhalim Humud 'Gaucho' na Haruna Chanongo na kuwaingiza William Lucian 'Gallas' na Said Ndemla, lilileta maajabu ya aina yake kwenye uwanja wa Taifa.
Simba iliwafunika Yanga na kurejesha mabao yote matatu na lau kama dakika zingeongeshwa zaidi katika pambano hilo ni dhahiri Simba ingeibuka na ushindi kwa vile ilionekana kupata uhai na kuwakimbiza Yanga watakavyo.

Unajua kwa nini?
Moja ya 'mashine' zilizoingizwa, iliwafunika nyota wote wa Yanga waliotawala awali  dimba la kati, akikaba vilivyo na kusukuma mashambulizi ya Simba langoni mwa wapinzani wao kiasi mabeki ya Yanga kutamani mpira uishe.
Said Khamis Ndemla ndiye aliyekuwa akifanya kazi hiyo na kuwafanya wale wote walioikatia tamaa Simba kupata uhai na hasa Simba ilipoanza kurudisha bao moja baada ya jingine na hatimaye kusawazisha bao na kuwa mabao 3-3.
Ndemla, chupukizi ambaye hilo lilikuwa pambano lake la kwanza kubwa kwa wapinzani wa jadi Simba na Yanga, alifanya kazi ambayo ilithibitisha kuwa Tanzania imejaliwa hazina kubwa ya vipaji vya soka iwapo vikitumiwa vyema.
Hata mwenyewe anakiri itamchukua muda mrefu kulisahau pambano hilo kwa namna alivyocheza kwa jihad na kusaidiana na wenzake kulazimisha sare ya mabao 3-3 wakati tayari Simba ilionekana imekubali kuelekea 'Kibla'.


"Siwezi kulisahau pambano la Simba na Yanga kwa sababu lilikuwa pambano langu la kwanza kubwa na gumu lenye ushindani na la kwanza kwangu kati ya Simba na Yanga na bahati nzuri niling'ara," anasema.
Ndemla, anayevutiwa na soka la kiungo wa Ujerumani anayeichezea klabu ya Bayern Munich, Bastian Schweinsteiger anasema anaamini kujiamini na kipaji alichojaliwa kilimbeba na kumfanya awe anafanya mambo makubwa dimbani.
Mkali huyo ambaye licha ya kumudu nafasi ya kiungo pia anamudu kucheza kama winga wa kulia na mshambuliaji namba 10, anasema anashukuru Mungu kwa kipaji alichonacho na kuota kuja kucheza soka la kulipwa barani Ulaya.
"Licha ya kufurahia kuichezea Simba, lakini ndoto zangu ni kuja kucheza nje ya nchi na hasa bara la Ulaya, naamini ninao uwezo mkubwa," anasema.
 

DALILI NJEMA
Ndemla aliyezaliwa Machi 11, 1994 jijini Dar es Salaam akiwa ni mtoto wa pili kati ya watoto wanne wa familia ya Mzee Khamis Ndemla, anasema licha ya kucheza kitambo kifupi, lakini soka limempa mafanikio ya kujivunia.
Anasema ukiacha mambo binafsi ambayo hakupenda kuyaanika gazetini, lakini tayari ameshanyakua mataji na medali kadhaa katika mchezo huo.
"Kwa kipindi kifupi tu nimeshanyakua vikombe vitatu na medali nikiwa na Simba B. Nimetwaa nao ubingwa wa Uhai, Kinesi na ule wa ABC Super8," anasema.
Anasema mafanikio hayo ni dalili njema kwake katika usakataji wake wa soka huku akisisitiza kuwa hajaridhika wala kuvimba kichwa na badala yake atazidisha juhudi ili aweze kufika mbali zaidi.
Kabla ya Simba kumuona, Ndemla aling'ara katika soka akisoma Shule ya Msingi Uzuri na Makongo, huku chandimu alicheza Soccer Rangers iliyokuza kipaji chake kabla ya kunyakuliwa na Messina Linea na baadaye Red Coast.
"Nikiwa naichezea Red Coast kwenye michuano ya Kinesi, ndipo Simba B waliponiona na kunishawishi kujiunga nayo nikianzia katika kikosi hicho kabla ya kupandishwa timu ya wakubwa," anasema.
Ndemla, anasema Simba ilivutiwa naye hasa baada ya kuifungia timu yake ya Red Coast mabao 2-0 dhidi yao na kumsajili kikosi chake cha vijana alichoichezea msimu miwili kabla ya mwaka huu kupandishwa timu kubwa.
Mchezaji huyo anayekiri kama siyo soka anmgependa kuwa mfanyabiashara anasema hakuna tukio la furaha kwake kama siku Simba iliponyakua ubingwa wa Super8 na kulizwa na kifo cha baba yake mzazi.
"Kwa kweli huzuni yangu ni kumpoteza baba yangu mzazi na furaha ni siku nilipotwaa ubingwa wa Super8 kwa kuwanyuka Mtibwa Sugar," anasema.

VIJANA
Ndemla anayependa kula kunywa ugali kwa samaki na mboga za majani na kunywa juisi ya matunda, anasema soka la Tanzania linazidi kupanda juu na kutaka vijana wapewe zaidi nafasi akiamini watalikomboa taifa kimataifa.
Anasema vijana wakipewa nafasi itawasaidia kujiamini na kupigana kwa mafanikio ya taifa kama mataifa mengine yaliyosonga mbele na kutamba katika soka la kimataifa kwa kutegemea nguvu ya vijana wenye vipaji.
Shabiki huyo wa Chelsea, hata hivyo anawakumbusha wachezaji wenzake kuzingatia nidhamu, kujituma na kuwasikiliza makocha wao iwapo wanataka kufika mbali na kulingana na nyota wanaowashabikia wanaotamba duniani.
"Bila nidhamu, kujituma na kuwaizngatia makocha ni vigumu kufikia kwenye malengo, pia ikumbukwe soka la sasa ni ajira," anasema.
Ndemla anayependa kutumia muda wake wa ziada kupumzika nyumbani na kusikiliza muziki akimzimia Diamond, anasema hakuna mchezaji yeyote nchini anayemnyima raha awapo dimbani kwa vile anajiamini.
Kiungo anayefurahia tukio la kwenda kujifunza soka nchini Ujerumani akiwa na kituo cha TSS cha Mwanza anasema anawashukuru wazazi wake kwa kumuunga mkono katika kucheza kwake soka na hasa mama yake.
Pia anawamwagia sifa na pongezi makocha wake wote waliomsaidia katika kukuza soka lake tangu utotoni mpaka sasa hasa Ramadhani Kipira, Max, Suleiman Matola, Ngongo na Abdul Mashine.

No comments:

Post a Comment