STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, December 18, 2013

Coastal Union kwenda Oman kuinolea makali JKT Oljoro

 
MABINGWA wa zamani wa kandanda nchini, Coastal Union ya Tanga wanatarajiwa kuondoka nchini Januari mosi kuelekea Oman kwa ajili ya kuweka kambi ya kuajindaa na duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara.
Aidha kikosi hicho hakikusajili mchezaji yeyote katika dirisha dogo lililofungwa mwishoni mwa wiki badala yake imewapandisha wachezaji watano kutoka kikosi chao cha vijana cha U20 kilichotwaa ubingwa wa Kombe la Uhai.
Ofisa Habari wa klabu hiyo, Hafidh Kido aliiambia MICHARAZO kuwa timu yao itaondoka na msafara wa watu wasiopungua 30 wakiwamo wachezaji 26 na viongozi watano akiwamo kocha wao mkuu mpya, Yusuph Chipo.
Kido alisema Coastal inaenda Oman kwa ajili ya kuweka kambi ya wiki mbili wakiwa chini ya wenyeji wao klabu ya Fanja inayoshiriki Ligi Kuu ya nchini humo.
"Kwa sasa Coastal tupo katika maandalizi ya ziara yetu ya kambi ya wiki mbili nchini Oman kwa mualiko wa klabu ya Fanja na tukiwa huko tutacheza mechi tatu ambazo tutapangiwa na wenyeji wetu," alisema Kido.
Alisema miongoni mwa wachezaji watakaokuwa katika msafara huo ni vijana watano waliopandishwa katika kikosi cha kwanza kutoka timu ya U20 iliyotwaa taji la Uhai 2013 baada ya kuwalaza vijana wa Yanga katika fainali iliyochezwa hivi karibuni.
Kido alisema mara wakirejea nchini moja kwa moja watakuwa wakikabiliana na JKT Oljoro katika pambano la fungua dimba la duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara.
Coastal ambayo ilimaliza duru la kwanza ikiwa katika nafasi ya nane kwa kujikusanyia pointi 16 chini ya kocha Hemed Morocco waliyemtema na kumnyakua Mkenya Yusuf Chipo atakayeanza kibarua akiwa ughaibuni.

No comments:

Post a Comment