STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, December 18, 2013

Meshack Abel asikitika kuikosa Simba


BEKI wa kati wa zamani wa Simba, Meshack Abel ameelezea kusikitishwa kwa kuikosa fursa ya kurejea kuchezea klabu hiyo ya Msimbazi.
Abel alikuwa katika mazungumzo na klabu ya Simba ili kurejea kikosini akitokea Bandari ya Kenya anakocheza soka la kulipwa kwa sasa, lakini mipango hiyo ilikufa kutokana na kubanwa na mkataba alionao na klabu yake hiyo ya Mombasa na Simba ikamsajili Donald Musoti kutoka Gor Mahia.
Akizungumza na MICHARAZO kutokea nchini Kenya, Abel anayetarajiwa kurejea nchini leo kwa mapumziko, alisema anasikitika kukosa nafasi ya kurejea tena Msimbazi, kwani alikuwa na hamu ya kuja kucheza soka nyumbani.
Hata hivyo, beki huyo aliyewahi kuzichezea timu za African Lyon, Ashanti United na Moro United, alisema ana matumaini ya kurejea kucheza nyumbani msimu ujao kwani mkataba wake na Bandari unakaribia kumalizika.
Abel alisema mkataba wake umebakisha miezi sita tu kabla ya kuisha na kudai kilikuwa kikwazo kunyakuliwa na Simba iliyokuwa ikisaka beki wa kati ya kuwasaidia mabeki waliopo sasa klabuni hapo, Joseph Owino na Gilbert Kaze.
"Mkataba wangu umesalia miezi sita na ulifanya mambo yasiende kama nilivyotarajia kutua Simba, lakini naamini msimu ujao nitarejea kucheza nyumbani baada ya kucheza nje kitambo tangu nije hapa Kenya," alisema.
Abel alikuwa akikipiga Bandari na Watanzania wengine akiwamo kiungo Mohammed Banka aliyerejea Tanzania na kujiunga Ashanti United, David Naftar na mshambuliaji nyota, Thomas Mourice waliosalia nchini humo.

No comments:

Post a Comment