STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, December 26, 2013

Je, wewe ni mlaji wa 'Kitimoto? Ebu soma hapa...!

Nyama ya nguruwe.
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimehadharisha walaji wa nyama ya nguruwe nchini, kuwa wanakabiliwa na hatari ya kupata kifafa.
Utafiti wa kisayansi uliofanywa na SUA, umebaini kuwa baadhi ya nguruwe wana minyoo aina ya tegu ambao nyama yao ikiliwa bila kuiva vizuri, mlaji atapata minyoo hiyo ambayo huingia kichwani na kusababisha kifafa.
Akizungumza na mwandishi hivi karibuni, Mhadhiri na Mtafiti wa Idara ya Sayansi ya Wanyama na Uzalishaji ya SUA, Profesa Faustine Lekule, alisema sampuli za utafiti huo kutoka Mbeya, zimebaini nguruwe wengi wakiwamo wanaosafirishwa katika miji mikubwa wameathirika na minyoo hiyo.
Kwa mujibu wa Profesa Lekule, wataalamu wa SUA wanaosimamia Mradi wa Utafiti wa Kuboresha Ufugaji wa nguruwe kwa mkoa wa Mbeya ili kuinua pato la kaya, unaofadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la  Denmark (DANIDA), walibaini hatari hiyo baada ya kuchukua sampuli ya nyama ya nguruwe kwa ajili ya vipimo.
“Majibu ya sampuli ambazo wataalamu wamezichukua kutoka kwa nguruwe wa wafugaji kwenye baadhi ya vijiji, wamebainika kukumbwa na hatari hii.
“Lazima jitihada za makusudi zichukuliwe katika kutafuta ufumbuzi wa pamoja wa tatizo hili kati ya watafiti na Serikali,” alisema Profesa Lekule.
Alisema maambukizi ya tegu au minyoo ya nguruwe yanatokana na tabia za baadhi ya wafugaji kutozingatia ufugaji bora kwa kuwaacha kujitafutia chakula na maji mitaani na kula kinyesi cha binadamu.
Kwa mujibu wa Profesa Lekule, baadhi ya wafugaji  wamekuwa wakijisaidia vichakani na kuwaacha  nguruwe kutafuta malisho katika vichaka na kula kinyesi chao, hali inayochangia ongezeko la maambukizi ya minyoo ya tegu hao.
Baada ya kula kinyesi minyoo humwingia  mwilini na kumdhoofisha na baadaye binadamu anapokula nyama ambayo haijaiva vizuri, minyoo hiyo humwingia na kusababisha kifafa baada ya kuingia kichwani.
Alisema athari za kuenea kwa maambuziki hayo inaweza kutokea katika miji mikubwa ikiwamo Dar es Salaam kwa kuwa  nguruwe wa Mbeya husafirishwa na kuuzwa maeneo hayo.
“Hatua hii inaweza kusababisha kusambaa kwa ugonjwa huu,  hivyo ushirikiano kati ya wafugaji, wafanyabiashara, Serikali na wataalamu wa afya katika kufikia hatua ya kumaliza changamoto hii unahitajika,” alibainisha Profesa Lekule.
Ziro99
 
NB:Licha ya vitabu vya dini kukataza ulaji wa nyama ya Nguruwe bado nyama hiyo imekuwa na walaji wengi bila kujali madhara mbali na kule kukiuka amri ya Mungu kama anavyoelekeza katika Biblia kupitia vitabu vya Kumb ya Torati na Kutoka na hata kwenye Qur'an kunakobainishwa dhahiri nyama hiyo ni haramu mpaka mzoga wake.

No comments:

Post a Comment