STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, February 2, 2014

Huyu ndiye Ali Badru: Straika aliyekimbia vurugu Misri akiamini Simba itampeleka Ulaya


Ali Badru akiwajibika uwanjani
 KAMA siyo vurugu za kisiasa zilizoibuka miaka miwili iliyopita nchini Misri na kusababisha kusimamishwa kwa ligi ya nchi hiyo baada ya tukio la fujo zilizoua mashabiki zaidi ya 70, huenda mshambuliaji mpya wa Simba, Ali Badru asingerejea nchini.
Mchezaji huyo alikuwa akiichezea klabu ya Al Canal (El Qanah) kabla ya kurejea hivi karibuni na kujiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili.
Badru anasema alikuwa ametoka kuisaidia timu hiyo kupanda Ligi Kuu, lakini vurugu na kusimamishwa kwa ligi kwa muda kuliwafanya wachezaji wakose la kufanya huku kiuchumi wakiyumba na kuona bora arejee nyumbani.
"Kwa kweli nisingerejea mapema nyumbani kama siyo vurugu zilizopo Misri zilizotishia amani na kule kusimamishwa kwa ligi ya nchi hiyo (tayari inaendelea kwa sasa), kazi yangu ni soka hivyo sikuona sababu ya kubaki huko," anasema.
Nyota huyo wa zamani wa Jamhuri-Pemba, anasema hajutii uamuzi wa kurudi nyumbani kwa sababu amejiunga na klabu bora aliyoiota tangu utotoni, akiamini itamsaidia kucheza soka la kulipwa Ulaya.
Anasema mfumo wa Simba wa kuruhusu nyota wake wanaopata timu nje ya nchi unamfanya aamini ndoto zake za kucheza Ulaya zitatimia.
"Nimefurahi kutua Simba klabu ninayoipenda tangu utotoni, ina mfumo mzuri wa kuwapa nafasi wachezaji wake kwenda nje, itanisaidia  kutimiza ndoto za kucheza Ulaya," anasema.
Anaongeza hali ya ushindani aliyokutana nayo Simba katika kuwania namba inazidi kumfanya afurahi kwa kuamini itamjenga zaidi kisoka.
Badru anayeichezea timu ya Taifa ya Zanzibar 'Zanzibar Heroes', anasema ndani ya Simba hakuna mchezaji mwenye namba ya kudumu hivyo kufanya kila mchezaji muda wote kuongeza bidii ili wasiachwe nyuma, akimsifu pia kocha Zdravko Logarusic  kwa ufundishaji wake uliotukuka na unaotaka nidhamu zaidi.
"Ushindani upo Simba, unajua hii ni klabu kubwa kila mchezaji anataka nafasi ili ajitangaze, hivyo inavutia na kutufanya wachezaji tusibweteke," anasema.


FURAHA
Badru aliyevutiwa kisoka na mshambuliaji wa zamani wa klabu anayoishabikia ya Arsenal anayeichezea kwa sasa Manchester United, Robin van Persie anasema hakuna tukio la furaha kwake kama aliposajiliwa Al Canal ya Misri ikiwa daraja la kwanza na kuipandisha Ligi Kuu.
Anasema fursa ya kucheza nje imemfanya ajifunze mambo mengi ikiwamo kuona tofauti ya mfumo wa soka kati ya Tanzania na Misri hasa namna ya kuthaminiwa kwa wachezaji.
"Kwa kweli kucheza kwangu soka la kulipwa Misri ni jambo la furaha kama ninavyofurahia sasa nikiwa Simba," anasema.
Badru anayependa kutumia muda wake wa ziada kupunga upepo ufukweni na kubadilishana mawazo na rafiki zake, anasema hakuna tukio la simanzi kwake kama kifo cha mdogo wake kilichotokea akiwa mdogo.
"Mpaka leo nikikumbuka tukio hilo naumia sana, nilimpenda sana mdogo wangu," anasema.
Badru anayelitaja pambano lao la mwisho la kuwania kupanda Ligi Kuu Misri na kushinda bao 1-0 kuwa ndilo gumu kwake, anasema anashukuru soka kumsaidia kwa mengi kimaisha na kiuchumi.
"Siwezi kukufuru, soka limenisaidia mengi ikiwamo kuitunza familia yangu, na kusafiri nchi mbalimbali kwa sababu ya mchezo huo," anasema.
Mkali huyo anayemudu pia nafasi ya kiungo, anawataka wachezaji wenzake kujituma, kuwa na nidhamu nje na ndani ya uwanjani na kutambua soka ni ajira yao hivyo waiheshimu ili waweze kufika mbali kimaisha.
Badru anawaomba viongozi wa FA na klabu kuwajali na kuwathamini wachezaji pamoja na kuwezesha maandalizi mazuri kwa timu zao ili kufanya vyema kwenye michuano inayoshiriki.
"Viongozi wakifanya maandalizi mazuri na kuwatimizia mahitaji wachezaji wao ipasavyo, ni rahisi timu kufanya vizuri, pia wazingatie kuwekeza kwenye soka la vijana," anasema.


LIGI
Badru aliyezaliwa mwaka 1990 mjini Pemba, alianza kucheza soka tangu akisoma Shule ya Msingi na klabu yake ya chandimu ni Finya Champion ya visiwani humo kisha kucheza Chasasa United kabla ya kudakwa na mabingwa wa zamani wa Zanzibar, Jamhuri.
Baada ya kutamba na Jamhuri, mwaka juzi alienda Misri kucheza soka la kulipwa kabla ya Simba kumnyakua hivi karibuni huku akiichezea timu ya Taifa ya Zanzibar.
Kuhusu duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara iliyoanza wiki iliyopita, anasema ni la ushindani mkubwa.
"Ligi ni ngumu, kila timu itataka kushinda ili ijiweke pazuri hali inayofanya isiwe rahisi kutabiri matokeo ya uwanjani," anasema.
Badru anayependa kula vyakula vya kawaida visivyo na madhara na kunywa vinywaji laini hasa juisi halisi, anaitabiria klabu yake ya Simba kuwa itafanya veme kwa jinsi ilivyojiandaa chini ya kocha Logarusic.
"Wapinzani wetu wakae chonjo, tupo fiti na wachezaji tuna ari kubwa ya kuona Simba inafanya vyema kwenye duru hili la pili baada ya kumaliza duru lililopita nafasi ya nne chini ya kocha mwingine," anasema Badru aliyetoa pasi kwa Ramadhani Singano 'Messi' na kumwezesha kufunga bao pekee wakati wakiilaza Rhino Rangers 1-0.
Anasema licha ya kutokuwa na uzoefu na ligi hiyo, lakini anajiamini atafanya mambo makubwa akiaminiwa na makocha wake kwa sababu anajiamini na kujua soka.
Badru aliyeanza kucheza soka la kulipwa mwaka 2006 anawashukuru wazazi, wajomba zake, kocha Mohammed Malik na wote waliomsaidia kufika alipo sasa, akidai zaidi ya yote ni Mungu aliyemuumba.
"Naamini bila ya Mungu kunijalia kipaji na kunipa afya njema ya kucheza, leo nisingekuwa hapa, ninamuomba anizidishie zaidi ili nitimize malengo yangu," anasema.
Badru anasema kama siyo soka alitamani baadaye kuwa 'Injinia' au mfanyabiashara, huku akidai kwa hapa nchini hakuna mchezaji anayemsumbua dimbani.

No comments:

Post a Comment