Kikosi cha Mbeya City
Kikosi cha Yanga
MABINGWA watetezi Yanga leo watakuwa na kibarua kigumu cha kujaribu kutibua rekodi ya Mbeya City ya kutofungwa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa inaicheza kwa mara ya kwanza msimu huu.
Yanga iliyokuwa imeweka kambi nchini Uturuki, itapepetana na Mbeya City katika pambano pekee litakalochezwa siku ya leo katika mfululizo wa ligi hiyo huku mashabiki wakiwa na kihoro cha kuona nani anayeibuka mbabe.
Katika pambano lao la awali lililochezwa Septemba 14 kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya, Yanga ilibanwa na Mbeya Cit licha ya ugeni wao kwa kulazimishwa sare ya bao 1-1 huku wakongwe hao wakifanyiwa fujo.
Timu zote zinakutana leo zikiwa zimetoka kuambulia sare katika mechi zao zilizopitwa Yanga ikibanwa na Coastal Union jijini Tanga kwa kutoka 0-0 wakati Mbeya wenyewe wakilazimisha sare ya 1-1 kwa Ruvu Shooting.
Yanga imeiendea Mbeya City  kuiwekea kambi  ili kuweza kuishikisha adabu, ilihali Mbeya City ikiwasili mapema jijini Dar es Salaam ili kuzoea hali ya hewa na kutaka kuwaadhiri watetezi hao.
Yanga ina Presha zaidi baada ya mtani wao Simba jana kutakata uwanja wa Taifa kwa kushinda mabao 4-0 na kuwasogelea kipointi wakitofautiana pointi mbili tu Simba ikiwa na 30 wenyewe wakiwa na 32, huku Mbeya ikiwa na 31.
Timu hizo zinakutana zikiwa zinafukuzana nyuma ya Azam wanaoongoza msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 33 na timu yoyote ikishinda katika mchezo huo wa leo itakwea kileleni na kuiengua Azam.
Je ni Yanga inayofundishwa na kocha Johannes va Der Pluijm aliyeanza kwa kutoa visingizio tangu arejee toka Uturuki au ni Juma Mwambusi ataendeleza rekodi ya kutopoteza mchezo hata leo? Tusubiri baada ya dakika 90.