STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, February 12, 2014

Yanga kuwafuata Wacomoro kesho

* Wenzao Azam wameshatimka zao Msumbiji

WAKATI timu ya Azam ikiwa imeshatimka zake kwenda Msumbiji kwa ajili ya mechi ya marudiano dhidi ya Ferroviario de Beira siku ya Jumapili, Wawakilishi wa Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga wenyewe wataondoka kesho mchana kuwafuata Komorozine de Domoni ya Comoro.
Kwa mujibu wa taarifa za mtandao wa klabu hiyo ya Young Africans Sports Club, itakwea pipa saa 6 kamili mchana kuelekea Visiwa vya Comoro tayari kwa ajili ya mchezo wa marudiano dhidi ya timu ya Komorozine de Domoni utakaofanyika siku ya jumamosi katika Uwanja wa stade International Said Mohamed Cheik  Mitsamiouli.
Kikosi cha mholanzi Hans Van der Pluijm kimekua kikifanya mazoezi asubuhi na jioni katika Uwanja wa Karume makao makuu ya TFF kwa ajili ya kujiandaa na mchezo huo wa marudiano ambao ni muhimu kwa Young Africans kuendelea kufanya vizuri na kuweza kusonga hatua inayofuata.
Young Africans inatarajiwa kuondoka na shirika la ndege la Precision majira ya saa 6 kamili mchana na kuwasili Visiwa vya Comoro majira ya saa 8 mchana ambapo kikosi kitaelekea hotelini kupumzika kabla ya jioni kufanya mazoezi mepesi.
Katika mchezo wa awali uliochezwa mwishoni mwa wiki Young Africans iliibuka na ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Komorozine mabao yaliyowekwa wavuni na Mrisho Ngasa (3), Didier Kavumbagu (2), Nadir Haroub (1) na Hamis Kiiza (1).
Msafara unatarajia kuwa na watu 30 wakiwemo wachezaji 19 Benchi la Ufundi saba (7) pamoja na viongozi wanne (4)
Magoikipa ni: Deogratias Munish "Dida" na Ally Mustafa "Barthez"
Walinzi: Juma Abdul, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, David Luhende, Nadir Haroub "Cannavaro", Kelvin Yondani na Rajab Zahir
Viungo: Athuman Idd "Chuji", Frank Domayo "Chumvi", Haruna Niyonzima, Hassan Dilunga na Hamis Thabit
Washambuliaji: Hamis Kiiza, Didier Kavumbagu, Said Bahanuzi, Saimon Msuva na Mrisho Ngasa 
Wakati huo huo, Azam wameondoka asubuhi ya leo tayari kwenda kulinda ushindi wao wa bao 1-0 iliyopata kwa Wamakonde siku ya Jumapili.
Wapinzani wao wamenyewe bado wamesalia nchini, japo wataondoka leo jioni kurudi kwao tayari kwa mechi hiyo inayotarajiwa kuwa mtihani mgumu kwa Azam kutokana na Ferroviario kuonekana wazuri.

No comments:

Post a Comment