STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, April 17, 2014

'Mzee Gurumo kama alikiona kifo mapema hospitalini

Masheikh wakiendelea na kisomo cha kumuombea Mzee Gurumo katika safari yake ya Ahera

Mwili wa Mzee Gurumo ukitolewa kwenye nyumba yake ya Mabibo tayari kwa safari ya kwenda kuzikwa Masaki

Mzee Jangala na JB wakiteta kwenye msiba wa Mzee Gurumo, Mabibo

Juma Ubao akimuelezea Mzee Gurumo kwa waandishi wa Habari

Umma uliojitokeza Masaki

Kaburi alilozikiwa Mzee Gurumo

Shamsa Ford alikuwapo kumsindikiza Mzee Gurumo

Said Mabela kizungumza na wanahabari

Jeneza la mwili wa Mzee Gurumo likiswaliwa Mabibo
Mwili waq Gurumo ulitoka kuswaliwa msikiti wa kijijini kwao Masaki

HUWEZI kujua ni kitu gani kilimjia, lakini ukweli ni kwamba saa chache kabla ya kufariki, gwiji wa muziki wa dansi nchini, Muhidini Gurumo aliyefia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), alikiona kifo chake na kujaribu 'kukikwepa'.
Inaelezwa Gurumo asubuhi ya Jumapili, alitoroka hospitalini hapo kabla ya kushtukiwa na kurudishwa wodini huku akiieleza familia yake amechoka kukaa hapo na kutaka aende nyumbani.
Kwa mujibu wa mmoja wa wanafamilia, Gurumo alitaka akakae nyumbani japo siku mbili kisha arejee hospitalini kuendelea na matibabu.
"Huwezi kuamini alitoroka wodini na kukamatiwa getini, tulimweleza haoni aibu kama wanahabari wakijua alitaka kutoroka bila ruksa ya daktari, lakini alidai asingejali kwa vile amechoka kukaa hospitalini hapo," alisema mwanafamilia huyo anayedai ameoa nyumba moja na Gurumo.
Aliongeza walimbembeleza na kumuahidi kumuombea ruksa kwa daktari wake ili aende nyumbani kwa siku nne badala ya mbili alizotaka na kutulia.
"Niliachana naye saa 7:30 mchana akiridhika akijua mpango huo utafanyika Jumatatu, ila nilipofika Mbagala nilipigiwa simu amefariki, nahisi huenda alikiona kifo mapema ndiyo maana alitaka kuondoka hospitalini."
Naye mdogo wa marehemu, Yahya Mikole alisema mara kadhaa Gurumo alimsisitizia akifa asizikwe haraka ili kutoa nafasi watu kuhudhuria mazishi yake.
"Alidai asizikwe haraka kama Tx Moshi William, ndiyo maana tumezingatia wosia wake na kumzika Jumanne badala ya Jumatatu," alisema Mikole.

ELIMU
Siyo katika muziki tu, Gurumo japo hakubahatika kusoma sana elimu ya kawaida zaidi ya ile ya dini ya Kiislam, lakini alikuwa mdau mkubwa wa sekta ya elimu.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Fatma Lusindilo alifichua kwenye msiba wa Mzee Gurumo kijijini kwake Masaki wakati akitoa ubani wao wa Sh.400,000 kwa familia ya marehemu, akidai enzi za uhai wake Gurumo alijali na kuthamini elimu kwa kuchangia kila mara Mfuko wa Elimu wa wilaya hiyo.
"Kwa mchango wake kwa jamii, tunatoa mkono wa pole kwa familia kiasi cha Sh.400,000, tunawaomba muwe na subira katika kipindi hiki kigumu," alisema DC Fatma.

CHOKI
Mkurugenzi wa Extra Bongo, Ally Choki, mmoja wa waombolezaji waliojitolea kwa hali na mali katika msiba wa Gurumo kama ilivyokuwa kwa Ruge Mutahaba na Lady Jaydee waliotoa usafiri kusafirisha waombolezaji, alisema itamchukua muda mrefu kusahau msiba wa Gurumo.
Choki alisema yeye ni kati ya wanamuziki wachache na wa pekee kwa kizazi kipya kuimba na Gurumo akirejea albamu yao akiimba vyema wimbo wa Kassim wa Kutumia.
"Ni pigo kwa wadau wa muziki na familia nzima ya gwiji huyo, lakini kwangu ni pigo zaidi kwa vile ndiye pekee wa kizazi cha sasa niliyeimba naye kazi binafsi, ila nadhani ni mipango ya Mungu nami kubakiwa na kumbukumbu yake," alisema Choki ambaye aliurudia wimbo wa Gurumo wa 'Kassim', ambao Choki aliimba sauti ya gwiji huyo.

SIFA
Waombolezaji wakiwamo viongozi na wanamuziki wenzake walimmiminia sifa Gurumo wakidai alikuwa mfano Tanzania, kiasi cha Rais wa Shirikisho la Muziki Tanzania, Ado Novemba alidiriki kumtaja kama 'Nyerere wa Muziki'.
Said Mabela aliyechukuliwa na Gurumo kutoka Kurugenzi Jazz ya Arusha mwaka 1973, alisema hana cha kusema zaidi ya kumuombea safari njema na atamkumbuka kwa mengi hasa katika kupeleka mbele muziki wa Tanzania.
Shaaban Dede, Juma Ubao, Kassim Mapili, Jamhuri Kihwelu, Shem Ibrahim Kalenga, Mafumu Bilal 'Bombega' na wengine walisema Gurumo ameacha pengo katika fani ya muziki na michezo kwani enzi za uhai wake alikuwa shabiki wa Simba ya Dar es Salaam na Manchester United ya Uingereza bila kificho.
Waliohudhuria msiba wa Gurumo mbali na Makamu wa Rais, Dk Gharib Bilal ni DC wa Kinondoni, Jordan Rugimbana, Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan, Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, Makamu wa Rais wa zamani wa TFF, Nassib Ramadhan, MB Doggy, Dully Sykes, Omar Tamba, Idd Seleman, Chiki Mchoma na wengine.

MAZISHI
Gurumo muasisi wa miondoko na bendi za Msondo Ngoma, Sikinde na Ndekule' aliyezipigia pia Kilimanjaro Chacha, Kilwa Jazz na Orchestra Safari Sound (OSS), alifariki saa 9 ya Jumapili na kuzikwa saa 7:53 ya Jumanne  kijijini kwao.
Alisumbuliwa na maradhi ya mapafu na moyo kwa miaka zaidi ya miwili na kusababisha kustaafu muziki Septemba mwaka jana.
Safari ya maziko yake ilianza saa 2 asubuhi mwili wake kutolewa Muhimbili na kuletwa nyumbani kwake saa 2:45 na kupokewa na umati wa waombolezaji kabla ya kuswaliwa saa 4:38 na saa 4:57 kusafirishwa kwenda Kisarawe.
Msafara kuelekea kijijini uliongozwa na gari la kubebea wagonjwa la Hospitali ya Mwananyamala na kuwasili saa 7:09 kisha kuswaliwa tena msikiti wa kijiji hicho na kuzikwa saa 7:53 kuhitimisha safari yake ya miaka 74 duniani.
Marehemu Gurumo aliyezaliwa 1940 ameacha mjane Pili bint Said na watoto sita na enzi za uhai wake alitamba na nyimbo mbalimbali ukiwamo wa 'Kassim Na.1' na Na.2.

No comments:

Post a Comment