STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, May 28, 2014

Stars yaizamisha Malawi ikiifuata Mighty Warriors kumaliza kazi

Kiemba akishangilia bao lake
TIMU ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, jana ilikuwa na maandalizi mazuri ya mechi yao ya marudiano dhidi ya Zimbabwe baada ya kuifunga Malawi 1-0 katika mechi ya kirafiki ya kimataifa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kiungo wa klabu ya Simba, Amri Kiemba alifunga goli pekee lililoamua mechi hiyo na kuipa Stars ushindi wa pili mfululizo tangu ilipokumbana na kipigo cha aibu cha 3-0 kutoka kwa Burundi katika mechi ya kuadhimisha miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na pia kujiandaa na michuano ya Mataifa ya Afrika 2015.
Stars inajiandaa na mechi yake ya marudiano dhidi ya Zimbabwe katika hatua ya awali ya mchujo wa kuwania kucheza hatua ya makundi ya kufuzu kwa fainali za Mataifa Afrika zitakazofanyika mwakani nchini Morocco. Katika mechi yake iliyopita kwenye jijini Dar es Salaam, Stars ilishinda 1-0 kwa bao la mshambuliaji John Bocco 'Adebayor' na itahitaji japo sare jijini Harare katika wikiendi ya kati ya Mei 30-31 na Juni 1. Ikivuka hatua hiyo itaingia raundi ya pili ya mchujo ambako itakutana na mshindi baina ya Sudan Kusini na Msumbiji.
Mshindi atafuzu kwa hatua ya makundi ya kufuzu. Endapo Tanzania itatinga hatua ya makundi ya kuwania kufuzu itaingia katika Kundi F la kufuzu ambalo linaundwa na timu za Zambia, Niger, Cape Verde.
Timu mbili kutoka kila kundi la kuwania kufuzu kati ya makundi saba yaliyopo, pamoja na mshindi wa tatu mmoja aliyefanya vizuri zaidi, wataungana na mwenyeji Morocco kwa ajili ya fainali hizo za Mataifa ya Afrika 2015 nchini Morocco.
Mechi ya jana iliyoshuhudiwa na mashabiki wachache mno waliokata tiketi na kuingia uwanjani, ilianza kwa wachezaji wote na marefa kukusanyika kwenye duara la katikati ya Uwanja wa Taifa na kuwa kimya kwa dakika moja kumkumbuka Balozi wa Malawi nchini, Flossy Gomile-Chidyaonga, aliyefariki hivi karibuni.
Winga Simon Msuva alikuwa katika nafasi nzuri ya kuifungia Stars goli la dakika ya kwanza lakini, akiwa ndani ya boksi, alipaisha na kushika kichwa asiamini kilichousibu mguu wake wa kulia.
Kiungo mkongwe Kiemba aliifungia Stars goli akimalizia pasi tamu ya mchezaji 'kiraka' Shomari Kapombe katika dakika ya 36. Mpira wa bao ulianzia kwa nyota wa Malawi, Gabadinho Mhango aliyenyang'anywa na Kapombe kisha mchezaji huyo wa AS Cannes akaanza kupigiana gonga moja moja na winga chipukizi Friday wakipita kwenye wingi ya kulia kusini mwa Uwanja wa Taifa kabla ya mpira kutua kwenye mguu wa kulia wa mfungaji aliyekuwa ndani ya boksi la wageni.
Bao hilo lilidumu hadi wakati wa mapumziko. Kipindi cha pili kilianza kwa Stars kuonekana kuelewana zaidi wakicheza soka la pasi fupi fupi na za haraka lakini tatizo la umaliziaji mbovu liliwanyima wenyeji ushindi mnono zaidi.
Dakika nne kabla ya mechi kumalizika kipa Deogratias Munishi 'Dida', aliinusuru Stars kufungwa goli la kusawazisha baada ya kupangua kishujaa shuti kali la ndani ya boksi kutoka kwa mtokeabenchini Rodric Gonani.
Katika hali ya kushangaza, Kapombe alikuwa amevaa jezi namba 19 ya Kelvin Friday huku winga huyo kinda wa mabingwa wa Tanzania Bara, Azam FC akivaa jezi namba 20 inayovaliwa na Kapombe.
Mechi hiyo iliyokosa mashamsham kutokana na mahudhuria madogo, ilichezeshwa na refa Mtanzania Israel Nkongo akisaidiwa na Hamis Chang'walu na Erasmo Jesse.
Vikosi vilikuwa: Stars: Deogratias Munishi 'Dida', Himid Mao, Edward Charles, Said Morad, Joram Ngezeke/ Kelvin Yondani (dk.72), Shomari Kapombe, Simon Msuva/ Ramadhani Singano (dk.46), Erasto Nyoni/ Frank Domayo (dk.76), Kelvin Friday/ Said Juma (dk.73), Amri Kiemba/ Mwinyi Kazimoto (dk.73) na Khamis Mcha.
Malawi: Richard Chipuwa, Moses Chabvula/ Francis Mulimbika (dk.79), Limbikani Mzava/ Bashiri Maunde (dk 57), John Lanjesi, Foster Namwera, Phillip Masiye, Young Chimodzi JR, Gabadinho Mhango, Chimango Kaira, Joseph Kamwendo/ Frank Banda (dk.67) na Atusaghe Nyondo/ Robin Ngalawe (dk.37)..
NIPASHE

No comments:

Post a Comment