Suarez akimtungua Joe Hart |
WAKATI wawakilishi tegemeo la Afrika, Ivory Coast wakiwa mguu ndani mguu nje kwenye michuano ya Kombe la Dunia, nyota wa Liverpool, Luis Suarez amethibitisha ubora wake kwa kuifungia nchi ya Uruguay mabao mawili yaliyoizamisha England katika fainali hizo zinazoendelea nchini Brazili.
Suarez aliyekosa pambano la kwanza la Uruguay dhidi ya Costa Rica na kulala mabao 3-1, alirejea uwanjani akitokea kwenye majeruhi kwa kufunga mabao hayo yaliyoilaza England 2-1.
Wayne Rooney alifunga bao lake la kwanza kwenye fainali za Dunia katika dakika ya 75, lakini halikutosha kuiokoa nchi yake ambayo sasa inasubiri majaliwa yake kutokana na matokeo ya mechi ya leo ya kundi lake kati ya Italia na Costa Rica.
Kama Costa Rica itafungwa itakuwa nafuu kwa England ikisubiri kuona mechi yao ya mwisho dhidi ya Costa Rica itaamua vipi juu ya hatma yao, ingawa dalili za wazi ni kwamba timu hiyo imeshapoteza matumaini ya kusonga mbele na kuweka rekodi ya kufungwa mechi mbili mfululizo za makundi katika michuano hiyo mkubwa ya dunia.
Mtukutu Suarez kinara wa mabao wa Ligi Kuu ya England, alianza kuiadhibu England kwa bao la dakika ya 39 ambalo lilidumu hadi wakati wa mapumziko kabla ya Rooney kusawazisha na kuonyesha kwamba mechi ingeisha kwa sare kabla ya Suarez kuzima ndoto hizo dakika ya 86.
Katika mechi nyingine zilizochezwa jana, Ivory Coast ilijikuta ikipokea kipigo cha mabao 2-1 toka kwa Colombia na kuwaacha wapinzani wao wakitangulia hatua ya 16 Bora.
Colombia iliyoitungua timu ya Ugiriki kwa mabao 3-0 katika mechi yao ya kwanza ilitangulia kupata mabao yake katika dakika ya 64 na 70 kupitia kwa James Rodriguez na Juan Quintero kabla ya Tembo hao wa Afrika kupata bao la kutia machozi lililokuwa la kuisawazisha kuptia kwa Gervinho dakika ya 74.
Nayo Japan na Ugiriki zimeshindwa kutambiana baada ya kutoka suluhu ya bila kufungana na kutoa nafuu kwa Ivory Coast ambao wanasubiri kujua hatma yao watakapoumana na Ugiriki wiki ijayo.
Kipute cha fainali hizo kinaendelea tena kwa michezo itakayozikutanisha Italia dhidi ya Costa Rica, Uswisi dhidi ya Ufaransa na Hondurus itapepetana na Ecuador
RATIBA IPO hivi:
LEO Juni 20, 2014
Italia v Costa Rica Saa 1:00 Usiku
Uswis v Ufaransa Saa 4:00 Usiku
Honduras v Ecuador Saa 6:59 Usiku
KESHO Jumamosi Juni 21, 2014
Argentina v Iran Saa 1:00 Usiku
Ujerumani v Ghana Saa 4:00 Usiku
Nigeria v Bosnia-Herze Saa 6:59 Usiku
No comments:
Post a Comment