STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, August 21, 2014

Simba, Yanga kuonyeshana kazi Okt.12

Kikosi cha wakali wa Msimbazi
Vijana wa Jangwani
WATANI wa jadi Simba na Yanga watakutana mapema katika raundi ya nne ya ligi Oktoba 12 mwaka huu, kwa mujibu wa ratiba ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara 2014-15 iliyotolewa jana na shirikisho la soka nchini (TFF).
Miamba hao wa soka nchini watarudiana katika raundi ya 17 ya ligi hiyo Februari 8, 2015, ratiba hiyo imeonyesha.
Mabingwa Azam FC wataanza kampeni ya kutetea taji lao la kwanza kwa kuwakaribisha Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Azam Complex katika siku ya kwanza ya ufunguzi wa msimu Septemba 20, siku ambayo viwanja sita 'vitawaka moto'.
Yanga waliomaliza katika nafasi ya pili msimu uliopita wataanza msimu mpya chini ya kocha mpya Mbrazil Marcio Maximo kwa kucheza ugenini dhidi ya timu inayozinyima usingizi timu kubwa ya Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa Jamhuri wakati Mbeya City waliomaliza katika nafasi ya tatu watawakaribisha JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya. Simba waliomaliza wa nne msimu uliopita wataingia katika mtihani wa kwanza chini ya kocha mpya Mzambia Patrick Phiri kwa kuwakaribisha Coastal Union kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam katika siku hiyo ya ufunguzi wa msimu.
Mechi nyingine za siku ya ufunguzi zitakuwa ni wageni wa ligi hiyo Stand United watakaowakaribisha wageni wenzao Ndanda FC kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga huku Mgambo JKT ikiwa mwenyeji wa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga wakati Ruvu Shooting itawakaribisha Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Mabatini, mkoani Pwani.
Yanga watakuwa na mechi mbili ngumu zilizofuatana katika raundi ya nane na ya tisa ya ligi pale watakapowakabili mabingwa Azam Novemba 9 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa na kisha kusafiri hadi ugenini Mbeya kuwavaa Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine siku sita baadaye.
Simba watawakaribisha Mbeya City katika raundi ya 10 ya ligi kwenye Uwanja wa Taifa Desemba 20 mwaka huu kabla ya kuwavaa Azam katika raundi ya 12 siku ya Mwaka Mpya Januari 1, 2015 kwenye Uwanja wa Taifa. Ligi hiyo itafikia tamati Aprili 18, 2015.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, ratiba hiyo imezingatia michuano ya Chalenji itakayochezwa Novemba, usajili wa dirisha dogo Nov 15- Des 15, ushiriki wa klabu za Azam na Yanga kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa (CL) na Kombe la Shirikisho (CC).
Wambura alisema mechi za ligi hiyo zitachezwa wikiendi ili kuongeza msisimko/kuwapa fursa washabiki wengi zaidi kuhudhuria na kwamba katikati ya wiki imeachwa wazi kwa ajili ya mechi za Kombe la FA (Federation Cup).
"Vilevile kutakuwa na mechi Boxing Day na siku ya Mwaka Mpya," alisema Wambura.

No comments:

Post a Comment