STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, March 2, 2015

BASATA LAMLILIA CAPT JOHN KOMBA

Mwili wa Kapteni Komba ukiwasilia Karimjee mapema leo kwa ajili ya kuagwa kabla ya kusafirishwa kwenda kuzikwa kijijini kwao Lutuhi, Nyasa, wilayani Mbinga.
Kapteni John Komba enzi za uhai wake katika picha tofauti akiwajibika katika sanaa yake ya uimbaji wa kwaya
Na Rahim Junior
BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) limetuma salamu za rambirambi kumlilia Mbunge wa Mbinga Magharibi, Kapteni John Komba aliyefarikia wikiendi iliyopita.
Kwa mujibu wa taarifa yake BASATA imekielezea kifo cha Komba kama pigo kubwa katika tasnia ya sanaa.
Taarifa ya BASATA inasomeka hivi;
BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) limepokea kwa masikitiko na majonzi makubwa kifo cha Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Captain John Damian Komba kilichotokea jioni ya Jumamosi ya tarehe 28/02/2015.
Captain John Damian Komba ni msanii na mdau wa muda mrefu wa sekta ya Sanaa nchini. Amekuwa ni taa na nuru ambayo katika kipindi chote cha uhai wake imeangaza na kutoa mwanga angavu kwenye sekta ya Sanaa.
Mchango wake katika muziki wa dansi, kwaya na ule wa kiweledi katika kuandaa na kukuza wasanii mbalimbali nchini hautasahaulika kamwe. Ni mdau aliyeacha alama kuu katika muziki wa bendi, kwaya na taarabu na amejitolea kwa kiasi kikubwa katika kuufikisha muziki wa dansi na kwaya mahali ulipo leo.
Aidha, pamoja na kujiunga na siasa na hatimaye kuwa Mbunge wa jimbo la Mbinga Magharibi, Mheshimiwa Komba hakukoma kuendelea kuipigania sekta ya Sanaa kwani alikuwa ni mjumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii ambayo kwa mujibu wa kanuni za Bunge ndiyo inayoisimamia na kuishauri Serikali katika masuala yote yahusuyo sekta ya Sanaa na Utamaduni.
Baraza, wasanii na wadau wote wa Sanaa hatuna budi kuendelea kuenzi mema yote aliyotuachia marehemu John Komba hasa katika kutunga nyimbo za hamasa na ujumbe makini na wenye mashiko kwa jamii yote ya Watanzania.
Hakika pengo lililoachwa na Marehemu haliwezi kuzibika, kwani imekuwa ni kama mshumaa uliyozimika ghafla wakati tukiingia kwenye giza.
Baraza linatoa pole kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Anne Makinda, wabunge na wadau wote wa Sanaa hususan wasanii kwa msiba huu. Ni matumaini ya Baraza kwamba, tutaendelea kuenzi mema yote yaliyotendwa na Marehemu, hasa kudumisha upendo na amani katika tasnia yetu ya Sanaa na taifa kwa ujumla.
Bwana ametoa na  Bwana ametwaa, Amen
Godfrey Mngereza
KATIBU MTENDAJI

No comments:

Post a Comment