STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, June 10, 2016

Beki ya Yanga majaribuni, kupaa J'Pili kuifuata Bejaia

Baadhi ya wachezaji wa Yanga
SIKIA hii. Zaidi ya nusu ya mabao ya Yanga msimu huu yamefungwa na mastraika wawili, Donald Ngoma na Amissi Tambwe ambao umoja wao umeipa vijana wa Hans Pluijm jumla ya mabao 42, kati yao 38 ya Ligi Kuu na manne ya michuano ya Afrika.
Hivyo ni rahisi kwa mabeki wa timu pinzani kama wameisoma vema safu ya ushambuliaji ya Yanga kuinyima ushindi kwa kuwazuia nyota hao, kwani hata katika Ligi Kuu Bara baadhi ya timu ziliweza kufanya hivyo na kuisumbua Yanga.
Lakini sasa kama ulikuwa hujui ni kwamba Yanga inayojiandaa na safari yake ya kwenda Algeria kuvaana na MO Bejaia katika mechi ya ufunguzi ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, mabeki wake watakuwa na ngoma nzito ughaibuni.
Mabeki hao watakuwa na kazi ngumu juu ya kubashiri wamkabe mchezaji gani wa Bejaia ili wasije wakaaumbua ugenini, kwani wapinzani wao hao hawana mfungaji mmoja tegemeo, mchezaji yeyote wa timu hiyo akipata nafasi ya kutupia mpira kimiani anafanya hivyo, kitu ambacho ni lazima mabeki wa Yanga wajipange mapema kabla ya kuwafuata Waarabu hao watakaocheza nao Juni 19.
Ukiondoa mastraika wake nyota, Okacha Hamzaoui, Zahir Zerdab na Mamadou N'Doye, Bejaiapia hufunga mabao yake kupitia viungo na mabeki wake wanaocheza soka la nguvu.
Staili hiyo ya Bejaia kutomtegemea mfungaji mmoja, itawapa kibarua kizito mabeki wa Yanga, Juma Abdul, Oscar Joshua, Vincent Bossou, Kelvin Yondani na nahodha  Nadir Haroub 'Cannavaro', kuanza mapema kusaka mbinu za kuhakikisha kipa wao iwe Ally Mustafa 'Barhez' au Deo Munishi 'Dida' hawasumbuliwi katika mechi hiyo.
Achana na mechi za Ligi Daraja la Kwanza (Division 1) ya Algeria ambapo ilimaliza katika nafasi ya sita ikikusanya pointi 44 kutokana na mechi 30 huku ikifunga mabao 33, kwenye mechi ya kimataifa timu hiyo ilifunga mabao saba hadi kutinga makundi ya Kombe la Shirikisho, yote yakifungwa na wachezaji tofauti.
Mabao mawili pekee ndiyo yaliyofungwa na mchezaji mmoja, Mamadou N'Doye wakati Bejaia ikipata sare ya bao 1-1 dhidi ya Zamalek katika raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kung'olewa na ilipovaana na Esperance ya Tunisia kuwania kutinga makundi ya Kombe la Shirikisho. Ndoye hata hivyo hatakuwepo kwenye mchezo huo wa Juni 20 kwani ana kadi zinazomzuai kucheza mechi ya Yanga.
Mabao yake mengine yamefungwa na Okacha Hamzaoui, beki Sofiane Khadir, Faouzi Yaya na kiungo Morgan Betorangal Mfaransa mwenye asili ya Chad na jingine mchezaji wa Club Africans ya Tunisia alijifunga katika mechi yao.
Kwa kuangalia hivyo ni wazi vijana wa Hans Pluijm wanatakiwa kuwa makini na wapinzani wao kuhakikisha wanavuna pointi tatu muhimu umangani kabla ya kuja kuvaana na TP Mazembe katika mechi yao ya pili ya Kundi A wiki mbili zijazo.
Yanga imetinga hatua hiyo ikiwa ni rekodi kwao na timu za Afrika Mashariki na ipo kundi moja na Medeama ya Ghana watakaoumana nao katika mechi mbili mfululizo mwanzoni mwa Julai.

katika hatua nyingine kikosi cha Yanga kitapaa alfariji ya Jumapili kuelekea Uturuki kuweka kambi kabla ya kuivamia Mo Bejaia kwao kwa mchezo wao wa Kundi A.
Awali safari hiyo ilitangazwa ingefanyika kesho Jumamosi, lakini mipango imeenda sivyo ikiwa ni pamoja na kupisha Uchaguzi Mkuu unaofanyika kesho kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar.

No comments:

Post a Comment