STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, July 27, 2010

DC mikononi mwa Takukuru *Anawania ubunge viti maalum *Akamatwa na wapambe wake, fedha gesti

MKUU wa Wilaya ya Kasulu, Betty Machangu, ni miongoni mwa mavuno mapya ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) katika operesheni ya kukamata wagombea ubunge wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya kugawa fedha.

Machangu alikamatwa juzi na maofisa wa Takukuru mkoani Kilimanjaro pamoja na vigogo wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) wa mkoani wa Kilimanjaro
na wa Wilaya ya Moshi Vijijini.

Mkuu huyo wa wilaya ambaye amejitosa kwenye kinyang’anyiro cha kusaka ubunge kupitia viti maalum mkoani Kilimanajro, alikamata na kuhojiwa kisha kuachiwa.

Machangu anadaiwa kutoa rushwa kwa wajumbe wa UWT mkoa ili wamchague.

Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Alexander Budigila, aliwataja
watuhumiwa wengine kuwa ni Katibu wa UWT mkoa, Mariam Kaaya, Katibu wa
UWT wilaya ya Moshi, Hadija Ramadhani, mfanyabiashara wa Moshi
mjini, Hawa Sultani na dereva wa gari alilokuwa wakitumia, Swalehe
Twalibu.

Alisema Takukuru ilipokea taarifa kutoka kwa raia mwema za kuwepo vitendo vya rushwa katika nyumba ya kulala wageni ya Safari Resort, ambapo walikuwa wakigawa rushwa ya fedha na vitu kwa wajumbe kwa kila mmoja kuingia mmoja mmoja kuanzia majira ya saa 8:30 mchana.

Tarifa hiyo ilionyesha kuwa mgombea huyo na wafuasi wake walikuwa wakigawa fedha kiasi cha Sh. 100,000 na 50,000, kanga, asali na vipeperushi na kadi za wajumbe wa mkutano mkuu wa UWT mkoa.

“Tuliizingira nyumba hiyo kuanzia majira ya saa nane hadi saa 10 ndipo tulipoingia ndani na kuwataka kufungua chumba namba 24 ambako
mgombea huyo na viongozi hao walikuwa wamejifungia huku dereva wa gari
lenye namba za usajili T 688 APQ aina ya Mitsubishi ambaye alikuwa anaimarisha ulinzi kwa kila anayefika,” alisema

Alisema walikaa kimya hadi saa 1:30 bila kufungua na ndipo maafisa wa
Takukuru walipojitambulisha na kugonga mlango kwa nguvu zaidi na
majira ya saa 2:15 usiku, ambapo ndipo walifanikiwa kuingia ndani na
kuwakuta watu wanne.

Alisema baada ya upekuzi walikuta Sh. 400,000 kwenye pochi ya katibu wa UWT, pea nne za vitenge, vipeperushi vya kumnadi mgombea
huyo, kadi za wajumbe wa mkutano mkuu wa UWT mkoa ambazo zilitumbukizwa
kwenye chombo cha kuingiza maji chooni (tanki la chooni).

Alisema pia walikamata Sh.100,000 zikiwa kwenye pochi ya mgombea huyo, ambazo ziliwekwa kwenye bahasha na kuandikwa majina, lakini baada ya kuhisi watakamatwa walizitoa kwenye bahasha na
kuzichanachana na kisha kuzitupa chini ya uvungu wa kitanda.

Budigila alisema pia kwenye pochi ya katibu huyo walikuta vipeperushi
vya mgombea mwingine Regina Chonjo ambaye pia ni Mwenyekiti wa UWT mkoa na walifanikiwa kulikamata gari hilo ambalo ni mali ya mgombea huyo.

Machangu akizungumza na wanahabari alisema kuwa majira ya saa 10 ndio
alikwenda kwenye baa hiyo kwa lengo la kupata chakula cha mchana na kwamba baada ya kufika alitafuta mahali penye utulivu, ili azungumze
na viongozi na msaidizi wake kabla ya kwenda kwenye mkutano wa kampeni.

Alisema walikosa pa kukaa na kumua kwenda kukaa chumbani na hakukua na
rushwa yoyote iliyotolewa kwa kuwa kila mmoja alikuja na mkoba wake na
hata kama angetaka kutoa rushwa angewafuata majumbani mwao.


Takukuru yashikiria saba

Wakati huo huo, Takukuru inawashikilia na kuwahoji watu saba waliodaiwa kuwa mabalozi, wajumbe wa vijiji na makatibu wa CCM katika kata ya Shirimatunda ambao wanadaiwa walikuwa wakila na kunywa na mgombea
udiwani mmoja.

Habari zinasema baada ya maafisa wa Takukuru kufika watu hao walikimbia akiwemo mgombea huyo na kwamba walifanikiwa kuwakamata watu hao kati
ya 30 waliokuwa wamekaa na mgombea huyo wakiwa na kikao cha kushawishi
mgombea huyo kupitishwa.

Kamanda wa Takukuru mkoani hapa alisema uchunguzi wa kina wa matukio hayo yote unaendelea na baada ya kukamilika watafikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa mujibu wa sheria.

Dodoma wataka
matokeo yafutwe

Baadhi ya wagombea udiwani wa Viti Maalum kupitia UWT katika Wilaya ya Dodoma Mjini, wametaka matokeo yafutwe na uchaguzi urudiwe kutokana na uchaguzi huo kutofanyika kwa haki.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ofisi ya CCM mkoa, mmoja wa wagombea hao, Catherine Mbiligwa, alisema uchaguzi huo haukuwa wa huru na haki kutokana na mmoja wa wasimamizi uchaguzi (jina tunalo) kutoa kauli za matusi kwa wagombea na wajumbe waliokuwepo kwenye uchaguzi huo.

Alisema moja ya sababu za kuomba uchaguzi huo kurudiwa ni kutokana na wagombea hao kutopata nafasi ya kuhesabu kura zao wala kuweka mawakala wao.

“Tulipojaribu kumuomba tuweke mawakala wetu kama haki yetu, tulifukuzwa kama mbwa na askari pamoja na katibu wa UWT wakishirikiana na msimamizi wa uchaguzi,” alisema.

Aidha, mgombea huyo alisema wakati wa kupiga kura pia hapakuwa na masanduku ya kutosha ya kuwekea kura, badala yake kura nyingine zililazimika kufungwa kwenye kanga za wajumbe.

Mgombea mwingine, Mwajuma Yame, alisema mbali na kutotendewa haki katika uchaguzi huo, pia hapakuwapo na uwiano wa nafasi za viti maalum kwa kila tarafa.

“Kila tarafa inatakiwa kuwa na madiwani watatu wa viti maalum, lakini tarafa zingine zina kata chache tofauti na Dodoma Mjini ambapo kuna kata takribani 20, lakini nafasi za viti maalum ni nne tu…Tunaomba uwiano,” alisema.

Akampeni harusini

Mgombea udiwani anaye maliza mda wake katika Kata ya Tambukareli Manispaa ya Dodoma, Edward Lamali, amejikuta akifanya kampeni katika ukumbi wa harusi.
Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa Hall Cross, ambapo diwani huyo aliteuliwa na ndugu kutambulisha wageni pamoja na kuwapa nasaha maharusi katika maisha yao ya ndoa.

Diwani huyo alitoa utambulisho huo kama alivyoagizwa, lakini kabla ya kuhitimisha alianza kupiga kampeni kwa kuwataka wageni waalikwa kumpigia kura za maoni wakati utakapowadia.

Aliwaomba wamchague kwa mara nyingine ili aendelee kuyamalizia mambo ambayo alikuwa ameshaanza kuyatekeleza kwa kipindi kilichopita.

Mwangunga akumbana na Loliondo jimboni Ubungo
Mgombea wa ubunge Jimbo la Ubungo, Shamsa Mwangunga, amezidi kubanwa na wanachama baada ya kuambiwa kuwa kama alishindwa kuwasaidia Wamasai wa Loliondo mkoani Arusha wasinyang'anywe ardhi na mwekezaji, atawezaje kutatua kero zinazowakabili wananchi wa Mabibo, jijini Dar es Salaam.

Mmoja wa wanachama wa CCM alimbana mgombea Mwangunga ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii kwenye mkutano wa kujinadi wagombea uliofanyika Mabibo na kukutanisha matawi manne.

“Ukiwa kama Waziri wa Maliasili na Utalii ulishindwa kuwasaidia wafugaji hao ambao serikali ilidai kuwa waliingia eneo la hifadhi ya Taifa je, utaweza kutusaidia sisi?” alihoji mwanachama huyo.

Baada ya kuulizwa swali hilo, Mwangunga alishangaa kisha alimjibu kuwa wafugaji hao ndiyo waliovunja sheria na kuingia eneo la hifadhi hivyo serikali iliwaondoa kwa kuzingatia sheria.

Hata hivyo, mwanachama huyo alionekana kutoridhika na jibu hilo ingawa alilikubali na kukaa chini ili kumpa mwenzake aendelee kuuliza
swali lingine.

Maghari ya kifahari yatumika

Wakati huo huo, wagombea wa CCM wamezidi kuonyeshana ufahari wa kuwa na magari ya gharama wakati wa kampeni zao zinazoendelea maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam licha ya chama chao kuwataka wasitumie vyombo hivyo na badala yake wapande basi moja.

Baadhi ya magari hayo yaliyoonekana kuvinjari maeneo ya mikutano ni yenye namba za usajili, T 626 AEX aina ya Toyota Land Cruiser Prado, T 780 AZJ aina ya Nissan Patrol na T257 AQT Toyota Land Cruiser VX ambayo yalikuwa yakitumiwa na wagombea katika jimbo la Segerea.

Katika jimbo la Ubungo nalo, Mwangunga alionekana akiwa ndani ya gari lake aina ya Land Cruiser huku wagombea wenzake wakiwa kwenye basi la pamoja kama chama kilivyowataka kufanya.

Akizungumza na NIPASHE siku ya kwanza ya kuanza kampeni hizo, Katibu Msaidizi wa CCM Wilaya ya Kinondoni, Abihudi Shilla, alisema wagombea wote hawaruhusiwi kutumia magari yao wala kuvaa suti au nguo nyingine tofauti na zile za chama.

Alisema chama kimeweka utaratibu huo ili wagombea wote waonekane wapo sawa kwa wanachama badala ya kila mmoja kufanya mbwembwe za kila aina ili kuwakoga wanachama.

Shy-Rose aibuka
na staili mpya

Mchakato wa kura za maoni kwa wagombea wa CCM Jimbo la Kinondoni umeendelea kuwa na vituko na moja ya matukio na vituko hivyo ni mmoja wa wagombea kutembea kwa gwaride mbele ya wanachama na kuwapigia magoti kuomba kura.

Mgombea huyo, Shy-Rose Bhanji, jana alitumia staili hiyo katika ukumbi wa DDC Magomeni Kondoa alipokuwa akiomba kura kutoka kwa wanaCCM wakazi wa Kata ya Ndugumbi.

Bhanji alitembea kwa gwaride wakati wa kujitambulisha na kupiga magoti kabla ya kuondoka kwa gwaride na kushangiliwa kwa makofi mengi.

Akijibu swali aliloulizwa la jinsi gani ataweza kupambana na dawa za kulevya na kitu gani alichowafanyia vijana kichama, Bhanji alisema kuwa atatetea kero mbalimbali ikiwemo ya kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya kwa vijana, kusaidia wajane kwa kuunda vikundi vya maendeleo.


Kigamboni wazozana

Kampeni katika Jimbo la Kigamboni jana zilikumbwa na mzozo baada wagombea ubunge kutaka kuwabana makatibu wa matawi na wanachama wao kususia kikao cha kampeni.

Matukio hayo yametokea katika mikutano ya katika Kata za Kibada na Mjimwema wakati wagombea hao walipokwenda kujinadi kwa wanachama.

Katika kata ya Kibada, wagombea ubunge walifika katika eneo la mkutano majira ya saa 4:00 asubuhi, lakini walijikuta wakiwa peke yao bila ya kupokewa na wenyeji, baada ya viongozi na wanachama kutokuwepo eneo hilo.

Kutokana na hali hiyo, baadhi walionekana kuja juu wakidai kuna dalili ya kuchezewa rafu, kwa sababu haiwezekani wasione hata mwanachama mmoja akiwa eneo la mkutano.

Juhudi za kusubiri wapiga kura ziligonga ukuta, baada ya mratibu wa kampeni hizo, Jimbo la Kigamboni, Sophia Kinega, kuwaagiza wagombea hao kujinadi mbele ya wanachama 50 pekee kati ya wapigakura 1,500 waliotakiwa kuwepo kwenye mkutano huo.

Akielezea tukio hilo, Mratibu huyo alisema hali hiyo ilisababishwa na makatibu wa matawi kususia kutoa taarifa kwa wanachama wao kwa sababu zisizoeleweka.

“Kwa kweli ni hali ya kusikitisha, nimewasiliana na katibu wa kata, lakini ameniambia makatibu wa matawi wamesusa na ndio maana hata wanachama hawakufika, jambo hili ni baya na ni lazima nilifikishe mbele,” alisema Kinega.

Mjumbe mmoja aliyejitaja kwa jina la Mohamed Namwogo, alisema kwa ujumla taarifa ya kuwepo kwa mkutano huo waliipata usiku na kusababisha wengi wao kushindwa kufika.


Nusura wapigane mkutanoni

Katika hatua nyingine, wagombea watatu nusura wapigane ngumi kwa madai kuwa mgombea mmoja alikuwa akieneza maneno yanayohusiana na ubaguzi wa kikabila.

Wagombea hao, John Kibaso na Magige Kiboko walimtuhumu Kazimbaya Makwega kwa kueneza maneno yanaoonyesha ishara ya kuwatenga kwa sababu wao wanatoka Mkoa wa Mara.

Tukio hilo lilitokea katika kituo cha Kata ya Mjimwema kabla ya kuanza kwa mkutano, ambapo wagombea hao walionekana kupandwa na hasira na kutishia kumtwanga ngumi kwa maelezo kuwa wamechoshwa na maneno yake.

“Haiwezekani bwana kila akisema utamsikia huyu mtu wa Musoma, sasa u-Musoma wetu unakuja vipi hapa, usitubabaishe bwana,” alisema Kibaso kwa hasira na kumfuata Makwega sehemu aliyokuwa amesimama.

Baada ya kuona hali imekuwa mbaya, baadhi ya wagombea waliingilia kati na kuwaingiza ndani ya gari wagombea hao na kuwasihi wapunguze jazba kwani wote ni wamoja.

Hata hivyo, wagombea wote walijinadi mbele ya wanachama na kuelezea mikakati na mipango yao ikiwa watachaguliwa.

Chanzo:GAZETI LA NIPASHE

No comments:

Post a Comment