STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, July 27, 2011

Viongozi Simba waenda kumalizana na Waturuki



VIONGOZI wa klabu ya soka ya Simba wameondoka nchini juzi kuelekea Uturuki kwa ajili ya kwenda kumalizia taratibu za ujenzi wa uwanja wao mpya wa kisasa utakaojengwa eneo la Bunju, nje kidogo ya jijini la Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Afisa Habari wa klabu hiyo, Ezekiel Kamwaga, viongozi walioondoka ni Mwenyekiti Ismail Aden Rage na Katibu wake, Evodius Mtawala.
Kamwaga alisema Rage na Mtawala waliondoka juzi kuelekea nchini humo kufanya mazungumzo ya mwisho na uongozi wa kampuni ya Petroland, ambayo ndiyo itakayoujenga uwanja huo utakaoingiza watazamaji wasiopungua 60,000.
"Viongozi wetu wawili wa juu wameondoka nchini jana, kwenda Uturuki kwa ajili ya kumalizana na watakaotujengea uwanja wetu wa kisasa utakaokuwa eneo la Bunju," alisema Kamwaga.
Afisa Habari huyo, alisema viongozi wao wameenda kuweka mambo sawa kabla ya wakandarasi hao kuja kuanza kazi yao na kuifanya Simba kufuata nyayo za klabu kubwa barani Afrika kama ASEC Memosa au Kaizer Chief zenye viwanja vikubwa vya kisasa.
Uwanja huo utakaokuwa wa kisasa na mkubwa kama ule wa Taifa, utaigharimu Simba kiasi cha Shilingi Bilioni 75 hadi utakapomalizika ukihusisha uwanja wa kuchezea, maduka, kumbi za mikutano na burudani, mbali na hoteli na kituo cha michezo.
Kwa hapa nchini ukiondoa Yanga yenye kuumiliki uwanja wa Kaunda, klabu nyingine yenye uwanja wake mwenyewe ni Azam iliyoujenga eneo la Chamanzi, Mbande nje kidogo ya jijini la Dar es Salaam ambao utaanza kutumika msimu mpya wa Ligi Kuu.

Mwisho

No comments:

Post a Comment