STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, December 30, 2011

Jinamizi la Talaka lipo Mwanza



BENDI kongwe ya muziki wa dansi ya Mlimani Park 'Sikinde' wanatarajia kuvitambulisha vibao vyao vipya kikiwemo 'Jinamizi la Talaka' kwa mashabiki wao wa jijini Mwanza.
Bendi hiyo iliyoondoka jana jijini Dar es Salaam ikiwa na kikosi chake kamili imeenda kuuaga mwaka 2011 na kuukaribisha mwaka mpya jijini Mwanza kwa kufanya maonyesho mawili.
Katibu Mipango wa bendi hiyo, Hamis Milambo alisema onyesho la kwanza litafanyika kesho kwenye ukumbi wa Villa Park, kabla ya kumalizia burudani yao keshokutwa kwa onyesho jingine ambalo litafanyika CCM Kirumba.
Milambo, alisema katika maonyesho yote watatambulisha nyimbo zao zinazoandaliwa kwa ajili ya albamu yao mpya iliyoanza kurekodiwa itakayokuwa na nyimbo sita.
"Tunaelekea Mwanza kufanya maonyesho mawili kwa ajili ya kuuaga na kuukaribisha mwaka 2012 na mashabiki wetu wa jijini humo, ambapo tutafanya onyesho la kwanza Villa Park na kumalizia CCM Kirumba," alisema Milambo.
Milambo alisema hata hivyo hakuwa na hakika ya onyesho la CCm Kirumba, akidai huenda wakafanya onyesho ukumbi wa ndani ambao watapangiwa na wenyeji wao waliowaalika jijini humo.
Katibu huyo alivitaja vibao vipya vitakavyotambulishwa ni Jinamizi la Talaka, 'Kilio cha Kazi', 'Kinyonga', 'Bundi', 'Samahani' na 'Deni Nitalipa'.
"Hivyo ni baadhi tu, lakini pia tutakumbushia nyimbo zetu za zamani zilizoifanya Sikinde kuwa Mabingwa wa Dansi Tanzania," alisema Milambo.

No comments:

Post a Comment