STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, December 30, 2011

Snake Jr apania kulinda rekodi, heshima ya baba yake



BONDIA chipukizi 'asiyepigika', Mohammed Matumla 'Snake Boy Jr', amesema amepania kumsambaratisha mpinzani wake, Cosmas Cheka atakayepigana nae kesho mjini Morogoro ili kulinda heshima ya baba yake, Rashid Matumla 'Snake Man.
Matumla na Cheka wanatarajiwa kuzichapa kesho kwenye uwanja wa Jamhuri, katika pambano lisilo la ubingwa la kumaliza ubishi baina yao, ambapo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Akizungumza na MICHARAZO, Matumla alisema kwa namna alivyojiandaa ni wazi atamsambaratisha mpinzani wao licha ya kucheza uwanja wa nyumbani, lengo likiwa ni kulinda hadhi ya baba yake, Rashid Matumla mbele ya ukoo wa akina Cheka.
Matumla, alisema mbali na kutaka kulinda heshima ya baba yake aliyewahi kupigwa na kumpiga Francis Cheka katika mipambano yao, pia anataka kulinda rekodi yake ya kutopigwa na bondia yeyote nchini.
"Naenda Morogoro kuhakikisha namchakaza Cheka ili kulinda heshima ya mdingi (baba), na kulinda rekodi yangu ya kutopigwa katika michezo 10 niliyokwishacheza hadi sasa," alisema Matumla.
Hata hivyo wakati Matumla akijiapiza hivyo, mpinzani wake amenukuliwa na vyombo vya habari kwamba hana hofu dhidi ya pambano hilo kwa kuamini ataibuka na ushindi kuendeleza ubabe wa ukoo wao mbele ya ukoo wa akina Matumla.
Kwa mujibu wa rekodi zilizopo baina ya mabondia hao wawili ni kwamba Matumla ambaye ni mtoto wa bingwa wa zamani wa WBU, amecheza michezo 10 na kushinda saba, huku Cosmas Cheka mdogo wa Francis Cheka amecheza mechi saba na kushinda manne, akipoteza moja na kupata sare mbili.
Kwa mujibu wa waratibu wa pambano hilo, kabla ya Cheka na Matumla kupanda ulingoni mabondia wa kike wenye upinzani wa jadi, Salma Kiogwa wa Morogoro na Asha Ngedere wa Dar watapigana sambamba na mapambano mengine ya utangulizi.

Mwisho

No comments:

Post a Comment