STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, December 30, 2011

Msondo kuuona mwaka Dar



WAKATI wapinzani wao wa jadi wakilikimbia jiji na kwenda kuukaribisha mwaka mpya jijini Mwanza, bendi ya Msondo Ngoma, yenyewe imejichimbia Dar ikiendelea kutambulisha nyimbo mpya zinazoandaliwa kwa albamu ijayo.
Msemaji wa Msondo Ngoma, Rajabu Mhamila 'Super D', alisema bendi yao imeamua kuwapa burudani mashabiki wa Dar kwa kufanya maonyesho yao ya mwishoni mwa wiki katika kumbi zao zilizozoeleka.
Alisema leo bendi yao itafanya mambo yake kwenye ukumbi wa Leaders Club, kabla ya kesho kutambulisha vibao vyao na kuukaribisha mwaka 2012 na mashabiki wao ukumbi wa TCC-Chang'ombe, wilayani Temeke.
"Sie tumeamua kukomaa Dar ambapo kama kawaida leo Ijumaa tupo Leaders Club wilayani Kinondoni, Jumamosi tutakuwa TCC- Chang'ombe kwa mashabiki wa wilaya ya Temeke na Jumapili tunamalizia hasira zetu kwa watu wa Ilala pale DDC Kariakoo," alisema.
Alisema katika maonyesho yote, Msondo watapiga nyimbo zao zote zilizowasambaratisha wapinzani wao, Sikinde katika mpambano wao usio rasmi uliofanyika siku ya Krismasi.
"Tutatumia silaha zetu zote zilizowasambaratisha wapinzani wetu wiki iliyopita, kuanzia Suluhu, Dawa ya Deni, Baba Kibene, Nadhiri ya Mapenzi, hadi nyimbo za albamu zetu za zamani kuanzia enzi za NUTA, JUWATA na OTTU," alisema Super D.

No comments:

Post a Comment