STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, November 29, 2012

'Tuta' laiua Kili Stars kwa Warundi





Mrisho Ngassa (kati) akitafuta mbinu za kuwatoka walinzi wa timu ya Burundi katika pambano lao la jana. (picha kwa jisani wa Bin Zubeiry.Blog


Na Somoe Ng'itu, Kampala
GOLI pekee la penalti lililofungwa na nahodha wa timu ya taifa ya Burundi, Selemani Ndikumana, liliipa Kilimanjaro Stars ya Tanzania Bara kipigo cha kwanza kwenye michuano ya Kombe la Chalenji katika mechi ambayo "bahati mbaya" ilikuwa ni moja ya sababu kubwa zilizoinyima Stars kuondoka na pointi kwenye Uwanja wa Namboole hapa Kampala jana.
Ndikumana ambaye aliwahi kuichezea klabu ya Simba ya Dar es Salaam alifunga 'tuta' hilo lililotolewa na refa Ronnie Kalema wa Uganda baada ya beki wa kati wa Kili Stars, Shomary Kapombe kumuangukia mfungaji kutokana na kujikwaa na kuumia vibaya wakati akijaribu kumzuia nahodha huyo asimkabili kipa Juma Kaseja.
Kapombe ambaye aliumia katika tukio hilo, alitolewa kwa machela kabla ya penalti kupigwa na nafasi yake ikachukuliwa na beki wa kulia Issa Rashid 'Baba Ubaya', mabadiliko yaliyomlazimisha kocha Kim Poulsen kumhamishia Erasto Nyoni katika nafasi ya ulinzi wa kati iliyoundwa pia na Kelvin Yondani.
Ndikumana alipiga penalti hiyo kulia na kumpeleka "marikiti" Kaseja ambaye aliruka kushoto kwake katika dakika ya 52 na kuwa goli la ushindi lililoifanya Burundi kufuzu kwa hatua ya robo fainali kutokana na kufikisha pointi 6. Katika mechi yao ya awali ya Kundi B, Burundi walishinda 5-1 dhidi ya Somalia.
Licha ya kipigo, Stars imeendelea kubaki katika nafasi ya pili kutokana na pointi 3, ilizozipata kwa kuifunga Sudan 2-0 katika mechi ya ufunguzi wa kundi hilo Jumapili.
Sudan nayo imeendelea kubaki katika nafasi ya tatu licha ya jana kushinda 1-0 dhidi ya Somalia katika mechi ambayo Wasomali walionyesha kupambana kiume tofauti na mechi yao ya ufunguzi waliyopigwa 5-1 na Burundi.
Tanzania itamalizia hatua ya makundi dhidi ya Somalia saa 12:00 jioni Jumamosi wakati vinara Burundi watacheza dhidi ya Sudan mapema saa 10:00 siku hiyo. Timu mbili kutoka kila kundi kati ya matatu yaliyopo zinafuzu moja kwa moja hatua ya robo fainali na timu mbili zitakazoshika nafasi ya tatu zikiwa na matokeo mazuri zaidi zitakamilisha timu nane za robo fainali.
Kili Stars ilipiga mashuti mengi ambayo yalimweka 'bize' muda wote kipa wa Burundi wakati wakisaka goli la kusawazisha.
"Bahati mbaya" iliinyima Kili Stars goli la kusawazisha katika dakika ya 89 wakati kichwa cha mshambuliaji John Bocco 'Adebayor' kilipogonga 'besela' na kuokolewa juu ya mstari na beki wa Burundi.
Kocha Poulsen alisema timu yake ilikosa bahati tu kwani ililishambulia mfululizo lango la Burundi ambao baada ya kupata goli walirudi nyuma na kuweka "kuta" mbili za mistari ya mabeki
wanne wanne huku wakimuacha mchezaji mmoja tu mbele.
"Kama tutaendelea kucheza hivi tutafika mbali. Ni bahati tu iliyotunyima pointi leo. Pia napenda niwapongeze wenzetu kwa ushindi," alisema kocha huyo Mdenmark, ambaye pia alimpoteza kiungo wake Mwinyi Kazimoto kwa majeraha kutokana na kukanyagwa vibaya na mchezaji wa Burundi.
Kocha msaidizi wa Burundi, Amars Niyongabo, alikiri kwamba walilazimika 'kupaki basi' kuelekea mwishoni mwa mechi kwa kuihofia Stars ambayo iliwafunga wakati walipokutana kwa mara ya mwisho.
Kikosi cha Stars kilikuwa; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Amir Maftah, Shomary Kapombe/ Issa Rashid (dk. 52), Kelvin Yondani, Frank Domayo, Mrisho Ngassa, Salum Aboubakar 'Sure Boy', John Bocco 'Adebayor', Mwinyi Kazimoto/ Shaban Nditi (dk.69) na Simon Msuva/ Amri Kiemba (dk.36).

No comments:

Post a Comment