STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, November 29, 2012

Sharomilionea azikwa
*Waliomuibia kusakwa nyumba kwa nyumba
*Serikali yamlilia pamoja na Mlopelo, Maganga
mwili wa Sharo Milionea ukiingizwa kaburini jana










Na Lulu George na Steven William, Muheza
MAELFU ya waombolezaji walijitokeza jana kushiriki mazishi ya msanii muigizaji na mwimbaji Hussein Ramadhani Mkiety (Sharomilionea) yaliyofanyika kwenye kijiji cha Lusanga wilayani hapa huku baadhi yao wakipoteza fahamu.
Mazishi hayo yaliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na vyama vya siasa, wakiwamo Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Subira Mgalu na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, yalifanyika saa 7:00 mchana katika makaburi yaliyopo nyumbani kwa mama wa msanii huyo, kitongoji cha Jibandeni katika kijiji cha Lusanga wilayani Muheza, Tanga.
Wasanii mbalimbali nyota walihudhuria pia mazishi ya msanii mwenzao, baadhi wakiwa ni Amiri Athumani ‘King Majuto’, Singo Mtambalike ‘Richie’, Jacob Steven ‘JB’, Claudi, Wema Sepetu, Jacqueline Wolper, Hamisi Mwinjuma Mwana-FA, Muhogo Mchungu, Kingwedu na Dude.
Wengine waliofika kwenye msiba huo ni Mbunge wa Jimbo la Muheza, Herbert Mntangi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Muheza, Amiri Kiroboto na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Muheza, Ibrahimu Matovu na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM aliyekuwa akimwakilisha Rais Kikwete, Nape Nnauye .
Waombolezaji kutoka nje ya Muheza walianza kumiminika kijijini Lusanga tangu juzi jioni na shughuli za mazishi zilikuwa zikiongozwa na kamati iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Mkuu wa Wilaya, Mgalu.
Shughuli za ibada ya mazishi ziliongozwa na Sheikh Twaha Juma ambapo baada ya jeneza kutolewa ndani ya nyumba ya mama wa msanii huyo, liliwekwa uwanjani na kuswaliwa na waumini kutoka maeneo mbalimbali nchini kabla ya kupelekwa makaburini, eneo la umbali wa
mita 100 kutoka nyumbani kwao.
Mamia ya waombolezaji waliojitokeza walionekana kujawa na simanzi kubwa na baadhi yao, wakiwamo ndugu wa marehemu, walipoteza fahamu na kukimbiziwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Muheza.

DC ATOA SIKU MBILI
Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Subira Mgalu, aliwapa siku mbili (kuanzia jana) watu waliopora vitu vya marehemu Sharomilionea wakati alipopata ajali ya gari na kufariki dunia katika Kijiji cha Maguzoni wilayani hapa kuvirejesha mara moja kabla ya kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Mgalu aliyasema hayo wakati akizungumza mbele ya umati wa watu waliofika kushiriki mazishi ya msanii huyo yaliyofanyika katika Kijiji cha Lusanga ambako ni nyumbani kwa marehemu.
Mgalu alilaani kitendo hicho na kusema kwamba hakikubaliki hata kidogo kwani ni cha aibu na si cha kiungwana, hivyo wote waliohusika na wizi huo wajitokeze na kurejesha vitu vya marehemu.
Alisema kuwa Wilaya ya Muheza inapitiwa na barabara kuu na hivyo, wakazi wake wote wanapaswa kuwa wakarimu na kusaidia kwa upendo watu wanaopata ajali badala ya kujihusisha vitendo vya wizi dhidi ya wanaopatwa na ajali.
Alisema kuwa baada ya siku mbili, polisi wataendesha msako mkali wa nyumba kwa nyumba katika kijiji cha Maguzoni na kwamba, ni lazima wahusika wote watajulikana na kutiwa nguvuni.
Mgalu alitangaza hatua hiyo kutokana na taarifa kuwa mara tu baada ya Sharomilionea kupata ajali saa 3:00 usiku juzi na kufariki dunia, watu wasiojulikana waliuvamia mwili wake na kumuibia vitu vyote ikiwa ni pamoja na nguo alizovaa kabla ya kumuacha na soksi na nguo yake ya ndani tu.

SALAMU ZA RAIS KIKWETE
Nape aliyekuwa akimwakilisha Rais Jakaya Kikwete, alisema Serikali imeguswa na msiba huo na kwamba iko pamoja na wasanii katika kuomboleza kifo cha Sharomilionea.
Alisema Serikali inathamini kwa kiasi kikubwa mchango wa wasanii wakiwamo wa filamu, na kwamba iko nao katika kuwaendeleza.
“Rais amenituma nimwakilishe katika msiba huu… anasema binafsi ameguswa sana na msiba huu wa Sharomilionea kwani ni msanii ambaye alikuwa mbunifu na alikuwa akichipukia kwa hali ya juu katika fani ya uigizaji,” alisema Nape.
Alisema sasa ni wakati muafaka kwa wasanii hao kuungana na kuhakikisha kwamba jasho lao halipotei wala kunyonywa na wajanja wachache wa kati ambao kila siku wamekuwa wakinufaika huku wasanii wakiendelea kurudi nyuma.
Nnauye alisema mbali ya wasanii wa filamu pia wasanii wa fani nyingine nao wanastahili kuungana kuhakikisha jasho lao linawanufaisha na siyo mtu mwingine ili kujiletea maendeleo wao binafsi na familia zao kwa ujumla.
Nape alimkabidhi bahasha ya rambirambi ya msiba huo Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), Simon Mwakifwamba.
Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mgalu, pia alisoma salamu za rambirambi kutoka kwa mke wa Rais, Mama Salma Kikwete, ambaye Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA).

SERIKALI YAWALILIA
Wakati huo huo, Serikali imeelezea kusikitishwa na vifo vya wasanii watatu wa filamu nchini vilivyotokea mwezi huu vya waigizaji John Maganga, Halid Hemed ‘Mlopelo’ na Hussein Ramadhani Mkiety 'Sharomilionea'.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Waziri ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, misiba hiyo mitatu imeleta simanzi kubwa kwa serikali, familia, wasanii wenzao na wapenzi wa filamu na muziki kwa ujumla.
"Wasanii wote hawa ndiyo kwanza wameanza kung'ara katika tasnia ya filamu na sote tu mashahidi kwamba walianza kuleta matumaini makubwa katika kukuza na kuendeleza tasnia ya filamu na muziki, hususan muziki wa kizazi kipya. Lakini Ghafla wametutoka. tunasikitika sana kwa kuwa vifo hivi vimekuwa ni vya ghafla mno," alisema Dk. Mukangara katika taarifa hiyo.
"Hili ni pigo kubwa kwa taifa na jamii nzima, hasa wakati huu ambao serikali inafanya juhudi kubwa za kuhakikisha tasnia ya filamu na muziki zinakuwa rasmi.
"Serikali inatoa pole nyingi kwa familia, ndugu, jamaa na wote walioguswa na misiba hii. Ni imani ya Serikali kuwa wasanii wa tasnia hizi wataendeleza yote mazuri waliyoyafanya wenzao ili kuendelea kuwaenzi. 
"Serikali inaungana na familia na wapenzi wa tasnia yza filamu na muziki katika kipindi hiki kigumu.
"Kwa pamoja tuungani katika kuwaombea marehemu John Maganga, Halidi Mohamed na Hussein Mkieti wapumziko kwa amani. Mungu azilaze roho zao mahali pema Peponi. Amina," ilimaliza taarifa hiyo.



Baadhi ya waombolezaji katika msiba huo

King Majuto akiwa katika sura ya huzuni makaburini
Chanzo: NIPASHE

No comments:

Post a Comment