STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, December 29, 2012

RIDHIWANI APONDA MFUMO UENDESHAJI YANGA ADAI AFADHALI WA SIMBA

Ridhiwani akihutubia Waandishi asubuhi ya leo Kiromo Hotel

Na Mahmoud Zubeiry, Bagamoyo
MWENYEKITI wa Kamati ya Kusaidia timu za soka za vijana za taifa, Ridhiwani Kikwete, amesema mfumo wa uendeshwaji wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam ni mbovu kwa sababu unategemea mfuko wa mtu mmoja.
Akizungumza wakati anatoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), Hoteli ya Kiromo, Bagamoyo mkoani Pwani, Kikwete alisema kwamba Yanga inahitaji kubadilika kutoka mfumo huo.
Kikwete alisema ni afadhali mfumo wa uendeshwaji wa Simba SC, ambao desturi yao ni kuchangishana.
“Nilijaribu kufanya uchunguzi wa mfumo wa uendeshwaji wa klabu ya Yanga, nikashangazwa ni mfumo mbaya, kwa sababu unategemea mfuko wa mtu mmoja, afadhali Simba wao huwa wanachangishana,”alisema.
Ingawa hakumtaja mtu ambaye mfuko wake unategemewa Yanga, lakini wazi ni Mwenyekiti wa klabu hiyo, Alhaj Yussuf Mehboob Manji.
Kwa ujumla katika hotuba yake, Kikwete alisema haridhishwi na mfumo wa uendeshwaji wa soka ya Tanzania na kwamba unahitaji mabadiliko.
Kikwete aliushauri uongozi wa TASWA upiganie nafasi ya uwakilishi ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kusisitiza juu ya umuhimu wa waandishi nchini kutambua haki zao.
Lakini pia Kikwete aliwaasa waandishi kuepuka uandishi wa kinazi wa Simba na Yanga na badala yake kuzama ndani zaidi katika kuripoti, sambamba na kuripoti michezo yote, badala ya kuegemea kwenye soka pekee.
“Vyombo vya habari lazima viwe na wataalamu tofauti wa kuripoti michezo tofauti, huyu akiegemea kwenye soka, mwingine aegemee kwenye mchezo mwingine, ili kuhakikisha tunafikisha ujumbe vema kwa jamii,” alisema mtoto huyo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.
Ridhiwani ambaye pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, NEC akiiwakilisha Wilaya ya Bagamoyo alisema kwamba ipo haja ya TASWA kuendesha semina kadhaa za kuelimisha Waandishi wa Habari kuweza kuripoti michezo mbalimbali nchini.  
Aidha, katika mkutano huo, wanachama walielimishwa kuhusu uanzishwaji wa Saccos na kuridhia kuanza kwa mchakato wa kuundwa kwa chama cha ushirika wa akiba na mikopo kwa Taswa. Walipendekezwa wajumbe waunde timu ya mpito.

CHANZO:BIN ZUBEIRY

No comments:

Post a Comment