STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, January 13, 2013

Mashali amtwanga Mkenya na kutetea taji la EAC

Mashali (kulia) akimshambulia Mackoliech katika pambano lao la usiku wa jana
Mwamuzi Mark Hatia akizungumza na Mashali baada ya kumtwanga kwa konde lililomuangusha Mkenya sakafuni
 
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela akimvisha taji la ubingwa bondia Thomas Mashali baada ya kumtwanga kwa KO, Mkenya Benard Mackoliech.
BONDIA machachari wa ngumi za kulipwa nchini, Thomas Mashali, jana usiku aliendeleza rekodi yake ya 'kutopigika' baada ya kumnyuka kwa KO, Mkenya Benard Mackoliech na kutetea taji lake la Afrika Mashariki na Kati.
Mashali anayefahamika kama 'Simba Asiyefugika' alipata ushindi huo katika raunsi ya sita katika pambano hilo la uzito wa kati lililokuwa la raundi 10 lililofanyika kwenye ukumbi wa Friends Corner, Manzese jijini Dar es Salaam.
Mtanzania huyo tangu raundi za awali alionyesha dhamira yake ya kushinda pambano hilo kwa namna alivyokuwa akimpeleka puta mpinzani wake, japo Mackoliech alionyesha ubishi kabla ya kusalimu raundi ya sita.
Mwamuzi wa pambano hilo Mark Hatia, alilazimika kulimaliza pambano hilo katika raundi hilo baada ya kumhesabia Mkenya huyo baada ya kupigwa konde zito lililompeleka sakafuni na kushindwa kuinuka na kumpa ushindi Mashali.
Mara baada ya pambano hilo lililokuwa limeandaliwa na Promota Aisha Mbegu na kusimamiwa na Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania, TPBO, Mashali alivishwa mkanda wake na aliyekuwa mgeni rasmi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela.
Kenyela alimwagia sifa Mashali kwa kuipeperusha vema bendera ya Tanzania pamoja na kuwasifia waratibu wa pambano hilo lililosindikizwa na michezo kadhaa ya utangulizi iliyowasisimua mashabiki waliofurika ukumbini hapo.
Ushindi huo wa Mashali umemfanya afanikiwe kuendelea kulishikilia taji hilo la Afrika Mashariki na Kati alilotwaa Oktoba 14 mwaka jana kwa kumshinda kwa pointi bondia toka Uganda, Med Sebyala.
Pia imemfanya aendeleze rekodi yake ya kutipoteza mchezo wowote mpaka sasa tangu alipotumbukia katika mchezo huo wa ngumi za kulipwa mwaka 1999.

No comments:

Post a Comment