STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, January 13, 2013

Mgosi atuliza 'mzuka' JKT Ruvu, aanza kujifua nao

Mussa Hassani Mgosi

KIUNGO mshambuliaji nyota wa zamani wa Simba, Mussa Hassani Mgosi amewatuliza mashabiki wa timu anayoichezea kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, JKT Ruvu baada ya kutua na kuanza rasmi mazoezi.
Mgosi, alianza kuwapa hofu mashabiki na benchi la ufundi la JKT baada ya kutoweka nchini kwenda China kushiriki michuano maalum, huku kukiwa hakuna taarifa zake za kurejea wakati kikosi cha timu yake kikiwa kimeshaanza mazoezi.
Mfungaji Bora huyo wa zamani wa Ligi Kuu, alijiunga na wenzake kufanya mazoezi jana kwenye uwanja wa Mlalakuwa inapojifua timu yake hali iliyomfanya kocha wake, Charles Kilinda kutabasamu.
Kocha huyo alisema kurejea kwa Mgosi kumempa faraja kwani amepanga kumtumia katika mechi za mzunguko wa pili wa ligi hiyo inayotarajiwa kuanza rasmi Januari 26.
Kilinda alisema uwepo wa Mgosi pamoja na ushirikiano wa wachezaji wengine inamfanya aamini JKT Ruvu itafanya vema kwenye duru lijalo na kutimiza ndoto zao za kuwa miongoni mwa timu zitakazokuwa kwenye 'Nne Bora'.
Mgosi alishindwa kuitumikia kikamilifu timu yake hiyo katika duru la kwanza kutokana na kuchezwa kuletwa kwa ITC yake kutoka timu ya DC Motema Pembe ya DR Congo aliyokuwa akiichezea baada ya kuondoka Simba.
Mara baada ya duru la kwanza kumalizika, Mgosi alitimka China kushiriki michuano maalum iliyohusisha wachezaji kutoka nchi za Afrika, ambapo mkali huyo aliongoza kwa ufungaji mabao katika michuano hiyo.

Mwisho

No comments:

Post a Comment