STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, January 16, 2013

Mkina, Ochieng waiponza Simba

Mkenya Pascal Ochieng

WACHEZAJI Pascal Ochieng na Shija Mkina wameiponza klabu ya Simba baada ya uongozi wa mabingwa hao wa soka Tanzania Bara kutakiwa kufika mbele ya Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutoa maelezo kuhusiana na madai mbalimbali ya wachezaji hayo.
Mkenya Ochieng aliwasilisha barua katika ofisi za (TFF) Desemba 19 mwaka jana akiliomba shirikisho hilo kumsaidia kupata haki zake zikiwamo fedha zake za usajili, Sh. milioni sita na mashahara wake wa mwezi mmoja (Novemba 2012), ambao hata hivyo hakuwa tayari kutaja ni kiasi gani kwa madai kuwa ni siri yake na Simba.
Ochieng, ambaye alilazimika kuununua mkataba wake wa miezi sita na klabu ya AFC Leopards ya Kenya ili ajiunge na Simba, alinukuliwa akisema kuwa anaidai Simba dola za Marekani 8,000 (Sh. milioni 12.6) na kwamba hajapatiwa barua ya kuvunjwa kwa mkataba wake na klabu hiyo, hivyo anaamini kuwa bado yeye ni mwajiriwa wa ‘Wekundu wa Msimbazi’.
Kwa upande wake, Mkina ambaye hivi sasa anaichezea kwa mkopo klabu ya ligi kuu Bara ya Kagera Sugar (akitokea Simba), anadai Simba haijamlipa Sh. milioni sita zilizokuwa zimebaki baada ya kusaini mkataba nao kwa makubaliano ya Sh. milioni 10 na kwamba walimlipa fedha ya utangulizi Sh. milioni nne mwaka 2010.
Mkina pia anadai kuwa uongozi wa Simba umekuwa ukimzungusha katika malipo ya fedha zilizobaki na kwamba anawadai pia fedha za mshahara wake wa miezi mitatu (Septemba – Novemba, 2012).
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam jana, Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema kuwa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ili ilikutana jijini Dar es Salaam Jumamosi kupitia masuala mbalimbali yakiwamo madai ya wachezaji hao.
Wambura alisema kuwa baada ya kamati hiyo kupitia madai ya Ochieng na Mkina, iliamua kuzikutanisha pande zote (Simba na wachezaji wanaolalamika) ili iwahoji kwa pamoja Jumamosi ya Januari 19.
“Ni kweli tulipata barua za wachezaji hao. Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ilikaa Jumamosi iliyopita ikaamua kuwaita viongozi wa Simba na wachezaji wanaolalamika ili wahojiwe kwa pamoja Jumamosi,” alisema Wambura.
Baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Novemba mwaka jana huku timu yao ikifanya vibaya na kuangukia katika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo, viongozi wa Simba waliamua kusitisha mikataba ya baadhi ya wachezaji wao wakiwamo beki Ochieng na mshambuliaji Daniel Akuffor wa Ghana.

No comments:

Post a Comment