STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, March 12, 2013

Kivumbi cha Ligi Kuu kuendelea J'mosi, Yanga kunusa ubingwa?



Wachezaji wa Yanga wakifurahia moja ya mabao yao ya Ligi kuu

Na Boniface Wambura

KIVUMBI cha Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) kinatarajiwa kuendelea tena Jumamosi kwa mechi tatu kupigwa viwanja vya mikoa mitatu tofauti ya Mwanza, Dar es Salaam na Morogoro.
Timu inayopigana kuepuka kushuka daraja, Toto Africans itakuwa dimba la nyumbani la CCM Kirumba jijini Mwanza kuvaana na Mgambo JKT katika moja ya pambano linalosubiriwa kwa hamu wikiendi hii.
Toto walio nafasi ya pili kutoka mkiani wakiwa na pointi 15 na ikiuguza kipigo cha 'kaka' zao Yanga itakuwa na kiu ya kupata ushindi ili kuweza kujinasua mkiani na kujiweka katika nafasi za kuepuka kushuka daraja.
Pambano jingine la mwishoni mwa wiki ni kati ya vinara wa ligi hiyo, Yanga watakaokuwa dimba la Taifa jijini Dar es Salaam kuwakaribisha maafande wa Ruvu Shooting, mechi ambayo itatoa taswira ya mbio za ubingwa kwa Yanga ambao msimu huu wameonekana wapo tofauti wakiwa na kiu ya kutwaa taji.
Mpaka sasa Yanga inaoongoza msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 45 kutokana na mechi 19 ilizocheza ikifuatiwa na Azam waliopo nafasi ya pili na pointi zao 37 kisha Simba wanaokamata nafasi ya tatu wakiwa na pointi 34 wote pia wakiwa wamecheza mechi 19 kila mmoja.
Mtanange mwingine wa Jumamosi utazikutanisha timu zinazolingana pointi na kutofautiana uwiano wa mabo ya kufunga na kufungwa, Coastal Union ya Tanga watakaokuwa wageni wa Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa Manungu, Morogoro.
Mshindi yoyote wa mechi hiyo wataweza kufikisha pointi 34 na hivyo kuwakamata mabingwa watetezi ambao wenyewe watashuka dimbani siku ya Jumapili.

No comments:

Post a Comment