STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, March 12, 2013

Mwandi yahimiza wachezaji kuchangamkia African Youth

Moja ya timu za vijana ya Yosso United ya Arusha
WACHEZAJI wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara na Zanzibar wenye umri kati ya miaka 18 na 21 wametakiwa kuchangamkia fursa ya kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa Barani Ulaya, Asia na Afrika wakiwa nyumbani Tanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Kampuni ya Tanzania Mwandi, Teonas Aswile, waandaaji wa Michuano ya African Youth Football Tournament amesema kuwa katika michuano hiyo wachezaji 11 bora watatafutiwa timu moja kwa moja katika mataifa nane barani Ulaya (Ufaransa, Ureno, Uholanzi, Denmark, Norway, Sweden, Ubelgiji na Switzerland), Asia na Afrika.

Bwana Teonas Aswile amesema kuwa wachezaji wa Tanzania bado hawajaonesha muamko mkubwa licha ya kiwango cha chini cha kushiriki ambacho wamewekewa ikilinganishwa na wachezaji wa kigeni, ambao licha ya kuwekewa USD 500 bado wamezidi kumiminika.

“Mpaka sasa kuna mawakala wawili ambao tumezungumza nao na wamethibitisha kuleta wachezaji wao zaidi ya 20 kushiriki kwenye michuano.”

“Hii ni mbali ya wachezaji mmoja mmoja ambao tunaowasiliana nao ambao wanataka kuja, wakiwa zaidi ya watano. Kwahiyo wachezaji wetu waamke na kuitumia fursa hii ambayo haipo katika nchi nyingine ya Afrika kwa wachezaji kufanya majaribio nchini mwao.”

Aidha Aswile ameviomba vilabu mbalimbali ambavyo vinaweza kuwalipia wachezaji wake ada ya shilingi laki tatu (Tsh 300, 000) ambayo inahitajika kwa mchezaji ili aweze kushiriki kwenye michuano ya African Youth Football Tournament kufanya hivyo kwani mchezaji huyo atakapouzwa klabu husika ndiyo itakayokubaliana na klabu itakayomchukua na si Kampuni ya Tanzania Mwandi.

“Sisi tunachokifanya ni kumuwezesha mchezaji aone njia za kufikia malengo yake. Kwa hiyo akishafanikiwa na amepata timu ya kuchezea iwe Ulaya, Asia au Afrika, klabu yake ndio itakayokubaliana na timu ya huko sisi hatutachukua chochote”, Teonas alisema.

Mkurugenzi huyo akitaja idadi ya wachezaji wa Tanzania ambao tayari wamethibitisha kushiriki amesema kuwa ni wachezaji watatu jambo ambalo bado linaonyesha mwamko umekuwa mdogo.

Michuano ya African Youth Football Tournament itafanyika Tanzania katika uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 10 hadi 14 mwezi wa sita mwaka huu na kuwashirikisha wachezaji wenye umri wa miaka 18 hadi 21 ambapo watafundishwa na makocha watatu kutoka nje ya nchi na wawili wa Tanzania.

Pia michuano hiyo itashirikisha mawakala kutoka nchi nane za barani Ulaya, Asia na Afrika ambao wanahitaji wachezaji kwaajili ya klabu wanazoziwakilisha kati yao wakiwa ni Budak Johan, Cabrera Oliver, Dag Larsson, Phillip Mwakikosa na Dahlin Martin huku wakala wa kimataifa wa Tanzania Dr Damas Ndumbaro akiwa miongoni mwa mawakala wa Tanzania watakaoshiriki katika michuano kusaka vipaji kwaajili ya klabu mbalimbali.

“Tuna maombi ya mawakala wawili ambao wanataka wachezaji mabeki, washambuliaji na viungo kwaajili ya klabu zao Kuwait, Qatar, Libya na sehemu nyingine kwa hiyo hii ndio fursa ya wachezaji wetu kwenda kucheza soka la kulipwa na lenye maslahi zaidi kwao.”

No comments:

Post a Comment