STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, March 15, 2013

Stars, Morocco kuvaana kwenye jua kali

Hekaheka wakati mechi ya Taifa Stars na Morocco mwaka juzi

MECHI ya Kundi C ya kuwania kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia kati ya timu ya soka ya Tanzania (Taifa Stars) dhidi ya Morocco itakayofanyika Machi 24 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam itachezwa kuanzia saa 9:00 kamili mchana.
Akizungumza jana, Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Saad Kawemba, alisema kuwa lengo la kupanga muda huo ni kunufaika na hali ya hewa ya iliyopo (ya joto) kulinganisha na wageni (Morocco) ambao wachezaji wao wengi wanatoka barani Ulaya ambako baadhi ya maeneo yake hivi sasa yana baridi kali.
Kawemba alisema kuwa kwa sababu hiyo, watu wa benchi la ufundi wanaamini kwamba muda huo utawanufaisha zaidi Stars ambayo inaundwa na wachezaji wengi wanaoishi jijini Dar es Salaam na kuzoea hali ya joto la jua la mchana.
"Kule wanakotoka (wachezaji wa Morocco) hivi sasa kuna baridi kali na hivyo kwa muda huo kwetu tunaweza kunufaika," alisema kiongozi huyo ambaye aliongozana na kocha wa Stars, Kim Poulsen, kwenda mjini Marakech wiki iliyopita kuipeleleza Morocco iliyokuwa ikicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Mali.
Aliongeza vilevile kuwa Morocco wanatarajiwa kutua nchini Alhamisi (Machi 21) kwa ndege ambayo itapitia Dubai kabla ya kutua jijini Dar es Salaam.
Kikosi kitakachoivaa Morocco kinatarajiwa kuingia kambini Jumamosi lakini kitakuwa kamili ifikapo Jumanne baada ya nyota wake wawili wanaocheza TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu, watakapotua nchini siku hiyo pamoja na wachezaji wa Azam ambao watakuwa wamerejea nchini kutoka Liberia.
Katika kujiandaa na mechi hiyo Februari 6 mwaka huu, Stars ilicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Cameroon ambapo ilishinda bao 1-0.
Mbali na Stars kuivaa Morocco, mechi nyingine ya Kundi C itakuwa ni kati ya Ivory Coast watakaowakaribisha Gambia.
Stars yenye pointi tatu inahitaji ushindi ili kuendelea kuwa kwenye nafasi nzuri ya kufuzu katika kundi hilo linaloongozwa na Ivory Coast yenye pointi nne, Morocco (pointi mbili) na Gambia wanaoshika mkia wakiwa na pointi moja.
Tanzania haijawahi kufuzu fainali za Kombe la Dunia. Mara ya kwanza na ya mwisho Stars kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) ilikuwa mwaka 1980 ambapo Rais wa TFF anayemaliza muda wake, Leodegar Tenga ndiye aliyekuwa nahodha wake.

No comments:

Post a Comment