STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, March 15, 2013

Afisa habari CECAFA afariki dunia

Finny Muyeshi (kushoto) enzi za uhai wake (Picha: NATION)

AFISA Habari wa Shirikisho la Soka la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Finny Muyeshi, amefariki dunia juzi Jumatano usiku.
Akizungumza kwa njia ya simu jana kutoka Nairobi, Kenya, Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye, alisema kuwa marehemu Muyeshi alifariki akiwa kwenye hospitali ya Coptic iliyoko jijini humo.
Musonye alisema kuwa marehemu Muyeshi alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa figo ambao ndiyo umesababisha kifo chake.
Alisema kuwa CECAFA imepata pigo la kuondokewa na afisa huyo ambaye alikuwa ni mmoja wa watendaji wa sekretarieti kwa muda wote.
"Tumeondokewa na kiongozi wetu, ni pigo kwa CECAFA na ni pigo kwa soka la ukanda huu, alikuwa ni zaidi ya afisa habari katika maendeleo ya kila siku," alisema Musonye.
Aliongeza kuwa jana jioni alitarajia kushiriki kikao cha familia kwa ajili ya kupanga taratibu za mazishi ya kiongozi huyo.
Marehemu Muyeshi ambaye ni Mkenya ameitumikia CECAFA kwa zaidi ya miaka 10 akiwa ni msaidizi wa Musonye katika kusimamia mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) pamoja na michuano ya Kombe la Chalenji ambayo hufanyika kila mwaka katika ukanda huu.
Kutokana na kusumbuliwa na maradhi hayo, hakuweza kuitumikia CECAFA tangu mwaka juzi.
Kufuatia hali hiyo, Afisa Habari wa Chama cha Soka cha Uganda (FUFA), Rogers Mulindwa, alikuwa akikaimu nafasi hiyo.
Mungu aiweke roho ya marehemu mahali pema peponi. Ameen.


CHANZO:NIPASHE



No comments:

Post a Comment