STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, April 9, 2013

NI VITA NYINGINE ULAYA, DROGBA ANA KIBARUA KIZITO, DORTMUND KUVUNA NINI NYUMBANI?

Ronaldo wa Real Madrid

Didier Drogba wa Galatarasay
ISTANBUL, Uturuki
DIDIER Drogba na wachezaji wenzake wa Galatasaray wana mtihani mgumu leo wakati watakapojaribu kupindua matokeo ya kipigo cha 3-0 dhidi ya Real Madrid katika mechi yao ya marudiano ya robo fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.
Drogba, ambaye alishinda taji hilo msimu uliopita akiwa na Chelsea, ataingia akiwa na kumbukumbu nzuri ya kiwango cha juu alichoonyesha katika mechi yao ya ligi Jumamosi dhidi ya Mersin Idman Yurdu ambapo alifunga magoli mawili ya kipindi cha pili katika ushindi wa 3-1.
Hata hivyo, furaha ya ushindi huo wa Galatasaray iliingia doa wakati kocha Fatih Terim alipocharukia maamuzi ya refa yaliyosababisha yeye na wasaidizi wake wawili kutolewa kwa kadi nyekundu, na hivyo kutia wingu maandalizi ya mechi yao ya marudiano mjini Istanbul leo.
Mjini Madrid wiki iliyopita, Galatasaray walifundishwa "somo zuri" na klabu hiyo ya  Hispania, kwa mujibu wa Drogba.
"Sisi hatupo katika matawi yao lakini nadhani ni tatizo la ukosefu wa uzoefu zaidi kuliko jambo jingine lolote," Drogba aliiambia beIN Sport. "Tunajifunza, sisi ni timu changa. Kuna mambo tunayohitaji kuyaboresha.
"Ni somo zuri, na tunapaswa kuonyesha kwamba tumejifunza vyema katika mechi ya marudiano. Tulitaka kuwabana Madrid lakini  tungeweza kufanya jambo hilo kwa njia tofauti, kwa umakini zaidi na ungangari zaidi. Tungeweza kuwasababishia matatizo mengi kwa sababu tulipata nafasi lakini hivyo ndivyo ilivyo," alisema.
Pigo mojawapo kubwa kwa Galatasaray ni kukosekana kwa mshambuliaji muhimu Burak Yilmaz, ambaye ambaye amefungiwa kutokana na kupewa kadi ya pili ya njano mjini Madrid.
Vyombo vya habari vya Uturuki viliripoti Ijumaa kwamba klabu hiyo ya Istanbul iliwasilisha rufaa kwa UEFA ili kadi hiyo itenguliwe.
Galatasaray pia watamkosa beki wao wa kati Dany Nounkeu baada ya kuonyeshwa kadi ya njano ya pili mjini Madrid.

GOLI LA RONALDO
Real walitoa kipigo kikali cha 5-1 nyumbani dhidi ya timu ya katikati ya msimamo ya Levante Jumamosi wakati kocha Jose Mourinho alipowaanzishia benchi nyota wengi, akiwamo mshambuliaji Cristiano Ronaldo.
Ronaldo aliiangia akitokea benchi wakati wa mapumziko huku Real ikiongoza 2-1 na akafunga goli lake la 29 katika La Liga msimu huu kabla ya kumpikia jingine mtokea benchi mwenzake Mesut Ozil.
Beki wa kati Sergio Ramos na kiungo Xabi Alonso wote walicheza kwa dakika 90 kwa kuwa wamefungiwa mechi ya leo wakitumikia adhabu ya kadi.
"Itakuwa hivyo kwa sababu hivi sasa tuko katika kiwango chetu cha juu zaidi kwa msimu huu," Ronaldo, kinara wa mabao ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu huu akiwa na magoli tisa, aliwaambia waandishi wa habari. "Tuna kikosi kilichokamilika ambapo wachezaji wote ni wazima na hilo ni habari njema."
Kuhusu mechi ya leo mjini Istanbul, alisema: "Ni mechi ngumu na kusonga mbele kwetu kwenye raundi nyingine bado hakujawa na uhakika. Magoli matatu ni uongozi mrefu lakini ni lazima twende pale na tucheze na tupate japo goli moja.
"Ni lazima tufanya mambo hatua kwa hatua, mechi baada ya mechi, lakini nadhani tuna nafasi ya kufika fainali."

Pambano jingine litakalochezwa kwenye mfululizo wa mechi za ligi hiyo Borussia Dortmund itawaalika Malaga ya Hispania nchini Ujerumani kurudiana nao baada ya mechi iliyopita kuisha bila timu hizo kufungana. 
Wajerumani hao ambao wameshatemeshwa ubingwa wa ligi yao ya nyumbani Bundesliga baada ya vinara Bayern Munich kutwaa taji mwishoni mwa wiki itahitaji ushindi kurejea mafanikio ya 1997.

No comments:

Post a Comment