STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, April 9, 2013

NSA JOB MATATANI, MWENYEWE AAHIDI KUFICHUA SIRI

 
Nsa Job (kulia) alipokuwa Yanga

MSHAMBULIAJI wa Coastal Union ya jijini Tanga inayoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Nsa Job, ambaye wiki iliyopita alikiri hadharani kuwahi kupokea rushwa ya Sh. milioni 2 ili asiifunge moja ya timu kongwe nchini, amesema kwamba yupo tayari kutoa ushirikiano kama alivyoombwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili hatua zaidi zichukuliwe katika kukomesha rushwa kwenye mchezo huo nchini.
Hata hivyo, Job ambaye kwa sasa yuko nje ya timu yake baada ya kufanyiwa upasuaji katika goti lake, hakuwa tayari kueleza rushwa hiyo aliipokea wakati anaichezea timu ipi au mashindano gani.
Katika mechi hiyo, Job alifunga goli na timu yake hiyo aliyokuwa anaichezea ilishinda bao 1-0 na kupata pointi tatu muhimu.
Nyota huyo ameshawahi kuchezea timu mbalimbali za Ligi Kuu zikiwamo Simba, Yanga, Moro United, Villa Squad na sasa Coastal Union.
Akizungumza jana, Job alisema kuwa tayari ameshapokea barua kutoka TFF inayomtaka atoe maelezo kuhusiana na tuhuma hizo na yeye ameahidi atatoa ushirikiano bila kikwazo.
Job alisema kuwa ameamua kufanya hivyo ili kuonyesha ni jinsi gani soka la Tanzania linavyoendeshwa licha ya kuwapo kwa mipango mbalimbali ya maendeleo ya mchezo huo.
"Niko tayari kutoa ushirikiano wanaouhitaji na barua ya TFF niliipata tangu Ijumaa," alisema kwa kifupi nyota huyo ambaye alikataa kueleza ni wakati gani alipokea rushwa hiyo.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, jana alisema kuwa wanamtaka Job atoe maelezo kuhusiana na suala hilo pamoja na kituo cha redio cha Clouds ambacho kilirusha hewani mahijiano hayo Aprili 3 mwaka huu kupitia kipindi chake cha 'Amplifier' ili kupata nakala ya ushahidi.
Osiah alisema kuwa endapo Job hatatoa ushirikiano hatua kali dhidi yake zitachukuliwa na lengo ni kutaka kupambana kikamilifu na vitendo vya rushwa kwenye soka.
Alisema baada ya kupata vielelezo katika pande zote ambapo pia wanaomba wadau watoe ushirikiano ili kukomesha rushwa watalipeleka katika Kamati ya Nidhamu kwa ajili ya hatua za kinidhamu.
Osiah alisema kwamba licha ya nyota huyo kutoweka wazi ni kiongozi yupi alimpa fedha hizo, timu gani alikuwa akiichezea dhidi ya timu ipi, TFF imefikia hatua hiyo ili kutaka nidhamu iwepo na makosa yaliyowahi kufanyika huko nyuma yasirudiwe.
Nsa alidai kuwa baada ya kufunga goli katika mchezo huo kiongozi huyo ambaye hakuwa tayari kumtaja hadharani kwenye mahojiano hayo alikuwa akimfuata na kumtaka arudishe fedha alizopokea.

No comments:

Post a Comment