STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, May 9, 2013

Anayedaiwa kumbeba gaidi aliyelipua kanisa Arusha aanikwa


http://kiswahili.irib.ir/media/k2/items/cache/eee1ce1cd4a113d8297f55b6f0c96c4a_XL.jpg
Heka heka ilivyokuwa baada ya mlipuko wa Kanisa Arusha

KABLA ya Mei 5, mwaka huu, jina la Victor Ambrose (20), hakuwa akijulikana miongoni mwa jamii kubwa ya wakazi wa Jiji la Arusha. Hali kadhalika, kwa Watanzania wengi.

Lakini baada ya tarehe hiyo, jina lake lilianza kujulikana nchi nzima na pengine kimataifa kwa kuhusishwa na tukio la kigaidi la mlipuko wa bomu katika Kanisa Katoliki la Parokia ya Mtakatifu Joseph Mfanyakazi Olasiti jijini Arusha.

Parokia hii mpya awali ilikuwa ni kigango cha Parokia ya Burca, ambako ndiko pia yapo makazi ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Arusha, Josephat Lebulu, na uzinduzi uliotarajiwa kufanyika Jumapili iliyopita, ilikuwa ni kukipandisha hadhi kigango hicho kuwa parokia kamili.

Hali ilianza kwa shamrashamra, waumini wengi walionekana kuwa na nyuso za furaha, ghafla shamrashamra zao zilizimwa muda mfupi baadaye kabla ya uzinduzi wenyewe na hali ya simanzi ikatawala.

Tukio la mlipuko wa bomu kanisani hapo lilitokea siku ya kuzindua jengo la kanisa hilo, uzinduzi ambao ulikuwa umepangwa kufanywa na Balozi wa Vatican nchini, ambaye ni mwakilishi wa Baba Mtakatifu, Askofu Mkuu Fransisco Padilla, akishirikiana na mwenyeji wake, Askofu Mkuu Lebulu.

Hata hivyo, uzinduzi huo ulikatishwa kwa tukio la mlipuko wa bomu hilo ambao hadi sasa umesababisha vifo vya watu wanne na zaidi ya 66 kujeruhiwa.

Ilikuwa ni asubuhi muda ambao mvua zilikuwa zikinyesha, baadhi ya waumini wakipika chakula kwa ajili ya mlo wa mchana, huku ibada ikiwa ndiyo kwanza imeanza kwa Balozi Padilla, kupiga ishara ya msalaba na kubariki maji.

Umati mkubwa wa waumini kutoka parokia mbalimbali mkoani hapa, unaokadiriwa kufikia zaidi ya watu 2,000 hivi, ulikuwa umejitokeza kuhudhiria uzinduzi wa parokia hiyo.

Baada ya kubariki maji hayo, Askofu Mkuu Padilla, alitaka kunyunyiza maeneo mbalimbali na huku akiwa ameshika kifaa cha kunyunyizia, ghafla mtu mmoja ambaye bado hajakamatwa akiwa nyuma ya watu na nje ya uzio, alirusha kitu kinachoelezwa kuwa bomu kwenye mkusanyiko huo. Haijafahamika mlengwa alikuwa nani, lakini mtazamo wa wengi hauweki shaka kwamba mlengwa Askofu Mkuu Padilla.

VICTOR AMBROCE NI NANI?
Huyu ni dereva wa pikipiki maarufu kwa jina la bodaboda, kazi ambayo aliianza tangu aliposhindwa kuendelea na masomo yake ya sekondari mwaka 2011 akiwa amefikia kidato cha pili.

Alimaliza elimu ya msingi katika Shule ya Terrat, mwaka 2009, na  akaendelea na masomo ya sekondari katika Shule ya Oljoro, zote za mkoani Arusha.

Victor, anaelezwa na bibi yake, Lucia Victor, kuwa katika familia yao walizaliwa watoto wawili, yeye akiwa ni mtoto wa pili kwa wazazi wake ambao wote wawili walishatangulia mbele ya haki. Kaka yake anaitwa Philip.

Bibi Lucia, anasema tangu kufariki dunia kwa wazazi wake, amekuwa akiwalea watoto hao mpaka hapo walipofikia, na kwamba wanaishi eneo la Kwa Mromboo kama linavyotamkwa na wakazi wa Jiji la Arusha.

“Wazazi wa Victor wote walifariki dunia, na mimi ndiye nimekuwa mlezi wao tangu wakiwa watoto wadogo,” anasema Bibi Lucia.

Inasemekana kuwa jina la eneo hilo linatokana na mkazi mmoja  tajiri kutoka wilayani Rombo Mkoa wa Kilimanjaro.

Mzee huyo maarufu alikuwa na biashara nyingi ikiwamo baa aliyokuwa akiita Rombo, hivyo watu wakazoea kuita eneo hilo kwa jina hilo, lakini kutokana na asili ya watu wa huku kupenda kutamka majina kwa kurefusha, ndiyo maana badala ya kuita Kwa Mrombo wanaita Kwa Mromboo.

Bibi Lucia anasema familia yao pamoja na mjukuu wake, ni Wakristu wa madhehebu ya Katoliki. Anasema wanasali kwenye kigango cha Kwa Mromboo, cha Parokia ya Sombetini. Anamwelezea mjukuu wake kwamba hajawahi kumuona akinywa pombe, kuvuta sigara au kutafuna mirungi.

SIMULIZI KUTOKA KIJIWE CHA BODABODA:

“Tunamfahamu Victor, na hapa ndiyo kijiweni kwake,” anaeleza dereva mmoja wa bodaboda wakati NIPASHE ilipoanza kuulizia kijiwe chake kipo wapi na anaishi wapi. Hata hivyo, dereva huyo alikuwa na wasiwasi mkubwa hata kule kusema tu kwamba hapo ndipo palikuwa ni kijiwe chake, lakini mara kwa mara alikuwa akitaka kujua ni nani anayeongea naye.

Na baada ya kuelewana naye alianza kunielekeza eneo analoishi ingawa alisema hajui nyumba yake ni ipi isipokuwa eneo.

Dereva huyo alikuwa msaada kwangu kwani baadaye alinipa namba ya Mwenyekiti wake wa Jumuiya ndongo ndogo za Kikristo za Kanisa Katoliki na bila kusita nikampigia na kumweleza shida yangu.

Mwenyekiti huyo alikuwa mbali na eneo hilo kwa shughuli za ujenzi na akasema asingeweza kuwahi kwa muda huo, lakini alinielekeza na kufuata ramani hiyo niliweza kuifuata hadi nyumbani kwa Victor, kama vile unaelekea Oljoro.

Baadhi ya wenzake katika kijiwe hicho wanasema kuwa Jumapili Victor alikodiwa na mtu asiyemfahamu ampeleke kanisani na alikubali. Lakini baaada ya kufika, mkodishaji aliteremke na kukimbia bila kumlipa na kwamba wakati anamfuatilia amlipe fedha zake, ghafla ulitokea mlipuko.

Wanasimulia kuwa baada ya mlipuko huo hakumuona aliyemkodi zaidi ya kujikuta akiwa amevamiwa na watu waliokuwa karibu na eneo la kanisa hilo wakimgang’ania kuwa ndiye aliyefika eneo hilo na mlipuaji.

HALI ILIVYO NYUMBANI KWAKE

Majirani wachache na wote akina mama ndiyo waliokuwapo hapo. Ilikuwa nyakati za jioni na walikuwa wenye nyuso za wasiwasi.

Hali hiyo ilinifanya nianze kwa kuwapa pole na kuwafariji kwa yote yaliyotokea nao wakanikaribisha ndani na kuanza mazungumzo huku sauti ya nyimbo za kwaya ikisikika kwenye redio yao, baadhi yao walikuwa wakipika kuandaa chakula cha jioni.

Baadhi ya majirani walisema walipokea kwa mshangao tukio la kukamatwa kwa Victor kwa maelezo kwamba hakuwa wamesikia kama ana matatizo yoyote.

PAROKIANI ST. JOSEPH
Paroko wa Parokia ya Burca, Padri Peddy Castelino, ambaye kigango cha St. Joseph kipo kwenye parokia yake, anasema licha ya kutokea kwa tukio hilo, bado shughuli za misa zinaendelea kama kawaida asubuhi.

Wakatoliki wana kawaida kuadhimisha Misa Takatifu kila siku, maadhimisho ambayo Padri Peddy anasema wanayafanya kwa waumini wa kanisa hilo la St. Joseph.

Mazingira katika eneo hilo la kanisa yapo vile vile, huku walinzi wachache wa kanisa wakilinda viti na vifaa vingine vilivyotumika kwa siku ya uzinduzi. Meza, viti na vitu vingine vimeachwa hapo hapo na pia viatu vya watu vilivyovulika wakati wa purukushani navyo ni vimeachwa hivyo hivyo.

Hakuna ulinzi wa askari waliovaa sare au wale waliovaa kiraia huku wakiwa wameshika bunduki, lakini kwa mbali na eneo hilo kulikuwa na gari la polisi aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili PT 0591, hali inayoashiria kuwa ulinzi upo katika eneo hilo.

Akielezea mahusiano na majirani zao, Padri Peddy, anasema hawana ugomvi wowote  na majirani zao tangu waliponunua uwanja huo hadi kukamilika kwa ujenzi.
“Hatuna ugomvi wo wote na majirani zetu, tunaishi nao vizuri tu,” alisema.

BUNGE LAPITISHA AZIMIO KALI

Bunge limetoa azimio la kuitaka Serikali kuchukua hatua mara moja dhidi ya viashiria vya aina zote vya uvunjifu wa amani unaojitokeza kwa kuzifungia taasisi za dini zinazokashifu imani za dini nyingine.

Aidha limeitaka serikali kuziangalia sheria zote ili kudhibiti maneno yanayotolewa bungeni yanayoleta chokochoko na kusababisha kuhatarisha amani ya nchi.

Hatua hiyo imefikia wakati wabunge wakichangia maoni ya Azimio la Bunge kulaani tukio la kulipuliwa kwa bomu katika kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi Parokia ya Olasiti jijini Arusha, Mei 5, lililowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Anna Abdallah.

Akisoma na kujibu michango ya wabunge katika azimio hilo, Anna alisema wakati mwingine wabunge wanalewa na vipaza sauti kwa kuongea maneno ya uchochezi.
Alisema wabunge hawana mamlaka ya kuongea uchochezi na kuleta chokochoko zinazosababisha uvunjifu wa amani.
“Tumeanzisha wimbo watu wanaitikia huko nje.Hakuna demokrasia ambayo haina mipaka. Tutadhibiti jambo hilo kwa vinywa vyetu na matendo yetu.

Kama kuna vikundi vya dini vinaavyoanzishwa kwa ajiili kupinga kingine kwa nini vinaandikishwa.”


Aliongeza kuwa hivi karibuni kumekuwa na dalili za kuvunjika amani na utulivu uliojengwa na waasisi wa nchi tangu ilipopata uhuru kwa pande zote mbili za nchi.
Alisema dalili hizo za kuashiria kupotea kwa amani zimekuwa zikitolewa katika miaka ya hivi karibuni ambapo viongozi wa dini wamekuwa wakijeruhiwa na wengine kuuawa na baadhi ya nyumba za ibada kuchomwa moto.

Alisema hali hiyo imekuwa ikiwatia hofu wananchi wa imani na hali zote na kuhoji kiini cha matukio hayo na kwamba tukio la Arusha limeongeza hofu miongoni mwa Watanzania na kuelekea kutikisa misingi ya amani, utulivu na mshikamano miongoni mwa Watanzania.

Wakichangia Azimio hilo, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, alisema Wabunge wamekuwa wakitoa kauli kama mzaha, lakini wanaopokea ujumbe huo ndio wanaoathirika kwa kudhani ni za kupambana.

Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), alitahadharisha kuwa nchi ikienda mrama Watanzania watatafuta kwa kwenda.

“Kujitambua ni jambo muhimu sana. Je tunatambua thamani ya usalama wa nchi yetu. Je tunatekeleza wajibu wetu ipasavyo, serikali inatenda wajibu wake kwa mujibu wa katiba na sheria zake,” alihoji.

Mbatia alisema wanasiasa wanamkono mkubwa kwa yale yanatokea hivi sasa na kuwaonya wale wenye tabia ya kutaka madaraka kwa kutumia damu ya Watanzania.

Mbunge wa Mkanyageni, Habibu Mnyaa (CUF), alisema chokochoko hizi ni hatari kubwa kama kuna watu wanaoweza kujidanganya kuwa nchi hii kuna watu wanaweza kutumia kundi lao la waislamu kutawala nchi hii wanajidanganya na wale wanaofikiria wakristo ndio wanaweza kutawala peke yao wanajidanganya.

Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema (TLP), alisema enzi za uzoefu wake huko akiwa Naibu Waziri Mkuu, kazi kubwa aliyoifanya ilikuwa ni kuhakikisha nchi inakuwa na amani na utulivu.

“Kuna siku Nyerere alinipigia simu saa tatu usiku, kulikuwa na machafuko, akaniuliza Mrema umechukua hatua gani? Nikamuuliza mbona unanipigia mimi si kuna kiongozi wangu, Mwalimu alipoona jambo hakusita kutoa amri kwa wahusika kuchukua hatua,” alisema.

Alisema  kuna chokochoko nyingi zinazojitokeza upande wa mashekhe, mapadre, makanisani na misiskiti, pengine kwa kutoa vibali vya kuanzisha taasisi hizo bila kuwafuatilia.

“Kila mtu anaanzisha kikundi chake kwa kusema anahubiri imani, wanatukanana lakini hatuchukui hatua.

Tunaanzisha vikundi vinahatarisha amani halafu serikali inanyamaza. Wanaohubiri wana qualification (uzoefu)? Naomba mihadhara yenye mwelekeo wa uvunjifu wa amani ifungwe na wanyimwe leseni. Natoa siku saba kazi hiyo iwe imefanyika.” Mchungaji Getrude Rwakatare (Viti Maalum-CCM), alisema inasikitisha kwani inaonesha wazi kuwa upendo uliozoeleka kwanza umekwisha na sasa watu wanauana.

Alitaka viongozi wote wa dini kupendana na kuwa na umoja na kuhoji mambo ya chuki ya kugombana na kuuana yametoka wapi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira, alisema hakuna dini inayomuogopa Mungu inayoweza kuunga mkono kitendo kilichotokea Arusha.

“Hakuna dini, chama cha siasa kinachoweza kuunga mkono jambo lile na kuendelea kuishi.”

Wasira alisema Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kusema, “tumeshinda ukabila, lakini tuangalie udini utatusumbua siku zinazokuja.”
Alisema wakristo, waislamu, wote wanataka amani. Madhehebu yote yanataka amani na kwamba wanasiasa wakifanya wajibu wao wa kuhakikisha wanaongoza nchi yao yenye amani matukio haya hayawezi kutokea.

SABA WAHAMISHIWA MUHIMBILI
Wizara ya Maliasili na Utalii kwakushirikiana na Shirika la Hifadhi zaTaifa (Tanapa) wametoa ndege iliyotumika kuwasafirisha majeruhi saba kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kutokana na hali zao kutokuwa nzuri.

Hayo yalisemwa jana na Naibu Waziri wa Malisili na Utalii, Lazaro
Nyalandu, kwenye  Uwanja  wa Ndege wa Arusha wakati alipokuwa akisaidiana na ndugu jamaa na marafiki kuwaingiza wagonjwa kwenye ndege kuwapeleka Muhimbili.

Majeruhi hao ni Atanasia Reginarld (14), mwanafunzi wa kidato cha kwanza  Shule ya Sekondari Olasiti; Faustine Shirima (34); Gabriel Godfrey (9), mwanafunzi wa darasa la tatu Shule ya Msingi Lucky Vicent; Albert Njau (35 ); Jenipher Joacim; Apolinari Malamsha na Fatuma Tarimo walioletwa uwanjani hapa wakitoka Hospitali za St. Elizabeth na Mount Meru kwa kutumia magari maalum ya kubebea wagonjwa.

Naye Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mount Meru, Frida Mokiti, alishukuru wizara na wadau mbalimbali kwa msaada huo.

LIPUMBA ALAANI
Chama  cha Wananchi (CUF), kimelaani vikali na kusikitishwa na tukio la shambulizi la kigaidi la Jumapili.

Mwenyekiti wa Chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, aliitaka serikali kufanya uchunguzi wa kina na kuwa wazi katika kutoa taarifa kwa wananchi ambao wanataka kujua lengo na nia ya wapangaji na waandaaji wa matukio mbalimbali yanayotokea nchini.

Aliitaka serikali kutoa maelezo yanayojitosheleza kuhusu hatua madhubuti zinazoonyesha kubaini chanzo cha tatizo na suluhisho la muda mrefu ili wananchi wasipoteze imani dhidi ya serikali yao.

Aidha alitoa wito kwa Watanzania wote kutokubali matukio mbaya kuwagawanya katika misingi ya kidini.

Pia Profesa Lipumba alipongeza kauli Askofi Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Kardinali Polycap Pengo, kwamba suala zima la tukio la Arusha halihusiani na imani yoyote ya kidini.

  CHANZO:NIPASHE

No comments:

Post a Comment