STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, May 8, 2013

Askofu Pengo awatuliza Wakatoliki mlipuko wa bomu, vifo vyaongezeka







Askofu Pengo

Baadhi ya Majeruhi wa tukio hilo akihudumiwa

WATANZANIA wametakiwa kuwa watulivu na kuachana na hisia za kunyoosheana kidole kwamba wahusika wa shambulizi la kigaidi dhidi Kanisa Katoliki la Mtakatifu Josefu Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti, jijini Arusha Jumapili iliyopita kuwa ni Waislamu kwa kuwa watuhumiwa waliokwisha kukamatwa pia kuna Wakristo.

Kauli hiyo ilitolewa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, alipokuwa akizungumza kupitia kituo cha televisheni cha  Tumaini.

Askofu Pengo aliwataka wananchi kuacha hisia badala yake waache uchunguzi wa kubaini waliohusika uendelee ili kupata matokeo mazuri.
“Siamini kama waliofanya tukio hili baya ni Waislamu kwa kuwa watuhumiwa wanaoshikiliwa mpaka sasa wamo Wakristo, ni bora kuacha kuhisi,” alisema  Askofu Pengo.

Hii ni mara ya kwanza kwa Kardinali Pengo kuzungumzia shambulizi hilo baya la bomu ambalo limeibua hisia kali miongoni mwa jamii kwani ni kwa mara ya kwanza kanisa linapigwa bomu kwa mbinu zinazodhihirisha kuwa ni harakati za kigaidi.

WASAUDI WALIINGIA NCHINI MEI 4
Pengo akiweka msimamo huo, NIPASHE imefahamishwa kuwa raia wanne wa Saudi Arabia waliokamatwa kwa tuhuma za kuhusika ugaidi dhidi ya Parokia ya Olasiti, walilala katika hoteli moja iliyopo jirani na stendi kuu ya mabasi ya kwenda na kutoka mikoani.

Uchunguzi wa NIPASHE umebaini kuwa watuhumiwa hao waliingia nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) Mei 4, mwaka huu, na baada ya tukio la mlipuko wa bomu hilo walianza safari ya kutoroka nchini kupitia mpaka wa Tanzania na Kenya wa Namanga.

Habari zinasema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa na vyombo vya usalama karibu na maeneo ya mzunguko wa Forida katika barabara itokayo Mianzini kwenda katikati ya jiji.

VIFO VYAFIKA WATU WANNE
Katika hatua nyingine, majeruhi mwingine wa mlipuko huo, Isabela Michael (19), amefariki dunia katika Hospitali ya Mtakatifu Elizabeth, maarufu kama ‘kwa babu’ jana.

Taarifa  hizo zilizotolewa na Mganga Mkuu wa Hospitali ya St. Elizabeth, Goodluck Kwayu mbele ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu jana.

Kifo cha Isabela ambaye mama yake mzazi naye yupo mahututi hospitalini hapo, kinafanya idadi ya watu waliokufa kutokana na shambulizi kufikia wanne.

Juzi waliotajwa kufariki dunia ni Regina Longino Kurusei (45) na James Gabriel (16) pamoja na majeruhi mwingine ambaye jina lake halikutajwa.

Katika tukio hilo, zaidi ya watu 66 walijeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, Hospitali binafsi ya Selian na St. Elizabeth.

Akizungumza katika Hospitali ya Mount Meru baada ya kuwatembelea majeruhi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, alilaani tukio hilo na akawataka Watanzania kuwa tukio hilo lisiwagawe Wakristo na Waislamu.

Alisema Wakristo na Waislamu kwa miaka mingi wamekuwa wakishirikiana kama ndugu, hivyo ni vyema ushirikiano huo ukaendelea.

“Tukio hili lisitugawe Wakristo na Waislamu, tuna historia ya muda mrefu ya kushirikiana vizuri,” alisema.

Balozi Idd aliwataka Watanzani kuwa watulivu wakati vyombo vya ulinzi na usalama vikifanya kazi ya uchunguzi wa tukio hilo na kuwanasa wahusika.

MAALIM SEIF: TUMESIKITISHWA
Naye Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharrif Hamad, ambaye aliwatembelea majeruhi hao, alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na Chama cha Wananchi (CUF) wanalaani vikali tukio hilo.

“SMZ na CUF tumesikitishwa na kulaani tukio hilo la uhalifu na ugaidi wa hali ya juu kufanyika hapa nchini,” alisema.

Aliwaomba Watanzania kuwa watulivu na akawaomba wananchi ambao wana taarifa kuhusiana na watu waliohusika kwenye tukio hilo kutoa taarifa hizo kwa vyombo vya dola.

TAARIFA YA PINDA BUNGENI
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amesema tukio hilo si jambo la kushabikiwa kisiasa.
Alitoa kauli hiyo jana bungeni mara baada ya kurejea kutoka Arusha alikokwenda kutembelea eneo la tukio, baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda, kumpa nafasi ya kutoa taarifa fupi ya safari yake.

Alisema kwa bahati mbaya wapo baadhi ya viongozi wachache wanapitapita eneo la tukio na badala ya kutumia wananchi kuzungumza nao wanaingiza visiasaisa. “Naomba sana jambo hili tusilitumie kwa namna hiyo.”

Pinda alisema uchunguzi bado unaendelea, wamekamatwa watu wanane, wanne ni watu wenye asili ya kutoka Uarabuni, watatu ni Watanzania ambao wameanza kuhojiwa katika vuguvugu la jambo hilo.

Alisema raia wanne wa Kenya ambao walikamatwa ni kwa sababu tu ya kutaka kujiridhisha kwa kuwa wako Arusha siku moja kabla na siku ya tukio ndipo walipoanza safari ya kwenda Nairobi.

“Kwa sababu barabara zile zilikuwa zimeshafungwa, isingewezekana wao kupita kiurahisi bila kuhojiwa kwa maana ya kujiridhisha. Ni matumaini yetu kuwa pengine taarifa itatoka mapema leo (jana) au kesho (leo) kwa sababu wameanza tangu jana kuzungumza nao kama wanahusika kwa namna moja au nyingine.

Wengine bado uchunguzi na mahojiano yanaendelea.” Alisema alipofika Arusha alikuta wananchi wameshatulia na eneo la tukio palikuwa na utulivu, ingawa watu walihamaki, lakini wamefarijika na hatua za serikali za kufanya uchunguzi mara moja.

Alisema hospitalini katika majeruhi 66, walioruhusiwa ni 24 waliobaki wanaendelea kuuguzwa katika hospitali mbalimbali, wengi wao wapo Mount Meru.

Alisema sehemu kubwa ya wale walioathirika wameshafanyiwa upasuaji kwa ajili ya kutoa vipande vya vyuma vilivyokuwa vimewaathiri.

“Wengi tumewakuta wako katika hali nzuri, wengine leo (jana) watapelekwa katika chumba cha upasuaji na wengine inawezekana kesho (leo).”

Alisema wamewaomba madaktari vile vipande vya vyuma vikipatikana wasivitupe wakabidhi kwa vyombo vya dola ili waweze kubaini kama bomu lile la mkono limetengenezwa kienyeji au lililotengenezwa viwandani na kwa hiyo ni bomu linalotokana na jeshi. “Tutaweza kubaini chimbuko la bomu hilo ni nini.”

Wakati uchunguzi ukiendelea, Waziri Mkuu alisema wamewaomba wakazi wa Arusha yeyote mwenye taarifa ambazo zinaweza kusaidia za kubaini kwa uhakika juu ya nani kafanya jambo hilo na kwanini ajitokeze.

WABUNGE:  AMANI KWA GHARAMA YOYOTE
Baadhi ya wabunge wamewataka Watanzania kuungana, kuepuka tofauti zao za kiitikadi, dini na viongozi kunyoosheana vidole ili amani ilindwe kwa gharama yoyote.

Wakichangia mjadala wa hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi jana, wabunge wengi waliochangia mjadala huo walisema  tukio la Arusha limeishtua nchi na dunia na  kilichotokea huko si utamaduni, desturi na jambo lililozoeleka kwa Watanzania.

Waliwaomba Watanzania wajikumbushe yaliyotokea Rwanda kwani mgogoro ule kwa kiasi kikubwa ulisababishwa na kauli. Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), alisema ni mambo ya kusikitisha kwa kuwa taifa ni la Watanzania.

Alisema janga likitokea inabidi Watanzania wote bila kujali imani, dini wala itikadi wawe wamoja.

“Amani inabidi ilindwe kwa gharama yoyote ile. Chochoko zilizozama miongoni mwa Watanzania kwa kauli za baadhi ya viongozi na Watanzania,” alisema.

Alisema Serikali haina dini na kila mtu ana imani yake ya dini, lakini leo unaweza kumpigia kiongozi wa serikali, hata askari simu mlio wake ni wa nyimbo za dini.

“Ningeomba kuanzia leo milio ya simu ya dini tuiondoe inasambaratisha Watanzania. Tuko wapi na tunaipeleka wapi. Naomba kwa moyo wa dhati mihadhara ya kidini iliyodumu kwa zaidi ya miaka 20 tuseme basi imetosha,” alisema.

Alihoji serikali inashindwaje kufanya maamuzi huku akinukuu maneno ya falsafa yanayosema ukiona maovu yanatokea, kemea, zuia. Alisema ukumbi wa Bunge ni baraza, lakini limefanywa la matusi.

Alishauri Watanzania wawe na utulivu na watafakari pamoja.

“Watanzania, viongozi wa dini tusiwe wepesi kuonyesheana vidole, mauaji ya padre, viongozi wamekata tamaa, wamesema sasa tumechoka.

Tusiwaruhusu viongozi wetu watupeleke huko,” alisema na kuongeza: “Ndimi zetu kauli zetu zitaliangamiza taifa la Tanzania. Tumefika mahali Tanzania tuseme basi.”

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsa Vuai Nahodha, akichangia mjadala huo alisema, ni kawaida kwa viongozi kulaumiana na kumtafuta mchawi.

Alisema viongozi wenye busara kama hawa hawapaswi kulaumu watu linapotokea tatizo kama hilo. Alisema ajenda iliyopo mbele ni tatizo la kuvurugika kwa amani.

“Huu si wakati wa kulaumiana ni wakati kujenga mshikamano wa kuwatafuta waliohusika na tukio hili.”

Alisema sifa ya uongozi ni kukubali ukweli hata kwa mambo ambayo hawayapendi. “Kuna mahali sisi viongozi tumekosea. Unaposikiliza mijadala ya wabunge, wakati mwingine kauli zetu haziashirii mema. Na hatuwezi kushangaa haya yanayotokea,” alisema.

Aliongeza kuwa kiongozi anaposema jambo ni lazima apime kwani Tanzania ni nchi changa ina miaka 50 tu na kutokana na kiwango cha elimu na uwezo wa kuchanganua mambo ni mdogo.

“Tujikumbushe yaliyotokea Rwanda. Mgogoro ule kwa kiasi kikubwa ulisababishwa na kauli.

Waswahili husema watu makini na wenye busara hujifunza. Najua ni ngumu sana mwanadamu kubadilika na kuacha mambo ambayo ameyazoea,” alisema.

Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema), alisema tukio la Arusha limeishtua nchi na kilichotokea Arusha siyo utamaduni, desturi na halijazoeleka kwa Watanzania.

“Nitoe wito kwa wabunge na Watanzania wote kuwa huu si wakati wa kutupiana lawama.

Katika jambo hili lazima tuhakikishe kwamba tunashirikiana kurejesha utulivu katika jiji la Arusha. Lazima tuchunge ndimi zetu, viongozi pamoja na sisi wananchi.

Tuanzie hapa bungeni. Hakuna sababu ya kuanza kunyoosheana vidole, kwamba jambo hili ni la kisiasa au la kidini. Mwenye kuhisi hivyo ashirikiane na tume ya uchunguzi kuwabaini,” alisema.

Alisema sheria zimetungwa na zipo, lakini kuna woga wa kuzitumia. Mtu mwenye uhakika kwamba ni la kidini au la kisiasa kwa nini asitoe ushahidi?”

Aliongeza kuwa jambo hili linafundisha kuwa nchi haiko salama, Watanzania wamegawanyika kwa sababu hiyo ni rahisi kutumiwa na maadui.

“Baadhi yetu tunasema jambo hilo limesababishwa na kundi fulani. Hatuko salama. Hakuna mashehe au maaskofu wanaotengeneza makundi kutukana wenzao.

Lakini naamini kuna kundi la wahuni wanaofanya hivyo. Sababu gani hawakamatwi, tunawaogopa nini. Nyinyi polisi ndiyo mnatoa vibali vya mikutano ya kutukana watu. Kwa nini watu hawa hawakamatwi?” alihoji.

Alisema watu wamefikia hatua ya kusimama hadharani na kushambulia kuwa chama hiki ni cha Waislamu, chama hichi ni cha Wakristo. Serikali ionyeshe ipo na weledi wake.
Aidha, alitaka Serikali itunge sheria ya kudhibiti lugha za uchochezi kwenye mikutano na majukwaa.

Mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndassa, alisema kutokana na matukio yanayotokea hivi sasa kuna haja ya kuimarisha ulinzi kwenye eneo la jengo la Bunge.

Alimwambia Spika wa Bunge kuwa asije kushangaa siku moja Bunge lake tukufu linavamiwa na wahuni.

“Arusha kusingekuwa na ulinzi wa kutosha hata wale waliohusika wasingekamatwa.
Kuanzia sasa huku nyuma (bungeni) mtu akirusha kitu kitafika ndani.

Watu kule nje wanatuona tunavyozungumza na tunavyosigana humu ndani. Lazima ulinzi uimarishwe,” alisema na kuongeza: “Tuzime moto kabla moto haujalipuka, anayechokozwa,  huchokozeka.”

Aidha, alipendekeza makomandoo wa Jeshi la Polisi, waongezewe muda wa kustaafu ili kutoa uzoefu kwa vijana.

Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Chiku Abwao , alihoji kuhusu uchunguzi wa kutekwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda, na kwamba serikali imefikia wapi kuhusiana na suala hilo.

Hamad Ali Hamad (CUF-Magogoni), alisema chama chake kimewagharimu muda mwingi kuwaambia Watanzania kuwa si chama cha kidini, lakini ilikuwa ikitumiwa kama propaganda ya kukiua.
Naibu Waziri wa Serikali za Mitaa, Tawala za Mikoa (Tamisemi), Aggrey Mwanry, alisema adui anaigawa Tanzania.

Alisema Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, aliposema nchi hii haina dini watu hawakumuelewa.

“Taifa hili likienda likateketea, sisi hatutaacha kulaumiwa. Hapa imezungumzwa habari za dola, hiki ni chombo cha kundi ni chombo kinachoangalia tabaka. Dola ni chombo cha mabavu, akifika anabamiza. Kiwango cha mabavu kinategemea na kiwango kitakachokutwa sehemu ya tukio,” alisema.

Alisema ikifika mahali kwamba nchi haitawaliki maana yake unafika kwenye shamba la mtu unavuna mahindi unaondoka, unaenda sokoni unachukua samaki wa watu unaondoka bila kulipa, hapo ndipo utasema nchi haitawaliki.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Samia Hassan Suluhu, alisema vitabu vyote vya dini havina maamrisho ya kuvuruga imani ya mwenzie.  “Kinachozungumzwa ndani ya ukumbi wa Bunge ni kizuri, lakini kinachotokea nje kinasababishwa na sisi wenyewe,” alisema.

Alisema amani ni kama uzi wa hariri, hivyo Watanzania wasiukate, ukikatika vinginevyo watashindwa kuunga.

Waziri Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika, alitaka polisi kuchapa kazi yao kwani hata nje ya nchi wanasifiwa. Alisema baadhi ya wanasiasa wanafanya kazi ya polisi kuwa ngumu.

“Kauli zetu wanasiasa tuchunge maslahi ya nchi hii, anayesema mtu huyu ni mhalifu tunamtia hatiani ni kazi ya mahakama,” alisisitiza.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisema Jeshi la Polisi litatimiza wajibu wake pamoja na kufanyakazi katika mazingira magumu.
Alisema ukiona mtu anaichukia polisi, lazima ujiulize ana nini.


CHANZO:NIPASHE

No comments:

Post a Comment