STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, May 14, 2013

Casillas wa Mtibwa aikana Simba

Kipa Husseni Sharrid 'Casillas' akiwa mazoezini
GOLIKIPA wa kutumainiwa wa klabu ya Mtibwa Sugar, Hussein Sharrif 'Casillas' amekanusha ripoti kwamba yupo mbioni kujiunga na Simba mwisho wa msimu huu.
Sharrif alisema taarifa kwamba ameshakutana na baadhi ya viongozi wa Simba ili kumalizana nao anazisikia na kuzisoma kwenye magazeti na mitandaoni tu, lakini hakuna kitu kama hicho.
Akizungumza na MICHARAZO jana, kipa huyo aliyeng'ara msimu huu kiasi cha kuitwa na kocha Mdenmark Kim Poulsen katika kikosi cha timu ya taifa (Taifa Stars), alisema hajui uvumi huo unatokea wapi wakati hajawahi kukutana wala kuzungumza na viongozi wa Simba.
"Hakuna kitu kama hicho siyo kiongozi wa Simba wala wa Yanga ambao nimewahi kukutana na kuzungumza nao juu ya mustakabali wangu wa soka kwa msimu ujao, sasa sijui hizi taarifa zinatokea wapi. Mimi ni mchezaji wa Mtibwa na nitabaki Mtibwa," alisema Sharrif.
Alisema kwa sasa akili yake ipo katika mechi yao ya mwisho dhidi ya JKT Ruvu ili kuisaidia Mtibwa imalize katika Nne Bora ili ifuzu kucheza Ligi ya Super8.
"Suala la usajili kwa sasa halipo kichwani kwangu, nawaza namna nitakavyoisaidia Mtibwa Sugar imalize msimu vizuri," alisema Sharrif.
Kipa huyo ni miongoni mwa wachezaji 30 walioitwa kwenye kikosi cha Young Taifa Stars kitakachotumika kupata wachezaji wa kuitumikia Taifa Stars, ambayo wakati ikijiandaa na pambano lao dhidi ya Morocco kipa huyo pia alijumuishwa japo hakucheza.
Sharrif aliyewahi kung'ara na Villa Squad kabla ya kunyakuliwa Mtibwa Sugar, amelazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya kuzagaa habari kupitia vyombo vya habari kwamba alikuwa katika mipango ya kuhamia Msimbazi baada ya kuzibania Simba na Yanga kwenye ligi msimu huu.

No comments:

Post a Comment