STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, May 18, 2013

Leo ndiyo leo, Simba au Yanga leo Taifa?

Wekundu wa Msimbazi watawapa nijni mashabiki wao kwa Yanga leo?

Vijana wa Jangwani wataweza kulipa kisasi kwa Simba leo Taifa?
LICHA ya kwamba ni pambano la kuhitimishia ratiba tu na hakuna kitakachoweza kubadilisha matokeo kwa timu hizo mbili kwa msimu huu wa 2012-2013, lakini upinzani wa jadi ulioppo baina ya Simba na Yanga ndiyo unaolifanya pambano lao la leo kwenye uwanja wa Taifa kuwa na msisimko mkubwa.
Tambo za timu hizo kutoka kwa viongozi, makocha na wachezaji mbali na mashabiki na wanachama wao kwa karibu wiki mbili mfululizo, wengi wanataka kuziona zinahitimishwa vipi baada ya dakika 90 za mtanange huo ambao utachezeshwa na mwamuzi, Martin Saanya.
Yanga ambao wameshatwaa taji la Ligi Kuu msimu huu wakiwanyang'anya watani zao hao wameapa kutoa kipigo kwa Wekundu wa Msimbazi ili kunogesha sherehe zao za ubingwa, wakati Simba wakipania kuwavurugia sherehe hizo.
Viongozi na makocha wa pande zote mbili wameelea matumaini yao kwa pambano hilo la leo wakiamini kwamba vikosi vyao vitaibuka na ushindi na kuzima ngebe za wapinzani wao.
Yanga wenyewe watashuka dimbani wakitokea visiwa vya Pemba wakati watani zao wanatokea Unguja walipokuwa wameenda kuweka kambi kujiandaa na mechi hiyo ambayo inasubiriwa kwa hamu na mashabiki wakikumbushia pambano kama hilo la msimu uliopita kuwa na matokeo ya aina yake.
Jangwani waliokuwa kwenye mgogoro mkubwa kati ya wanachama na viongozi wao waliaibishwa kwa kunyukwa mabao 5-0 na Simba na kunyang'anywa taji lao huku wakiongezewa idadi ya deni la vipigo baada ya kushindwa kulipa kisasi cha mabao 6-0 walichopewa tangu mwaka 1977.
Safari hii Yanga wapo vyema wana amani na utulivu na wameshanyakua taji la ubingwa mapema, tofauti na wapinzani wao ambao ni hivi karibuni hali imerejea kuwa shwari klabuni kwao.
Simba iliyo chini ya kocha Patrick Liewig kutoka Ufaransa inapewa nafasi kubwa ya kuizima Yanga inayonolewa na Mholanzi, Ernie Brandts kutokana na rekodi nzuri iliyowekwa na kikosi chake cha vijana waliopewa jukumu baada ya 'mafaza' kudengua na kuenguliwa kikosi cha Mfaransa huyo.
Hata hivyo Yanga wanapewa turufu zaidi kwa uimara wa kikosi chao na reklodi yao ya kutopoteza mechi yoyote katika duru zima la pili na mwaka mzima wa 2013 mpaka sasa, huku safu yake ya mbele ikiwa kama wembe na safu yao ya ulinzi kuwa kama zege kwa kutopitika kirahisi.
Lakini kwa soka la Simba na Yanga lenye kila aina ya mbinu lolote linaweza kutokea na pengine burudani wanayoisubiria mashabiki wa timu hizo na soka kwa ujumla kushindwa kuipata kwa nama timu zilivyokamiana.
Timu zote zina wachezaji wazuri wenye vipaji na uwezo mkubwa wa kufanya lolote muda wowote na katika eneo lolote la uwanja, hivyo mashabiki wanapaswa kusubiri kuona kipi kitakachotokea baada ya filimbi ya mwisho ya mwamuzi Saanya toka Morogoro na wasaidizi wake.
Katika pambano la raundi ya kwanza timu hizo zilitoshana nguvu kwa kufungana bao 1-1 na Simba itaingia uwanjani leo ikiwa na kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kiungo wao nyota na aliyekuwa mfungaji wa moja ya mabao yaliyoizamisha Yanga Mei 6 mwaka jana , Patrick Mutesa Mafisango alipofariki kwa ajali ya gari Mei 17, 2012 ambapo inaelezwa wachezaji watavaa vitambaa vyeusi kama ishara ya kumkumbuka.
Pia mashabiki maalum wameandaliwa kwa mechi ya leo wakiwa na jezi namba 30 aliyokuwa akiivaa mchezaji huyo kama ishara ya kumuenzi mkali huyo kutoa DRC, ingawa alikuwa pia na uraia wa Rwanda.
Mbali na pambano hilo la Taifa pia leo kuna mechi nyingine sita katika viwanja vingine zitakazofungia msimu huu, huku masikio na macho ya mashabiki yakielekezwa kwenye mechi inazozihususisha timu zinazopigana kuepuka kushuka daraja inazozihusisha timu za Polisi Morogoro, Toto Africana na Mgambo JKT.
Toto wenyewe watakuwa uwanja wa nyumbani CCM Kirumba kuwakaribisha Ruvu Shooting, kama itakavyokuwa kwa Polisi Morogoro watakaokuwa Jamhuri, Morogoro kuumana na Coastal Union ya Tanga kadhalika Mgambo JKT watakuwa uwanja wa Mkwakwani kuumana na African Lyon iliyoshuka daraja.
Matokeo yoyote ya viwanja hivyo vitatu vitatoa picha halisi ya timu zipi mbili za kuungana na Lyon kucheza Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao na kuzipisha rasmi Ashanti United, Mbeya City na Rhino Rangers zilizopanda daraja.
Mechi nyingine za leo za kuhitimishia msimu ni JKT Oljoro watakaowakaribisha washindi wa pili wa ligi hiyo, Azam kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, JKT Ruvu wataumana na Mtibwa Sugar uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam na Prisons Mbeya itaialika Kagera Sugar katika uwanja wa Sokoine Mbeya.
Je, ni Simba au Yanga itakayocheza leo Taifa ama ni Toto, Polisi na Mgambo itakayoungana na Lyon? Tusubiri.

No comments:

Post a Comment