STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, May 18, 2013

Ugaidi? Watano wanaswa na vifaa vya milipuko Dar


https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgTqetlsLeH_ScYXsPtt6WO1C0fCX-TowGb2uhPjHn6Tr5y1FeOFQlW2IKA6Gvj_SbkIxEdBwIkNjl_C_wq6S1VMWROlSa0pU8X4P2JHsx_PisWpU2abyDZBphoYSSGa0JX6_sKaf-j_NY/s1600/Kova1%252814%2529.jpg
Kamanda Kova

WAKATI  hofu ya ugaidi iliyotanda Jijini Arusha hivi karibuni haijatulia, Jeshi la polisi nchini linawashikilia watuhumiwa watano, akiwamo mwanamke mmoja baada ya kuwanasa na vifaa vya milipuko mbalimbali ya hatari eneo la Kunduchi Mtongani jijini Dar es Salaam.

Watuhumiwa hao ni Juma Khalifani (24), Ruben Patrick (26), Happy Charles (28), Sadick Self (32) na Iddi Shaban (40) wote ni wakazi wa Kunduchi Mtongani.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini,  Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Sulemain Kova, alisema kupitia oparesheni yao walifanikiwa kuwakamata wahalifu hao ambao walikuwa na milipuko hatari kinyume cha sheria.

Alisema kuwa watuhumiwa hao hawana uhalali wa umiliki wa vifaa hivyo hali ambayo iliwapa shaka zaidi juu ya suala hilo.

Kamanda alisema watuhumiwa hao baada ya kukamatwa walifanikiwa kuwakuta na nyaya 62 za milipuko zikiwa zimefungwa betri, vifaa vya kusababisha milipuko zikiwa nane (Supreme Plain detonator), nyaya ndefu mizunguko minne, mabomba 20 ya urefu wa sentimenta 30 ambazo zilijazwa mbolea ya urea na tambi rola moja.

Kova alisema vifaa hivyo ni hatari vikiunganishwa vinaweza kuhatarisha maisha ya watu pamoja na mali zao.

Pia alisema milipuko hiyo hutumika kupasulia miamba na kwamba jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi zaidi ili kujua madhumuni halisi ya watuhumiwa hao katika kumiliki vifaa saidizi na milipuko hatari.

Hata hivyo, alisema katika tukio hilo walifanikiwa kukamata dawa za kulevya aina ya bhangi gunia moja.

Kamanda Kova alisema wanashikilia gari aina ya Noah iliyosajiliwa kwa namba T.772 BYC pamoja na bajaji ya miguu mitatu yenye namba T959 BTE ambazo zimekamatwa zikiwa nyumbani kwa mtuhumiwa Sadick Seif ambaye alishindwa kuthibitisha uhalali wa kumilki  vyombo hivyo vya usafiri.

Alisema baada ya upelelezi kukamilika watuhumiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani.
Aidha Kamanda Kova amewataka watu ambao wanatumia milipuko hiyo kujisalimisha kwa haraka lasivyo watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria za usalama za nchi.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema kuwa wamejipanga vyema katika suala la oparesheni ili kuwakamata wahalifu wote.

Alisema katika mkoa wake kuna matapeli wa aina mbalimbali na kwamba hivi karibuni kuna watuhumiwa walimtapeli raia wa kichina kumuuzia kiwanja ambacho tayari kilishatolewa hati ya uhalali kwa mtu mwingine.

Kenyela alisema katika tukio hilo wanamshikilia wakili mmoja wa kujitegemea kuhusika katika utapeli huo na kwamba atafikishwa mahakamani hivi karibuni.

Alisema tatizo jingine ni kuwepo kwa raia wa kigeni kuingia nchini bila kuwa na kibali hali ambayo inasababishia kuhatarisha usalama na kwamba tayari wameshachukuliwa hatua.

Pia aliwataka wananchi kutoa taarifa dhidi ya watu wahalifu ili waweze kuchukuliwa hatua

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment