Amri Kiemba akishangilia moja ya mabao yake uwanjani |
KIUNGO
mshambuliaji wa timu za Simba na Taifa Stars, Amri Kiemba amewashukuru
waandaji wa tuzo za Mwanasoka Bora Tanzania, Chama cha Wachezaji Soka
Tanzania (SPUTANZA) kwa kumpa heshima hiyo ambayo haikutarajia baada ya
kutoka kwenye kipindi kigumu ndani ya klabu yake.
Akizungumza
na MICHARAZO mchana huu, Kiemba alisema heshima aliyepewa na SPUTANZA ya kuwa
Mwanasoka Bora kwa mwaka 2013, imemfanya ajisikie fahari na kutambua
kuwa wapo wanaokubali mchango wake katika soka la Tanzania.
"Nimefurahi
kwa kutwaa tuzo hii ya Sputanza, hata kama maandalizi yake yalikuwa ya
haraka haraka, lakini siku zote mwanzo mgumu na ninawapongeza na
kuwashukuru, nikiamini kwamba mchango wangu unathaminika kwa wadau,"
alisema Kiemba.
Kiemba, alisema anaamini tuzo hiyo ni changamoto kwake kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara inayotarajiwa
kuanza Agosti 24 mwaka huu.
"Kunyatua
tuzo hii ni changamoto kwangu kwa msimu ujao, watu watapenda kuona
nafanya kitu gani baada ya msimu uliopita kung'ara, lakini yote kwa yote
namuachia Mungu kwani yeye ndiye mpangaji wa kila jambo," alisema
Kiemba baba wa watoto wawili, Shaaban na Amri Kiemba Jr.
Kiungo
huyo aliyewahi kung'ara na timu za Kagera Sugar, Yanga na Miembeni
amenyakua tuzo hiyo baada ya kung'ara msimu uliopita akiifungia Simba
mabao 8 na pia kuipigania Stars kwenye mbio zake za kuwania Fainali za
Kombe la Dunia za mwakani, japo Tanzania imekwama.
Kabla
ya kurejea kwenye kiwango kilichowavutia makocha na mashabiki wa soka,
Kiemba alikaa nusu msimu wa 2011-2012 bila kucheza kupinga maamuzi ya
uongozi wa Simba kumtoa kwa mkopo kumpeleka timu ya Polisi Dodoma ambayo
ilikuja kuteremka daraja mwishoni mwa msimu huo.
Mbali na Kiemba tuzo hizo za SPUTANZA pia ilinyakuliwa na Salum Abubakar 'Sure Boy' wa Azam kama Mchezaji Bora Chipukizi, Hussein Sharrif 'Casillas' (Kipa Bora) na kocha Mecky Mexime wa Mtibwa aliyetangazwa kuwa Kocha Bora wa Mwaka.
No comments:
Post a Comment